Waziri Ummy Mwalimu agawa futari kwa kaya 200 jimboni kwake

WAZIRI wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amegawa futari kwa wananchi wa kaya 200 wa jimbo lake la Tanga,anaripoti Mashaka Mhando (Tanga).

Waziri Ummy  ambaye ni mbunge wa jimbo hilo,  amegawa futari hiyo kwa wananchi wanaoishi katika kata za Mabokweni na Mzizima kwa msaada mkubwa kutoka Taasisi ya Doreen Mollel Foundation, wakishirikiana na Taasisi ya Kuratibu Maendeleo ya Uturuki (TIKA). 


Mkurugenzi wa taasisi ya Doreen Mollel Foundation, Doreen Mollel alisema taasisi hiyo imetekeleza maombi ya Waziri Ummy aliyeomba msaada wa futari kwa ajili ya wananchi wake wasiojiweza. 

Alisema licha ya kutoa msaada wa futari kwa wananchi wa jimbo hilo la Waziri, kwa mwaka huu wamepanga kutoa pia msaada wa futari katika miji ya Zanzibar, Kilwa,  Mafyia na Dar es salaam ambako kwa mwaka huu wamelenga kuzifikia kaya 3,000.

Doreen alisema taasisi yake imeonelea igawe futari kama sehemu moja wapo ya kuungana na Waislamu nchini katika kutekeleza funga ya Ramadhani. 

"Ndugu zangu wana Tanga, leo tunawakabidhi futari hii tuliombwa na mbunge wenu mheshimiwa Ummy (Mwalimu- Waziri wa Tamisemi), na humo ndani ya boksi kuna mchele, maharage, sukari, unga wa ngano, mafuta, sabuni na chumvi, " alisema Doreen. 

Naye msimamizi wa taasisi ya TIKA nchini Tanzania Badru Hassain alisema huu ni msimu wa tatu wanajumuika na Waislamu nchini Tanzania kugawa futari kuwaunga mkono wadau wao mbalimbali nchini. 

Akitoa shukrani zake kwa msaada huo wa futari Waziri Ummy alishukuru taasisi ya Doreen Mollel Foundation, kwa kumsaidia kugawa futari hiyo kwa kaya hizo katika jimbo lake ambazo zinakabilia na ugumu wa upataji futari. 

"Nawashukuru Doreen Foundation, kwa asilimia 100 kwa kunipatia msaada huu wa futari na washirika wako wa TIKA" alisema Ummy. 

Waziri alisema kuwa huu ni mwezi wa toba kwa waislamu na kwamba zipo zipo kaya hazina uwezo wa kupata mahitaji ya futari hivyo msaada aliopatiwa utasaidia kupunguza makali ya utafutaji wa futari kila siku.

Alisema mahitaji ya futari ni makubwa kwa wapiga kura wake hivyo akaomba taasisi nyingine nchini zisaidie mahitaji hayo kwa watu wengine. 

Pia  Waziri Ummy alimpongeza Mkurugenzi wa Doreen Foundation, akieleza ni msichana wa mfano nchini kwani ubunifu wake wa kusaidia shida mbalimbali ikiwemo kusaidia watoto njiti ni wa mfano kwa mabinti wengine. 

"Doreen hiki unachokifanya kwa kweli ni kitu muhimu na wewe ni mfano wa mabinti wengine waliogombea Miss Tanzania ukiwemo wewe na Jokate Mwegelo mnaonekana mnaweza na ni wa mfano, " alisema Waziri Ummy.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news