Serikali yataka Watanzania kumpuuza Profesa Assad

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Watanzania kumpuuza Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali Mstaafu, Prof. Mussa Assad kwa kutoa tuhuma kuwa, Maafisa na Viongozi katika Taasisi za Umma wana uwezo mdogo kiutendaji, anaripoti James K.Mwanamyoto (OR-UTUMISHI).

Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo kwa Watanzania kupitia vyombo vya habari, baada ya Prof. Assad hivi karibuni kuzungumza kwenye mdahalo uliofanyika Chuo Kikuu cha Kiislam mkoani Morogogoro, kuwa asilimia 60 ya Watumishi na Viongozi wa Umma nchini hawana uwezo wa kutekeleza majukumu yao wakati asilimia 40 wana uwezo kidogo.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari jijini Dodoma kuhusu tuhuma za Prof. Mussa Assad dhidi ya Sekta ya Umma. Kulia ni Mkurugenzi Idara ya uendelezaji Sera Ofisi ya Rais - UTUMISHI, Bi. Agnes Meena.

Akifafanua kuhusu uwezo wa kiutendaji walionao Watumishi na Viongozi wa umma, Dkt. Ndumbaro amesema tuhuma alizozitoa Prof. Assad zilijikita katika hisia na maoni yake binafsi kuliko uwezo wa kiakili na kitaaluma alionao na wala hakufanya tafiti, kwani watumishi na viongozi wanatekeleza majukumu yao vizuri na ndio maana nchi imepata maendeleo makubwa katika sekta za elimu, miundombinu pamoja na afya na hatimaye taifa limeingia katika uchumi wa kati.

Dkt. Ndumbaro amefafanua kuwa, Watumishi Watendaji na Viongozi wa Umma hupanda au kuteuliwa kuwa Viongozi katika Utumishi wa Umma kwa mujibu wa Miongozo ya Utumishi wa Umma ambayo pamoja na mambo mengine huzingatia sifa mbalimbali za weledi na vigezo vya majukumu wanayopaswa kuyatekeleza.

Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) wakati akitoa ufafanuzi jijini Dodoma kuhusu tuhuma alizozitoa Prof. Mussa Assad dhidi ya Sekta ya Umma nchini.

Ametoa mfano wa namna Serikali inavyohakikisha inakuwa na rasilimaliwatu yenye sifa stahiki kwa kuzingatia ipasavyo Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma Kifungu Na. 4.3 (ii) ambayo imebainisha kuwa, Vigezo vya Uteuzi katika Utumishi wa Umma vizingatie Uwiano kati ya Taaluma na Ujuzi wa kazi pamoja na sifa nyingine kama Uzoefu Kazini, rekodi kazini na uwezo wa kujifunza.

Dkt. Ndumbaro ameuthibitishia umma kuwa, Watumishi wana uwezo kiutendaji kwani pindi Watumishi wa Umma wanapoteuliwa kwa mara ya kwanza kushika nafasi za uongozi katika taasisi za Serikali, hupatiwa mafunzo elekezi ya utawala na uongozi ndani ya kipindi cha miezi mitatu hivyo kuondoa uwezekano wa kuwa na viongozi wasiokuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Ameongoza kuwa, viongozi wengine wa Umma, hupewa mafunzo ya stadi na weledi (profiency and meritocracy) ambayo yamewawezesha kuboresha utendaji kazi wao ndani ya Utumishi wa Umma, pia mafunzo katika ngazi mbalimbali za elimu yaani Stashahada, Shahada, Shahada ya Uzamili na uzamivu hutolewa ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo wa kiutendaji.

Dkt. Ndumbaro amesisitiza kuwa, kutokana na mafunzo hayo waliyopatiwa na wanayoendelea kupatiwa Watumishi na Viongozi wa Umma, yamewawezesha kuimarika katika kutekeleza majukumu yao na baadhi yao wameaminiwa na kuteuliwa kutekeleza majukumu mbalimbali katika Taasisi za Kikanda na Kimataifa, hivyo wamedhihirisha kwa vitendo kuwa hoja ya Prof. Assad ya kuwatuhumu kutokuwa na uwezo kiutendaji ni ya kizushi na haina mantiki wala mashiko yoyote. 

Aidha, Dkt. Ndumbaro amemkumbusha Prof. Assad kuendelea kuheshimu Katiba, Sheria, Maadili ya Uongozi na kiapo cha kazi aliyowahi kuifanya licha ya kuwa ni kiongozi mstaafu, kwani kinyume chake atakuwa ameipuuza katiba kwa kuvunja sheria.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kama msimamizi wa masuala ya Kiutumishi na Utawala Bora nchini imelazimika kutolea ufafanuzi tuhuma za Prof. Assad kwani hazina ukweli wowote hivyo wananchi waendelee kuwa na imani na Utumishi wa Umma uliopo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news