EWURA yapiga hatua udhibiti uchakachuaji wa mafuta nchini

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendesha mafunzo kwa waandishi wa habari Kanda ya Ziwa kwa lengo la kuwafahamisha kuhusu kazi,wajibu na mafanikio ya EWURA katika udhibiti wa huduma za nishati na maji, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Godfrey Chibulunje akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari Kanda ya Ziwa leo Jumatatu, Februari 1,2021. Kushoto ni Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano EWURA, Titus Kaguo. 

Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika leo Jumatatu Februari 1,2021 na kukutanisha waandishi wa habari kutoka Mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Mara, Geita na Simiyu katika ukumbi wa Gold Crest jijini Mwanza ambapo wamepata fursa ya kufahamishwa kuhusu kuanzishwa kwa EWURA, sekta inazozitawala, muundo wake, mafanikio na changamoto zake.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Godfrey Chibulunje amesema waandishi wa habari ni wadau wakubwa wa EWURA katika utendaji wao wa kazi na kwamba wanafanya kazi kwa uwazi na mara nyingi wamekuwa tayari kutoa ufafanuzi kwa jambo lolote lile ambalo waandishi wa habari wanahitaji ili kuihabarisha na kuielimisha jamii.  

Chibulunje amesema EWURA itaendelea kutoa ushauri kwa serikali katika kuandaa sera,sheria na kanuni zitakazowezesha kukua kwa sekta za nishati na maji na kuendelea kusimamia watoaa huduma ili kuhakikisha huduma zinakuwa bora kwa manufaa ya taifa.

Aidha, amesema EWURA imesaidia kuzuia mfumko wa bei, kuimarisha mamlaka za maji nchini na kukuza umeme binafsi na kwamba itaendelea kuzingatia misingi mikuu sita ya utawala bora katika maamuzi ya udhibiti ambayo ni weledi, uwajibikaji, utabirikaji, ushirikishaji, uwazi na kufuata sheria.

Ameeleza kuwa,EWURA imefanikiwa kupambana na kupunguza tatizo la uchakachuaji wa mafuta kutoka asilimia 80 mwaka 2007 hadi asilimia 4 mwaka 2020.

Mhandisi Chibulunje amesema suala la uchakachuaji wa mafuta hapa nchini imekuwa changamoto, lakini wao kama EWURA wamefanikiwa kupambana na kupunguza changamoto hiyo kwa asilimia kubwa.

Amesema, EWURA inadhibiti ubora wa miundombinu ya mafuta ili kulinda afya,usalama na mazingira ambapo kutokana na udhibiti huo maghala na vituo vya mafuta vimeendelea kuwa bora zaidi na imeandaa masharti nafuu ili kuvutia wawekezaji kwenye maeneo ya vijijini pamoja na kutoa muongozo wa ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini vya gharama nafuu.
Pia amesema,EWURA inatoa leseni ili kuhakikisha huduma za mafuta zinatolewa kwa kufuata sheria, kanuni na viwango stahiki hadi kufikia Juni 2020 imetoa leseni 1,515 katika sekta ya mafuta, kati ya hizo leseni 58 ni za kuuza mafuta kwa jumla.

Amesema, leseni 1,360 za vituo vya mafuta vya rejareja,leseni tano za kuhifadhi mafuta,leseni 50 za biashara ya vilainishi,leseni 18 za kuagiza na kuuza gesi ya kupikia (LPG),leseni mbili za kutoa huduma ya mafuta kwenye meli,leseni 15 za kuweka miundombinu binafsi ya kuhifadhia na kujaza mafuta,leseni 4 za kusafisha mafuta,leseni 1 ya kuchakata mafuta machafu,leseni 1 ya kusafirisha mafuta na leseni 1 ya wakala wa uagizaji mafuta kwa pamoja.

Pia Mhandisi Chibulunje amesema,mamlaka hiyo imeandaa mfumo wa kuuza mafuta vijijini kwa kutumia vituo vinavyotembea (mobile petrol stations) ili kuongeza upatikanaji wa mafuta kwa njia ambazo ni salama na inayozingatia utunzaji wa mazingira. Amesema, mfumo huo utaondoa utunzaji na uuzaji wa mafuta kwenye mapipa,madumu na chupa za plastiki.

Amesema EWURA itaendelea kutoa ushauri kwa Serikali katika kuandaa sera,sheria na kanuni zitakazowezesha kukua kwa sekta za nishati na maji na kuendelea kusimamia watoa huduma ili kuhakikisha huduma zinakuwa bora kwa manufaa ya taifa.

"EWURA mesaidia kuzuia mfumko wa bei, kuimarisha mamlaka za maji nchini na kukuza umeme binafsi na itaendelea kuzingatia misingi mikuu sita ya utawala bora katika maamuzi ya udhibiti ambayo ni weledi, uwajibikaji, utabirikaji, ushirikishaji, uwazi na kufuata sheria,"amesema Mhandisi Chibulunje.
Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, George Mhina akizungumza wakati wa mafunzo hayo. 

Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, George Mhina amewaomba waandishi wa habari kuendeleza ushirikiano walionao kwa EWURA nao wataendelea kutoa ushirikiano. 

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Mwanza, Edwin Soko akizungumza kwenye mafunzo hayo. (Mpigapicha Wetu).

Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Mwanza, Edwin Soko ameishukuru EWURA kwa kuandaa mafunzo hayo na kuahidi kuwa waandishi wa habari Kanda ya Ziwa wataendelea kushirikiana na EWURA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here