Bernard Kamillius Membe ang'atuka ndani ya ACT Wazalendo

Mheshimiwa Bernard Kamillius Membe ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati wa Serikali ya Tanzania Awamu ya Nne chini ya Mheshimiwa Rais mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete na baadaye kutangaza kujiondoa katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo mwaka 2020 ameamua kujiuzulu nyadhifa zote, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Membe ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa wanadiplomasia mahiri amefikia uamuzi huo leo Januari Mosi, 2021 licha ya kuwa na hadhi kubwa ndani ya chama hicho ikiwemo kupewa nafasi ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ulifanyika Oktoba 28, 2020, na kura zake zikawa finyu.

Uamuzio huo ameufikia huku pia akiwa na cheo cha Mshauri wa chama hicho ambacho wakati wa hatua za mwisho za uchaguzi ilionekana yeye kuacha kabisa kufanya kampeni huku hali ya vuta ni kuvute ikitawala baina ya viongozi wa juu wa chama hicho.

Mheshimiwa Membe ametangaza uamuzi huo akiwa nyumbani kwake katika Kijiji cha Rondo Chiponda kilichopo Wilaya ya Mtama mkoani Lindi.

Amesema,hajafanya uamuzi huo kwa shinikizo lolote na kwamba kwa sasa atakuwa mshauri wa masuala mbalimbali yanayoihusu nchi ya Tanzania na kupigania demokrasia ya kweli.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamemueleza Mwandishi Diramakini kuwa, Mheshimiwa Membe ana nafasi kubwa ya kushirikiana na Serikali kwa hadhi aliyokuwa nayo kuendelea kulijenga Taifa katika nyanja mbalimbali ikiwemo kisiasa, kiusalama, kidplomasia na kijamii. 

"Maamuzi ya Mheshimiwa Membe kung'atuka ndani ya ACT Wazalendo yanapaswa yaheshimiwe na kila mmoja, jambo moja jema ni kwamba, kila mmoja atambue kuwa siasa si uadui, siasa ni kama daraja la kuwaunganisha wenye maono chanya kwa ajili ya kuleta hamasa zenye msisimko wa maendeleo kwa umma, hivyo Membe bado ana nafasi nzuri na kubwa ya kuwatumikia Watanzania," ameeleza Mchambuzi huyo katika mahojiano na Mwandishi Diramakini. 

Awali Mheshimiwa Membe akiwa kijijini kwake amesema kuwa, “Wiki tatu zilizopita nilitangaza kwamba ifikapo Januari Mosi, 2021 nitajiuzulu nafasi yangu ya ushauri mkuu wa ACT-Wazalando na uanachama wa chama hicho kwa mpigo.

“Ninatumia haki yangu ya kikatiba kujiuzulu kwenye nafasi yangu ya ushauri mkuu ya chama na uanachama wa ACT-Wazalendo kwa hiari yangu mwenyewe bila kulazimishwa wala kutishiwa na mtu yeyote na bila kuadhirika na jambo lolote. 

“Ibara ya 105 kifungu kidogo cha kwanza kinasema mwanachama atakoma kuwa mwanachama na atajiuzulu iwapo atatangaza hadharani kwamba anajiuzuli au ataandika barua kwa viongozi wa chama na mimi nimefanya yote mawili,"amesema Membe.

Ameongeza kuwa alishamwandikia barua Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe kuhusu uamuzi wake huo. Kwani alijiunga rasmi na ACT Wazalendo Julai, 2020 na baadaye kuteuliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho, lakini alianza kutofautiana na viongozi wenzake baada ya kusitisha kampeni za urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news