NAIBU WAZIRI MAJI ARIDHISHWA NA UJENZI WA MIRADI JIJINI MWANZA

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi ameridhishwa na ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa na kwenye Wilaya za Nyamagana na Ilemela Mkoani Mwanza, anaripoti Mohamed Saif (Mwanza).
Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi akishiriki shughuli ya ujenzi wa tenki la maji la Buswelu wilayani Ilemela.

Amesema hayo kwa nyakati tofauti Februari 24, 2021 wakati wa ziara yake kwenye miradi ya ujenzi wa tenki la maji la Sahwa Wilayani Nyamagana na ujenzi wa tenki la Buswelu Wilayani Ilemela.

“Lengo la ziara yangu ni kufika hasa maeneo yenye changamoto ili tupate majawabu ambayo ni kuona wananchi wanapata maji bombani,”amesema Naibu Waziri Mahundi.

Aidha, Mhandisi Mahundi amepongeza ushirikiano baina ya taasisi za maji mkoani humo na Serikali za wilaya hizo na amezitaka taasisi nyingine kwenye sekta hiyo kuiga ushirikiano huo.

Ametoa pongezi hizo baada ya kukutana na Wakuu wa Wilaya hizo na kuelezwa namna ambavyo wanashirikiana katika suala zima la ujenzi wa miradi ya maji kwenye wilaya hizo.

“Ninahitaji kuona taasisi za maji zikishirikiana, mnapaswa kutambua kwamba mnatekeleza majukumu yenu kwa niaba ya Wizara ya Maji lakini pia ni muhimu sana kuhakikisha mnashirikiana na viongozi wa Serikali katika ngazi zote,”amesisitiza Naibu Waziri Mahundi.

Mara baada ya kutembelea miradi hiyo ya ujenzi wa matenki, Naibu Waziri Mahundi alisema ameridhishwa na hatua zinazochukuliwa na MWAUWASA kuhakikisha inatatua changamoto ya upatikanaji wa maji Jijini Mwanza.

“Ninampongeza Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele kazi anayofanya inaonekana na inaridhisha na hiki ndicho tunachotaka kuona kwenye maeneo mengine pia,”amesisitiza Naibu waziri Mahundi.

Awali, katika taarifa ya hali ya maji Wilayani Nyamagana, Naibu Waziri Mahundi alielezwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Dkt. Phillis Nyimbi namna ambavyo serikali ya wilaya yake inavyoshirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) katika kuhakikisha inaboresha upatikanaji wa huduma ya maji.

Dkt. Nyimbi alimueleza Naibu Waziri Mahundi kuhusiana na changamoto ya upatikanaji wa maji kwenye baadhi ya maeneo yakiwemo ya Buhongwa, Igoma, Kishiri na Lwanima ambayo hata hivyo alisema kuwa MWAUWASA imeonyesha jitihada kubwa za kuhakikisha changamoto inamalizika.

“Kuna baadhi ya kata bado zina changamoto ya maji mfano Kata ya Buhongwa hii wananchi wanaongezeka na hivyo miundombinu haitoshelezi pia Igoma na Kishiri na pia Lwanima maji hayatoshelezi licha ya kwamba MWAUWASA imejitahidi kutoa maji kwa awamu yaani mgao na tunatamani hii ifike kikomo,”amesema Dkt. Nyimbi.

Amesema, anatambua ujenzi wa miradi ya maji unaoendelea na alimhakikishia Naibu Waziri Mahundi ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika mapema iwezekanavyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt.Severine Lalika amesema, mradi wa tenki la Buswelu ni miongoni mwa miradi ambayo ilitengewa fedha Mwaka wa fedha 2019/2020 ikiwa ni utekelezaji wa sera ya Serikali ya kuhakikisha wananchi hawatembei umbali mrefu kufuata huduma ya maji.

Amesema, anatambua miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na MWAUWASA kwenye wilaya hiyo na aliipongeza kwa jitihada zake katika kusimamia ujenzi wa miradi ya maji kwa niaba ya Serikali ambapo alisema kupitia miradi hiyo kero ya maji inakwenda kuwa historia.

“Natambua MWAUWASA inatekeleza miradi mingine ya maji Wilayani Ilemela mbali na huu tuliotembelea leo ambayo ni pamoja na Mjimwema, Nyasaka, Nyamhongolo, Kabusungu, Kabangaja, Igalagala na Kayenze, ninaamini kero ya maji itabaki historia,”amesema Dkt. Lalika.

Kwa upande wake, Mhandisi Msenyele amesema, ujenzi wa miradi hiyo ya matenki (Buswelu na Sahwa) unagharamiwa na Serikali kwa asilimia Miamoja kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa wahisani ambao ni Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa.

Mhandisi Msenyele alisema ujenzi wake unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na alimhakikishia Naibu Waziri Mahundi kwamba yote kwa pamoja itakamilika kwa wakati kama ilivyo kwenye mikataba yake.

Ziara ya Mhandisi Mahundi kwenye Wilaya za Nyamagana na Ilemela Mkoani Mwanza ni ya kwanza tangu ateuliwe na kuapishwa rasmi kuwa Naibu Waziri wa Maji baada ya ziara yake Wilayani Kwimba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news