NBC yavutiwa na mipango ya maendeleo, Rais Dkt.Mwinyi awapongeza

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kuimarisha sekta mbalimbali za maendeleo na kukuza uchumi wa nchi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya NBC Tanzania,Theobald Sabi akiongoza ujumbe wa benki hiyo walipokutana na Rais leo Desemba 3, 2020 katika Ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).

Rais Dkt.Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo Desemba 3, 2020 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na uongozi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, Theobald Sabi akiwa amefuatana na Meneja Uhusiano William Kallaghe na Ramadhan Lesso ambaye ni Meneja wa Tawi la NBC Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameueleza uongozi huo kwamba amefarajika kwa kiasi kikubwa na utayari wa benki hiyo katika kuunga mkono juhudi za Serikali na kusisitiza kwamba watawapa ushirikiano wa hali ya juu kwani lengo ni kuwahudumia wananchi.

Amesema kuwa, hatua hiyo itasaidia katika kuendeleza yale yote ambayo walielezwa wananchi wakati wa kampeni ili kuweza kuyafanyia kazi na kuhakikisha wananchi hao wanapata faraja katika kutimiziwa ahadi zilizoahidiwa. 

Ameongeza kwamba, kwa sasa Serikali ipo katika kutayarisha maeneo ya ndani na nje na baadae kuyapambanua yale ya kushirikiana na sekta binafsi na yale ya kushirikiana na sekta ya umma.

Rais Dkt.Hussein amesema kuwa, msaada huo wa gari maalum la kuchukulia wagonjwa utasaidia hasa kwa akina mama na watoto katika kuhakikisha juhudi za kupambana na vifo vya akina mama na watoto zinafanikiwa na kupatiwa ufumbuzi wa uhakika. 

Aidha, ameipongeza azma ya benki hiyo ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya afya. Sambamba na hayo, Rais Dkt. Hussein ametoa angalizo kwa uongozi huo kwamba ni vyema pale wanapotaka kutoa misaada yao wakakutana na wataalamu wa sekta wanayotaka kuiunga mkono ili iwe rahisi katika kufikia malengo waliyoyakusudia. 

Amesema kuwa, Serikali iko tayari katika kushirikiana na benki hiyo katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya afya, elimu na nyinginezo.

Pamoja na hayo, Rais Dkt.Hussein ametoa shukurani kwa pongezi zilizotolewa na benki hiyo pamoja na Bodi na wafanyakazi wake za kumtakia kila la kheri kufuatia ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi mkuu uliopita. 

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Taifa ya Biashara, Theobald Sabi alimpongeza Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa niaba ya benki hiyo, Bodi ya Wakurugenzi pamoja na wafanyakazi wake kwa kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu uliopita na kumuahidi kumpa ushirikiano katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2020-2025. 

Aidha, Mkurugenzi huyo alimemueleza Rais Dkt.Mwinyi historia ya benki hiyo ambayo imeanza rasmi mwaka 1967 na kwa upande wa Zanzibar shughuli zake zilianza rasmi mnamo mwaka 1969 huku akieleza kwamba imekuwa ikipata ushirikiano mzuri kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea ilipoanzishwa benki hiyo.

Ameeleza kuwa, benki hiyo ilitoa hisa kwa Benki ya Afrika Kusini (Absa Group Limited) kwa asilimia 55, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 30 ya hisa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) kama mwanachama wa Benki ya Dunia ilipata asilimia 15. 

Uongozi huo ulieleza kuwa uko tayari kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Nane katika kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa azma ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Ameongeza kuwa, benki hiyo iko tayari kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuanza kutoa mchango wake kwa kuipa Wizara ya Afya gari la kubebea wagonjwa pamoja na kuchangia dawa za binaadamu. 

Ameeleza kwamba, ni utaratibu uliowekwa na Benki hiyo ya NBC kutoa huduma za afya kwa kupitia gari kusaidia jamii kwa kuwasaidia wagonjwa kuwapeleka hospitali katika mikoa mbalimbali hapa Tanzania jambo ambalo wameona haja ya kutoa huduma hiyo kwa upande wa Zanzibar. 

Amesema kuwa, miongoni mwa kazi ya benki hiyo ni kutoa huduma za kliniki za biashara kwa wafanyabiashara wakubwa na wale wa kati kupitia ushirikiano huo kati ya ubia wa benki hiyo na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), kutoa huduma mbalimbali za ukusanyaji fedha na huduma nyingine za kibenki kwa wateja wake pamoja na utoaji wa mikopo na mafunzo kwa wajasiriamali sambamba na kutoa elimu ya kibenki nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news