Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wakuu wa mikoa wapya wa Zanzibar kuwa na utaratibu maalum unaotambulika wa kusikiliza kero za wananchi pamoja na kuzitafutia ufumbuzi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais Dkt.Mwinyi ametoa ushauri huo leo Desemba 3, 2020 Ikulu jijini
Zanzibar katika hafla ya kuwaapisha wakuu wa mikoa wapya, watakaohudumu
katika mikoa mitano ya Zanzibar.
Walioapishwa ni Ayoub Mohamed
Mahamoud wa Mkoa Kaskazini Unguja, Rashid Hadid Rashid wa Kusini Unguja,
Idrissa Kitwana Mustafa wa Mjini Magharibi, Salama Mbarouk Khatib wa
Kaskazini Pemba pamoja na Mattar Zahor Masoud wa Mkoa wa Kusini Pemba.
Amesema,
viongozi hao wana jukumu la kuandaa utaratibu maalum utaowawezesha
wananchi kuwasilisha kero mbalimbali zinazowakabili na kuzipatia
ufumbuzi wa haraka, huku akiwataka kutokuwa sehemu ya kero hizo kwa
kigezo kuwa wapo baadhi ya viongozi wanaojihusisha katika migogoro
mbalimbali ikiwemo ya ardhi.
Aidha, amewataka viongozi hao kuondokana na utamaduni wa kuoneana aibu
au muhali, pamoja na kuwataka kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo
iliyopo katika mikoa yao hata kama miradi hiyo inatekelezwa na wizara za
Serikali.
“Mradi wowote unaofanyika katika mkoa wako ni mradi
wako una jukumu la kufuatilia hata kama unatekelezwa na wizara,"amesema
Rais Mwinyi.
Amesema, viongozi hao wana jukumu la kuhakikisha
miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika na kumalizika kwa
wakati, akibainisha kuwepo miradi kadhaa ikiwemo wa ZUSP (unaogharimu
dola dola milioni 93) ambao utekelezaji wake hauridhishi kwa msingi kuwa
umetekelezwa chini ya viwango katika maeneo mbalimbali.
Dkt.Mwinyi
amewataka wakuu hao wa mikoa kujiridhisha iwapo miradi inayotekelezwa
katika mikoa yao inaendana na thamani halisi ya fedha zilizotumika.
Sambamba na hayo, amewataka viongozi hao kuzifuatilia kwa karibu
Manispaa na halmashauri zilizopo mikoani mwao kutokana na utendaji wa
kazi usioridhisha, kiasi cha kushindwa hata kukusanya taka pamoja na
kusimamia makusanyo ya fedha.
Aidha, amesema pamoja na kuwepo
miradi ya wizara katika mikoa yao, wana jukumu la kubuni miradi mipya
ili kutekeleza kwa vitendo ilani ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na
kumtaka kila mmoja kuwa sehemu ya utekelezaji kwa vitendo ahadi
alizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita.
Akigusia
suala la uwajibikaji kwa watendaji, Rais Dkt. Mwinyi amewakumbusha
viongozi hao wajibu walionao katika kuwasimamia wafanyakazi wao ili kila
mmoja aweze kutekeleza wajibu wake na kuhakikisha huduma bora
zinatolewa kwa wananchi, akibainisha kuwepo dhuluma,manyanyaso na
udhalilishaji kwa wananchi.
Vile vile ametaka kuwepo mifumo bora
ya ukusanyaji mapato ili yaweze kutatua matatizo mbalimbali katika
sehemu zinazohusika, sambamba na kuwataka kuwa wabunifu, kuondokana na
urasimu na kusisitiza umuhimu wa kusimamia vyema dhamana zao katika
taasisi zote za ukusanyaji mapato.
Katika hatua nyingine, Dkt.Mwinyi amewataka viongozi hao kupiga vita rushwa na kuondoa ubadhirifu katika matumizi ya mali za serikali, sambamba na kuondoa wizi katika maeneo mbalimbali , huku akisema makusanyo na fedha za bajeti zimekuwa zikipotea sana.
Aidha, amesema kuna changamoto kubwa katika suala la utiaji saini mikataba ya miradi mbalimbali nchini, ikiwemo ile ya wizara za Serikali ambapo Wizara ya Fedha imekuwa ikihodhi jukumu hilo.
Amesema, hakuna ulazima kwa wizara hiyo kuingia mkataba katika kila mradi wa wizara, akibainisha hatua hiyo inaviza utendaji kutokana na ufuatiliaji duni, akitolea mfano wa mradi wa mashine ya MRI katika Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja iliyoshindwa kutengenezwa kwa wakati kwa vile mkataba wake ulisainiwa na Wizara ya Fedha.
“Inatia mashaka kila mradi mkataba wake lazima uingizwe na Wizara Fedha,”amesema.Akiahidi kufuatilia utendaji wa wakuu hao wa mikoa hao, Dkt.Mwinyi aliwataka kufanya kazi kwa utaratibu mpya wa ubunifu na utatuzi wa kero za wananchi ili kila senti ya serikali iweze kutumika vizuri.
Mapema, Dkt.Mwinyi amewakumbusha viongozi hao jukumu linakowakabili katika kusimamia mikoa kuwa sio jambo dogo, hivyo akawataka kutekeleza wajibu huo kwa kujituma ili kutekeleza vyema Ilani ya CCM pamoja na kuondoa kero mbalimbali za wananchi.
Aidha, amewashauri wasichelewe kujifunza majukumu yao na kufanya kazi zinazowakabili, akitaka kuweka kipaumbele suala la ulinzi na usalama kwa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama.
Amewataka kusimamia kikamilifu Manispaa na hamashauri ziliopo mikoani mwao, akibainisha kuwepo mapungufu makubwa katika usimamizi.
Nao wakuu wa mikoa mitano ya Zanzibar, walisema wameajianda kutekeleza kikamilifu majukumu yote ya kazi zao, ili kufikia malengo yaliokusudiwa.
Viongozi mbalimbali wa kitaifa wamehudhuria katioka hafla hiyo, akiwemo Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdalla, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Abdulahamid Yahya Mzee, Mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Dkt.Mwinyi Talib Haji, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid,Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Viongozi wa Idara maalum za Serikali ya Zanzibar pamoja wanafamilia.
