Waziri Biteko asisitiza uwazi biashara ya madini

Aonya upotoshaji kuhusu usimamizi Sekta ya Madini, aagiza ujenzi wa Soko la Madini Mirerani kukamilika ndani ya miezi miwili, aelekeza ukaguzi eneo la Ukuta wa Mirerani ufanyike kwa kuzingatia utu (staha)

 

Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema Serikali imeweka Sheria, Kanuani na Taratibu za Madini ili kuweka mazingira rafiki ya ukusanyaji kodi ambao unatekelezwa kwa umakini na wasimamizi wakuu, Wizara ya Madini,anaripoti Steven Nyamiti (WM), Mirerani.
Kauli ya Biteko imekuja kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wafanyabiashara wa madini (Brokers) na wachimbaji waliopo Mirerani wakilalamikia utaratibu unaotumika sasa wa kutumia Lakiri (Seal) kwa kila madini yanayopatikana kabla ya kwenda sokoni huku wakipendekeza utaratibu huo wa Lakiri kubadilishwa kwa kuwa unachangamoto nyingi.

Waziri Biteko ameyasema hayo leo Januari 13, 2021 Mirerani mkoani Manyara alipofanya ziara hiyo ambapo, awali katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama na watendaji wa Serikali amesisitiza uthaminishaji wa madini yapatikanayo kwa haraka na uwazi ili muuzaji apate kibali maalumu cha kwenda kuuza (Declaration Form) mapema na kwa uharaka zaidi.

"Ukitoka eneo la Ukuta wa Mirerani lazima uwe na nyaraka za serikali zitakazokutambulisha ili kupunguza usumbufu utakaojitokeza.
Serikali inasisitiza sana utaratibu wa uthaminishaji ufanyike kwa haraka na uwazi pasipo kuuliza maswali mengi ili serikali ipate mrabaha,"amesema Biteko.

Kwa upande mwingine, Waziri Biteko ameruhusu wanaapolo kufanya biashara ya madini ndani ya ukuta isipokuwa wafuate taratibu zilizowekwa kabla ya kuuza madini. 

Pia, Biteko ameelekeza wachimbaji wadogo maarufu wana Apolo kuruhusiwa kuuza madini.Ameongeza kuwa wakitoka nje lazima wapatiwe cheti maalumu au nakala iliyothibitishwa kwa ajili ya utambuzi (Certificate) ili kuondoa usumbufu utakaojitokeza na kupelekea Serikali kukusanya kodi.

Aidha, Waziri Biteko ameagiza ujenzi wa Soko la Madini Mkoa wa Manyara uanze na ukamilike ndani ya miezi miwili. 

"Soko hilo litaondoa changamoto ya kwenda mbali mrefu kuuza madini. Ujenzi wa Soko utapunguza usumbufu wanaopata wachimbaji na wafanyabiashara sasa kusafiri umbali mrefu hadi Jijini Arusha ambapo ndipo lilipo soko la madini linalotumiwa hivi sasa,"amesisitiza Biteko.

Akijibu kuhusu malalamiko ya ubovu na uchakavu wa miundombinu ya eneo la Ukuta wa Mirerani, Waziri Biteko amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila kukarabati barabara zilizo ndani ya ukuta sambamba na kutatua Changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara na pia kuongeza vyumba vya ukaguzi ambapo Prof. Msanjila alijibu kwa kueleza kuwa tayari bajeti ilishatengwa na ujenzi wa miundombinu hiyo kuanzia barabara na ununuzi wa jenereta unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti amemshukuru Waziri wa Madini kwa kukubali kujenga Soko la Madini mkoani Manyara. Amehaidi kuendeleza ushirikiano ulipo na Wizara ya Madini ili kuendelea kuilinda rasilimali hiyo hapa nchini.

Waziri Biteko yupo kwenye ziara ya kuwatembelea wachimbaji wa madini, wafanyabiashara Wakubwa na Wadogo kwenye migodi mbalimbali hapa nchini yenye lengo la kusikiliza kero mbalimbali, kuelekeza Utekelezaji wa Sera kwa wachimbaji na wafanyabiashara ili kuweka uwazi uwajibikaji kwenye Sekta ya Madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news