Diwani wa Kata ya Mtambani iliyopo katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlandizi Halmashauri ya Kibaha Vijijini, Godfrey Mwafulilwa (CCM) amemmwagia sifa aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa kwa kusema alikuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mwafulilwa amemwaga sifa hizo kupitia vyombo vya habari mbalimbali pamoja na mitandao ya kijamii kwa kusema amemkumbuka Jumaa kutokana na kukaa jimboni miaka 10 akiwa kiongozi mwenye upendo mkubwa na jamii.
Amesema kuwa, ameamua kumkumbuka Hamoud Jumaa kwa kuwa alikuwa na sifa kubwa sita ikiwemo subira,uvumilivu, Mbunge mwenye akiba ya maneno,ukarimu,hekima na mwenye kumcha Mungu.
Mbali na sifa hizo, lakini pia Mwafulilwa amesema kuwa, sifa nyingine ni pamoja na uchapakazi wake,kujitoa katika jamii katika misaada mbalimbali na hata uchungu wa kusaidia wananchi wa jimbo lake.
Aidha, Mwafulilwa amesema kuhusu subira, Jumaa alikuwa kiongozi aliyejaliwa subira katika uongozi wake kwani hakuwa na papara katika kufanya maamuzi hata katika jambo lenye kuonyesha mafanikio ya haraka.
Diwani huyo ameongeza kuwa, Jumaa alikuwa na uvumilivu na kwamba hajawahi kuona kiongozi mvumilivu kama huyo kwa Kibaha Vijijini na wakati mwingine unaweza kusema huenda ana moyo wa kupokea maumivu.
Amesema,Jumaa alikuwa na tabia ya uvumilivu hata kama kuna jambo linamuumiza lakini hakuna anayeweza kujua na badala yake kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa zaidi.
"Asilimia 90 ya watu waliokuwa karibu na Jumaa waliwahi kumchukiza na kumuumiza, lakini hakuna aliyejibiwa vibaya kwa kuwa alikuwa anajua nguvu ya kujibu maumivu,"amesema Mwafulilwa.
Mwafulilwa amesema kuwa, kama kiongozi anaweza kuwa na akiba ya maneno ni wazi kuwa unaonyesha ujasiri kwa watu unaowatumikia na kusema jambo hilo limewafundisha watu wengi na hata madiwani.
"Namkumbuka Jumaa wakati palipozuka sakata la kumkataa Mkurugenzi Tatu Selemani, mbunge alitusihi tusimalize maneno na tuache ya akiba jambo ambalo lilichukuliwa katika mtazamo tofauti, lakini leo madiwani tunajionea na kujua nini cha kufanya,"smesema Mwafulilwa.
Kuhusu ukarimu na hekima Mwafulilwa amesema kuwa,katika kipindi chake cha uongozi Jumaa alikuwa mstari wa mbele kuonyesha ukarimu pale kiongozi wa mkoa au Kitaifa wanapokuja jimboni.
Amesema kuwa,Jumaa alikuwa anawapokea wageni wakati huo madiwani hamjui mgeni analala wapi,anakula nini na mambo mengine lakini ikagundulika kuwa yeye alikuwa anafanya bila kumtangazia mtu.
"Jumaa alikuwa na hekima ya uongozi,alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwashauri watu na mara nyingi hata mimi mwenyewe aliniambia, ukiwa kiongozi hakikisha majibu yako kwa watu wako yawe yenye kuleta furaha na ukishindwa basi yalete matumaini sio machungu na machukizo,"amesema Mwafulilwa.
Mwafulilwa amesema kuwa, kiongozi ukiwa na sifa nzuri, lazima utaacha kumbukumbu nzuri kwa watu wako na kwamba hiyo inasaidia watu wengine kuiga mfano kutoka kwako kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo
Hata hivyo, Mwafulilwa ameweka wazi kuwa hawataweza kumaliza sifa za mbunge huyo mstaafu, lakini ilijionyesha katika chaguzi za CCM walivyomchagua kwa kishindo jambo ambalo halikuwahi kutokea jimboni humo.
