Bilioni 5.799/- kutekeleza miradi minne ya maji Songea

Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma inatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 5.799 kutekeleza miradi nane ya maji katika kipindi cha mwaka 2020/2021, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mradi wa maji Kijiji cha Lituta Halmashauri ya Madaba ambao unagharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili.

Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Songea, Mhandisi Mathias Charles amesema hadi kufikia Januari mwaka huu RUWASA Wilaya ya Songea imepokea zaidi ya shilingi milioni 877 sawa na asilimia 15.12 ya bajeti iliyopangwa. 

“Hadi kufikia Januari 2021 wakazi wanaopata huduma ya maji wilaya ya Songea wanakadiriwa kuwa 132,362 sawa na asilimia 63.6 ya wakazi wote,’’amesema Charles. 

Hata hivyo amesema hadi sasa mamlaka hiyo imetumia zaidi ya shilingi bilioni tatu kutekeleza miradi tisa ya maji katika wilaya hiyo na kwamba RUWASA inaendelea na kazi ya uboreshaji wa huduma ya upatikanaji wa maji kwa kujenga miradi mipya. 

Kulingana na Meneja huyo,RUWASA inaendelea kukarabati miradi iliyokuwa imechakaa na kuboresha usimamizi wa miradi ya maji iliyokamilika ili iwe endelevu kwa kuunda na kusajili Jumuiya za watumiaji maji(CBWSOs) ambazo zitakuwa zinasimamia miradi hiyo na kuhakikisha inatoa huduma wakati wote. 

Amesema, katika kipindi cha mwaka 2019/2020 RUWASA Wilaya ya Songea ilipanga kuunda na kusajili jumuiya za watumiaji maji 17 ambapo hadi kufikia Juni 2020 jumuiya 10 zilikuwa zimeundwa na kusajiliwa. 

Hata hivyo amesema, kwa mwaka wa fedha 2020/2021 jumuiya za watumiaji 28 zilipangwa kuundwa na kusajiliwa ambapo hadi kufikia Januari 2021 jumuiya 11 zimeundwa. 

Ameitaja miradi ya maji iliyopangwa kutekelezwa katika Halmashauri ya Madaba kupitia P4R kuwa ni Ndelenyuma,Lutukira na Mbangamawe ,kupitia PBR4 mradi mmoja wa maji katika kijiji cha Igawisenga unatarajia kutekelezwa. 

Kwa mujibu wa Meneja huyo wa RUWASA,katika Halmashauri ya Songea vijijini kupitia P4R miradi ya maji inatarajia kutekelezwa katika vijiji vya Lipaya,Lundusi na Maposeni,kupitia PBR4 mradi mmoja wa maji unatarajia kutekelezwa katika kijiji cha Ndongosi na mradi mmoja unatarajia kutekelezwa Ndilimalitembo Manispaa ya Songea. 

Amesema, RUWASA Wilaya ya Songea imepanga kukamilisha zoezi la usajili Jumjuiya za watumiaji maji ifikapo Juni 30 mwaka huu na kwamba RUWASA imejipanga kuendelea kutoa elimu juu ya utunzaji vyanzo vya maji na elimu kuhusu umuhimu wa ulipaji wa huduma ya maji ili kuifanya miradi iwe endelevu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news