Rais Dkt. Mwinyi ataja mambo matatu ya kuipaisha Zanzibar kiuchumi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa baada ya kupatikana amani na umoja nchini kilichobaki hivi sasa ni kuendelea kuhubiri uwajikaji katika sekta za umma na sekta binafsi ili kuleta maendeleo ya haraka, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Imam Sheikh Omar Abeid wa Masjid Afra Binti Issa Kidongochekundu Wilaya ya Mjini wakati alipowasili katika Masjid hiyo leo Januari Mosi, 2021 kushiriki sala ya Ijumaa. (Picha na Ikulu/Diramakini).

Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo wakati akiwasilimia waumini wa dini ya Kiislamu huko katika Masjid Afraa Bint Issa (Msikiti Shurba), Kidongochekundu Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja mara baada ya kujumuika nao katika Sala ya Ijumaa. 

Katika salamu zake kwa waumini wa Msikiti huo pamoja na wananchi wote kwa jumla, Alhaj Dkt. Mwinyi amesisitiza haja ya kuwajibika kwa kila mtu kwa nafasi yake aliyonayo kwa lengo la kuleta maendeleo yaliyokusudiwa. 

Akieleza mambo matatu muhimu ambayo yakifuatwa yataleta maendeleo ikiwemo amani, umoja na suala zima la uwajibikaji, Alhaj Dkt. Mwinyi amesisitiza kwamba kila mmoja anapaswa kuwajibika kwa nafasi aliyonayo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya Swala ya Ijumaa katika Masjid Afra Binti Issa Kidongochekundu Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi. (Picha na Ikulu/ Diramakini). 

“Anayekushanya kodi akusanye maana asipokusanya hatuwezi kuwa na fedha za kuleta maendeleo, anayetakiwa kuzoa taka azoe vinginevyo miji itakuwa michafu, aayetibu hospitali atoe huduma nzuri kwa wagonjwa na aliyekuwa skuli atoe elimu bora, sote tukiwajibika maendeleo makubwa tutayapata”, amesisitiza Alhaj Dkt. Mwinyi. 

Katika maelezo yake Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kuwa akiwa kiongozi tayari ameanza kuchukua hatua dhidi ya mambo ambayo yanarudisha nyuma hatua za kuleta maendeleo nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi (wa tano kulia) akijumuika na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa iliyoswalishwa na Sheikh Khalid Ali Mfaume (mbele) katika Masjid Afra Binti Issa Kidongo chekundu Wilaya ya Mjini wakati alipowasili katika masjid hiyo leo kushiriki sala ya Ijumaa. (Picha na Ikulu/ Diramakini).

Amesema kuwa, wapo watu ambao hawatoridhika na hatua hizo anazozichukua ambazo ni muhimu katika kuleta nidhamu ya utumishi wa umma na nidhamu ya uwajibikaji na nidhamu ya kuhakikisha kwamba fedha za Serikali ni vyema zikatumika kwa watu wote na sio kwa mtu binafsi. 

Hivyo, amewataka waumini kuendelea kumuombea dua kwani wapo ambao hawatoridhika na wapo watakaoridhika na hatua hizo hivyo dua zao ni muhimu kutokana na lengo lililopo la kuwatumikia wananchi kwa kadri matarajio yao yalivyo.

Alhaj Dk. Mwinyi ametoa shukurani kwa viongozi wa dini kwa kuendelea kuwaunga mkono mara zote wanapochukua hatua zenye lengo la kujenga. 

Sambamba na hayo, Alhaj Dkt. Mwinyi amewasisitiza wafanyakazi wote kwa nafasi walizonazo wawajibike ipasavyo ili maendeleo zaidi yaweze kupatikana. 

Rais Alhaj Dk. Mwinyi ametoa shukurani kwa wananchi na waumini wote kwa kuiitikia wito wa kudumisha amani ambalo ni miongoni mwa mambo matatu aliyoyataja na kutoa shukurani kwa wananchi kwa kuidumisha katika kipindi chote cha Uchaguzi Mkuu. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Husseinn Ali Mwinyi (kushoto) akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya Swala ya Ijumaa katika Masjid Afra Binti Issa Kidongochekundu Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi. (Picha na Ikulu/ Diramakini).

Alhaj Dk. Mwinyi amesema kuwa, katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu watu waliombwa kuwachagua viongozi wanaowataka ambapo kila aliyechagua alikuwa na matumaini na kiongozi anayemtaka kwa lengo la kuleta maendeleo. 

Aidha, katika mambo hayo matatu aliyoyaeleza Alhaj Dkt. Mwinyi ni umoja ambapo amesisitiza kwamba hatua ya kudumisha umoja imesaidia kwa kiasi kikubwa kawni hapo siku za nyuma haukuwepo hatua iliyopelekea mfarakano kutokana na imani za kisiasa jambo ambalo lisingeweza kuleta maendeleo. 

Alhaj Dkt.Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wote kwa kudumisha umoja na kueleza kwamba kwa upande wao viongozi wa kisiasa wameshaanza kuchukua hatua kwa kuanza kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa lengo la kuwaunganisha watu na kuleta umoja nchini kwa azma ya kuleta maendeleo. 

Alhaj Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wote kuendeleza tunu ya amani na umoja ili kuweza kupata maendeleo. 

Ameongeza kuwa waumini walimuomba Mwenyezi Mungu kuleta amani na umoja ambapo hivi sasa vyote hivyo vimepatikana na kusisitiza kwamba kazi iliyobaki ni kuleta maendeleo na wale waliokuwa bado hawajakubaliana na hali ya umoja waendelee kuwaelisha. 

Mapema akisoma hotuba ya Ijumaa, Sheikh Omar Bin Abeid amesisitiza haja kwa waumini wa dini ya Kiislamu kusimamia maadili ya uongozi huku akitumia fursa hiyo kueleza hatua anazozichukua Alhaj Dk. Mwinyi katika suala zima la uwajibikaji kuwa ni sehemu ya kutekeleza majukumu yenye tija katika umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news