Tanzania, Ethiopia zakubaliana kukuza ushirikiano wa kibiashara, uwekezaji

Serikali ya Tanzania na Ethiopia zimekubaliana kukuza zaidi ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji ambao kwa sasa bado upo kiwango cha chini licha ya kuwepo ongezeko la biashara kutoka sh.Bilioni 3.07 mwaka 2016 hadi kufikia sh. Bilioni 13.55 mwaka 2019/2020, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na Rais wa Jamhuri ya Ethiopia, Mhe. Sahle-Work Zewde wakati akimsindikiza mgeni wake huyo baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya siku moja nchini katika Uwanja wa Ndege wa Geita mjini Chato leo Januari 25, 2012. (Picha na Ikulu).

Sambamba na kuwepo uwekezaji wa miradi 13 ya Ethiopia yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 14.57 iliyozalisha ajira 567 hapa nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli ameyasema hayo leo Januari 25, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari akiwa na mgeni wake Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde mara baada ya kumaliza mazungumzo yao nyumbani kwake mjini Chato,Geita.

Dkt.Magufuli ametaja maeneo mengine waliozungumzia viongozi hao kuwa ni kuimarisha ushirikiano katika usafiri wa anga na utalii, ulinzi, kupeleka walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Ethiopia, kushirikiana mbinu za kunufaika na mazao ya mifugo hasa ikizingatiwa Ethiopia na Tanzania zinashika nafasi ya kwanza na ya pili (mtawalia) kwa idadi kubwa ya mifugo Barani Afrika.

Amesema wameitaka Kamati ya Pamoja ya Majadiliano (JPC) baina ya nchi hizo kuhakikisha zinakutana haraka ili kupitia maeneo yote ya ushirikiano na kuongeza maeneo mapya.

Rais Magufuli amesema, Tanzania ipo tayari kuwaachia wafungwa na maabusu 1,787 wa Ethiopia wanaoshikiliwa katika mahabusu mbalimbali hapa nchini baada ya kukamatwa na kukutwa na hatia ya kuingia nchini kinyume cha sheria.

Pia ameiruhusu Ethiopia kutuma ndege wakati wowote ili kuwarejesha nyumbani kwao hata kama ikiwemo aliyehukumiwa leo.

Kuhusu viwanja vya Tanzania vilivyopo Addis Ababa ambavyo Serikali ya Ethiopia ilivinyang’anya kutokana na Tanzania kutoviendeleza kwa mujibu wa sheria za Ethiopia, Rais Magufuli amesema, Serikali ya Tanzania imechukua hatua dhidi ya waliohusika katika upotevu wa fedha za uendelezaji wa viwanja hivyo na ameiomba Serikali ya Ethiopia kuvirejesha kwa Tanzania ili viendelezwe.

Rais Magufuli amemshukuru Rais Sahle-Work Zewde kwa kufanya ziara hapa nchini na kwamba hii inaimarisha na kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na Ethiopia ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mtawala wa Ethiopia Hayati Haile Selassie I tangu mwaka 1963.

Naye Rais Sahle-Work Zewde amemshukuru Rais Magufuli kwa kumkaribisha hapa nchini na ameshukuru kwa kuendeleza uhusiano mzuri wa Tanzania na Ethiopia uliodumu tangu enzi za kupigania ukombozi wa Afrika.

Amempongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kwa kipindi cha pili kuiongoza Tanzania na amebainisha kuwa Ethiopia ipo tayari kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania hususani kukuza biashara na uwekezaji.

Rais Sahle-Work Zewde amesema, Tanzania ni nchi muhimu Barani Afrika kutokana na kuhusika kwake katika masuala ya kijumuia ikiwemo kutafuta amani na ndio maana Ethiopia ipo tayari wakati wote kushirikiana na Tanzania.

Amepokea ombi la kurejeshwa kwa viwanja vya Tanzania vilivyonyang’anywa na Serikali ya Ethiopia kutokana na kutoendelezwa.

Pia ameshukuru kwa utayari wa Tanzania kupeleka walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Ethiopia, ameafiki ushirikiano wa Tanzania na Ethiopia katika kunufaika na utajiri wa mifugo mingi iliyopo na ameishukuru Tanzania kwa utayari wake wa kuwaachia Wafungwa na Maabusu wa Ethiopia 1,789 waliopo magerezani hapa nchini baada ya kukamatwa na kukutwa na hatia ya kuingia nchini kinyume cha sheria.Sahle-Work Zewde amemaliza ziara yake na amerejea Addis Ababa nchini Ethiopia leo.

Rais Sahle-Work Zewde ni nani?

Sahle-Work Zewde ni Mwanadiplomasia nguli na Rais wa Ethiopia.Mama huyu alizaliwa jijini Addis Ababa mnamo Februari 21, 1950 na kupata elimu ya msingi na sekondari katika shule ya Lycee Gibre-Maryam na kisha akajiunga na Chuo Kikuu cha Montepillier nchini Ufaransa ambapo alisomea Sayansi Asilia (Natural Science).

Mhe. Zewde ana weledi wa lugha ya Kifaransa, KiAmhara (Amharic) na Kingereza.

KAZI ZA KIDIPLOMASIA 

1989-1993:

Balozi wa Ethiopia nchini Senegal ambapo pia alikuwa akiliwakilisha nchi yake kwenye mataifa ya Mali, Guinea-Bissau, Cape Verde, Gambia na Guinea. 

1993-2002:

Balozi wa Ethiopia nchini Djibouti huku akiiwakilisha Ethiopia katika Mamlaka ya Maendeleo (IGAD). Baadae aliteuliwa kuwa Balozi wa Ethiopia nchini Ufaransa.

2002-2006:

Mhe. Zewde alikuwa Mwakilishi kwenye UNESCO ambapo alifanya kazi huko Tunisia na Morocco.

Mwanadiplomasia huyu pia alikuwa Mwakilishi wa Ethiopia kwenye Umoja wa Afrika na chombo cha UN kinachoshughulikia Uchumi wa Afrika (ECA). Pamoja na vyeo hivyo, Mhe. Zewde alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mambo ya Afrika kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia.

AFANYA KAZI NA UMOJA WA MATAIFA

Mpaka 2011, Mhe. Zewde alikua ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN Mh. Ban Ki Moon pia alikua Mkuu wa Ofisi ya UN inayoshughulikia amani huko Afrika ya Kati (BINUCA).

Mwaka 2011, Ban alimteua Mhe. Zewde kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya UN Jijini Nairobi (UNON). Katika kipindi cha uongozi wake, Nairobi ikawa sehemu muhimu ya UN katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.

Mnamo Julai 2018, Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akamteua Mhe. Zewde kuwa Mwakilishi Maalum wa UN kwenye Umoja wa Afrika na Mkuu wa Ofisi ya UN kwenye Umoja wa Afrika (UNOAU) katika ngazi ya Under-Secretary General of the United Nation.Ni mwanamke wa  kwanza kushika nafasi hiyo nyeti Ethiopia.

RAIS WA ETHIOPIA

Mnamo Oktoba 25, 2018 Mhe. Zewde alichaguliwa na Bunge la Ethiopia kuwa Rais baada ya mtangulizi wake Mhe. Mukatu Teshome kujiuzulu kwa sababu zisizojulikana.Mhe. Zewde anatarajiwa kuliongoza Taifa hilo kwa mihula miwili kila muhula ukiwa na miaka sita.Mhe. Zewde ni Mwanamke  wa kwanza kuwa Rais katika Taifa hilo la  Ethiopia

Post a Comment

0 Comments