Jumuiya ya Kimataifa yahaidi kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika sekta mbalimbali

Umoja wa Ulaya umeahidi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika jitihada za kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nchi za Umoja wa Ulaya kuja kuwekeza hapa nchini, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akieleza jambo kwa Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Mhe. Manfred Fanti wakati walipokutana na kufanya mazungumzo kuhusu masuala ya uwekezaji Januari 22,2021 jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa Januari 22, 2021 jijini Dodoma na Mhe. Manfred Fanti, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (kulia) akisisitiza jambo kwa Naibu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Bibi Lianne Houben ambapo katika mazungumzo hayo walijadili na kukubaliana maeneo mbalimbali yanayoweza kuboreshwa ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nchini Uholanzi.

“Nimekuwa nikisikia ushuhuda kutoka kwa wawekezaji wengi wanaotoka nchi za Umoja wa Ulaya kuwa wanapata faida katika uwekezaji wao hapa nchini na nikiwa kama mwakilishi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania ni jukumu langu kuhakikisha kuwa nashirikiana ipasavyo na Serikali ya Tanzania kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuwekeza Tanzania,"amesema Mheshimiwa Balozi Fanti.

Ameongeza kuwa, Umoja wa Ulaya unatambua jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuboresha mifumo ya kisheria, kisera na ya kitaasisi ili kuweka mazingira rafiki zaidi yatakayovutia wawekezaji na hivyo wako tayari kuendelea kuiunga mkono Serikali ili kufanikisha lengo hilo.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Kitila Mkumbo na Balozi Fanti walijadili pia maeneo bayana ambayo Tanzania na Umoja wa Ulaya wanaweza kukuza ushirikiano wa uwekezaji ikiwemo katika sekta ya uzalishaji nguo, uchimbaji na uchakataji wa madini, uchakataji wa mazao ya mifugo na uvuvi, uzalishaji wa nishati.

Vilevile Waziri Mkumbo aligusia baadhi ya maeneo ya kimkakati ambayo tayari Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeweka nguvu kuyatekeleza ikiwemo kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Uwekezaji, utekelezaji wa programu ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara (ROADMAP) pamoja na kuandaa mfumo kabambe wa ukusanyaji takwimu za uwekezaji nchini.

Aidha, amemweleza Balozi huyo kuwa hayo ni baadhi ya maeneo ambayo Serikali ipo tayari kuendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya, ili pamoja na mambo mengine, kumaliza kabisa changamoto zinazowakabili wawekezaji wa kigeni hapa nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (kushoto) akipokea kitabu kinachoeleza masuala mbalimbali kuhusu nchi ya Uholanzi kutoka kwa Naibu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Bibi Lianne Houben mara baada ya mazungumzo yao jijini Dodoma kuhusu masuala ya uwekezaji.
Naibu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Bibi Lianne Houben akisisitiza jambo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo leo Januari 22,2021 jijini Dodoma wakati wa mazungumzo yao kuhusu masuala ya uwekezaji.

Kwa upande mwingine Waziri huyo wa Uwekezaji alikutana pia na Bibi Lianne Houben, Naibu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania ambapo katika mazungumzo hayo walijadili na kukubaliana maeneo mbalimbali yanayoweza kuboreshwa ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi, hususani wanaotoka nchi ya Uholanzi.


Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na kuweka mfumo mzuri wa kuziwezesha taasisi mbalimbali wezeshi zinazohudhumia wawekezaji kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi huku zikizingatia maslahi mapana ya wawekezaji, pamoja na suala la uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi na fani mbalimbali ambazo wawekezaji wanazihitaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Mhe. Manfred Fanti mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo kuhusu masuala ya uwekezaji leo Januari 22,2021 Jijini Dodoma. (Picha zote na MAELEZO).

Uholanzi ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kuwa na wawekezaji wengi nchini Tanzania waliowekeza katika sekta za mbalimbali kama vile Kilimo (kwa mfano makampuni ya maua yaliyowekeza Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro), huduma za kifedha (kwa mfano Benki ya NMB), Viwanda (kwa mfano Kampuni Unilever na Heineken), usafirishaji (kwa mfano Kampuni ya KLM).


Takwimu zinaonesha kuwa takribani miradi 161 ya kutoka Uholanzi imesajiliwa katika za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ikiwa na mitaji yenye jumla ya thamani ya Dola za Marekani biilioni 1.1 na kutoa ajira 13,995.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news