Wise Mgina ashinda uwenyekiti Kamati ya Madiwani Ludewa

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, Bakari Mfaume amemtangaza Diwani mteule wa Kata ya Mundindi, Wise Mgina kuwa mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Madiwani kwa kupata kura 19 kati ya 32 zilizopigwa na madiwani hao huku mshindani wake, Edward Haule akipata kura 13,anaripoti Damian Kunambi (Diramakini) Njombe.

Akitangaza matokeo hayo baada ya uchaguzi huo, Mfaume amesema nafasi hiyo iligombewa na madiwani hao wateule wawili ambapo katika nafasi ya makamu mwenyekiti imechukuliwa na diwani mteule wa Kata ya Mawengi, Leodgar Mpambalyoto ambaye alikuwa mgombea pekee na amepigiwa kura za ndiyo 18 na hapana 14.

Ameongeza kuwa, katika nafasi ya katibu wa kamati hiyo iligombewa na madiwani wawili Diwani wa Masasi, Daudi Mhagama ambaye amepata kura 18 na diwani mteule wa kata ya Lifuma, Michael Haule ambaye amepata kura 14 na kupelekea Daudi kuwa katibu wa kamati ya madiwani na Michael kuwa naibu katibu wake.

Aidha, baada ya uchaguzi huo Mwenyekiti wa kamati hiyo aliyepitishwa Wise Mgina amewashukuru madiwani wote na kuwaomba kushirikiana naye katika masuala mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.


Amesema, nafasi hiyo ataitendea haki katika kuleta maendeleo, hivyo wakazi wa Ludewa wanapaswa kuwapa nafasi ya kufanya maendeleo viongozi wote waliopitishwa ndipo wawapime uwezo wao wa uongozi.

Ameongeza kuwa, kumekuwa na maneno mengi katika makundi mbalimbali ya mitandao ya kijamii yanayounganisha wakazi wa Ludewa yakijadili uchaguzi wa 2025 kitu ambacho si chema sana kwa kipindi hiki kwani viongozi walioteuliwa bado hawajaanza utendaji wao.


"Si vyema kuanza kuwajadili na kuwatolea kasoro viongozi waliopitishwa na kuanza kujadili uchaguzi ujao, tunaomba mtupe nafasi ya kuwaonyesha uwezo wetu kiutendaji ndipo mtujadili,"amesema Wise.

Naye Mbunge wa jimbo hilo, Joseph Kamonga amewaomba wabunge wote kuwa na ushirikiano ikiwemo kumshirikisha katika changamoto mbalimbali zinazowasilishwa kwao kutoka kwa wananchi ili kuweza kuzitatua na kuzijadili kwa pamoja.

"Mimi ni mbunge wa wote hivyo kila Diwani anapaswa kuwa huru kunishirikisha changamoto zilizopo ndani ya kata yake na kuzitafutia ufumbuzi,"amesema Kamonga.

Post a Comment

0 Comments