Morogoro yajipanga kukuza uzalishaji zao la mahindi

Wito umetolewa kwa maafisa ugani mkoani Morogoro kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula hususani zao la mahindi, anaripoti Victor Makinda (Morogoro).
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare akimkabidhi pikipiki, Afisa Ugani wa Kijiji cha Mwaya wilayani Ulanga, Samweli Ibwela wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki 10 kwa maafisa ugani waliofanya vizuri kwenye mradi wa kukuza kilimo cha zao la mahindi mjini Morogoro. Picha na Victor Makinda/Diramakini).

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki 10 zilizotolewa na Serikali ya China na Serikali ya Mkoa wa Morogoro kwa maafisa ugani 10 kati ya 42 waliofanya vizuri katika utekelezaji wa mradi wa kukuza kilimo cha zao la mahindi mkoani Morogoro, mradi unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha China na Serikali ya Mkoa wa Morogoro huku ukisimamiwa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). 

Akizungumza katika hafla hiyo, Sanare amesema kuwa, Mkoa wa Morogoro una ardhi kubwa na nzuri ifaayo kwa kilimo cha mazao ya aina mbalimbali ikiwemo mahindi, lakini uzalishaji wa zao hilo uko chini kulinganisha na ubora wa ardhi ya mkoa huo.

“Mradi huu wa kukuza kilimo cha zao la mahindi, umeonesha tija na ninatumai kuwa utakuwa na tija kubwa za zaidi katika kukuza uzalishaji wa zao hili muhimu la chakula. Ni wakati sasa maafisa ugani kumuunga mkono kwa vitendo Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kuchapa kazi kwa bidii, kutoka ofisi na kwenda kwa wakulima kuwafundisha njia bora za uzalishaji wa zao hili ili wazalishe kwa wingi,”amesema.

Sanare ameongeza kusema kuwa pikipiki walizopewa maafisa ugani hao ziwe chachu ya kufanya kazi kwa bidii kwa kuwafikia wakulima mashambani mwao na kuwapatia utaalamu wa kuzalisha kwa tija. 

Amewaasa maafisa ugani hao kutotumia pikipiki hizo kwa shughuli binafsi kinyume na malengo yanayo tarajiwa ambayo ni kuwafikiwa wakulima kwa wakati. 

Akitoa taarifa ya mradi mradi huo wa kukuza uzalishaji wa kilimo cha zao la mahindi, Mratibu wa mradi, Ernest Mkongo, alisema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2013 katika vijiji viwili na baadae kufikia vijiji 10 huku ukiwa umeonesha mafanikio makubwa.

“Mradi huu unatarajiwa kufikia ukomo mwaka huu wa 2021, ambapo zaidi ya wakulima 2000 wamefikiwa moja kwa moja. Ni matarajio yetu kuwa idadi hiyo ya wakulima itaongezeka kwa haraka kwani tunao wataalamu wa kutosha wenye nyezo za kuweza kulifikia kundi kubwa zaidi la wakulima mkoani hapa,"amesema Mkongo.

Naye Afisa Ugani wa Kijiji cha Mtego wa Simba,Halmashauli ya Morogoro moja ya kijiji kinachotekeleza mradi huo, Veronica Lugano amesema kuwa, kabla ya mradi huo wakulima walikuwa katika kijiji chake wakizalisha kati ya gunia 2 mpaka 3 kwa hekari moja, kwa sasa wakulima hao wanazalisha kati ya gunia 10 mpaka 20 kwa hekali moja. 

Lugano amesema kuwa, ana matumaini makubwa kuwa tenkolojia hiyo ya kukuza uzalishaji wa zao la mahindi ikiwa itatumiwa vizuri na wakulima itaufanya mkoa wa Morogoro kuzalishaji zao la mahindi kwa wingi.

 Amesema kuwa, maafisa ugani wamejipanga kusimamia kikamilifu uzalishaji wa zao hilo mkoani Morogoro kwa kuhamasisha na kuwafundisha wakulima kulima kilimo cha kisasa kwa kutumia kanuni bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa ajili ya kukuza uchumi wa mkoa wa Morogoro na Taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news