Bandari ya Mafuta eneo la Mwangapwani jijini Zanzibar wakaribia

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar iko tayari kutekeleza mpango wa Ujenzi wa Bandari ya Mafuta katika eneo la Mangapwani.Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar baada ya kupokea Mpango wa ujenzi wa Bandari ya Mafuta (Master Plan) katika eneo la Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja, uliotayarishwa na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA).
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman Bw. Mohamed Al Tooqi akiwasilisha Mpango wa Ujenzi wa Bandari ya Mwangapwani Zanzibar (Master Plan) hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar

Amesema Serikali hivi sasa iko tayari kuanza majadiliano ya kina na wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika eneo hilo, baada ya kupokea mpango huo unaobainisha maeneo tofauti ambapo bandari tofauti zitajengwa.Alisema wakati mchakato wa utayarishaji wa mpango huo ukiendelea
kuna wawekezaji kadhaa waliojitokeza na kuonyesha nia ya kuwekeza katika miradi tofauti, hivyo akatowa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kujitokeza na kuwekeza.

“Wafanyabiashara wa Zanzibar wana nafasi kubwa ya kuwekeza, ni vyema wakatumia fursa hiyo”, alisema.Aidha, alitoa shukuran kwa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman kwa kushirkiana kikamilifu na watendaji wa Serikali na hatimae kufanikisha kazi hiyo muhimu kwa wakati muafaka na kwa ufanisi mkubwa.Aidha, Dk. Mwinyi alisema Zanzibar kama ilivyo kwa nchi za Visiwa, inategemea zaidi uwepo wa Bandari kubwa na za kisasa katika kuimarisha uchumi wake.

Amesema Zanzibar hivi sasa inapita katika changamoto kubwa ya kuwa na Bandari isiyokidhi mahitaji ya wakati, hivyo akabainisha hatua ya Serikali ya kujenga Bandari ya Mafuta katika eneo la Mangapwani kuwa ni muhimu kwa vile inakusudia kuondoa changamoto zilizopo.Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa atahakikisha mchakato wa Ujenzi wa Bandari ya Mafuta ya Mangapwani unafanyika kwa haraka na kwa umakini mkubwa, hivyo akawataka watendaji serikalini kuhakikisha kunakuwepo mikataba mizuri katika uwekezaji huo.

Alimshukuru Mtendaji mkuu (CO) wa OIA kwa kuonyesha nia ya kuisaidia Zanzibar ili hatimae iweze kupata wawekezaji wazuri katika maeneo yote.Aidha, aliishkuru OIA kwa kuja na ‘master plan’ inayolenga kuiendeleza Bandari ya Malindi Mjini Unguja ili iweze kutumika kama Bandari ya Utalii, na kubainisha hatua hiyo itafungua mlango wa majadiliano na Serikali kwa kulishirikisha Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni Duniani (UNESCO) ikizingatiwa kuwa eneo hilo ni la Urithi wa Ulimwengu .

Mapema, akiwasilisha ‘master plan’ ya ujenzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA) Sheikh Mohamed Al Tooqi, alisema mpango huo mkubwa unahusisha maeneo makuu matatu, ikiwemo ujenzi wa Bandari mbali mbali, mji wa kisasa wa makaazi pamoja na Mpango wa kuiendeleza Bandari ya Malindi ili iweze kutumika kama Bandari ya utalii. Alisema mambo mbali mbali yamezingatiwa, kama vile matumizi bora ya ardhi yatakayoweza kuvutia wawekezaji pamoja na athari za kimazingira.

Aliitaja baadhi ya miradi itakayowekezwa katika maeneo tofauti ya eneo hilo la Bandari ya Mangapwani, kuwa ni pamoja na Bandari ya Uvuvi, Chelezo,majengo ya Utawala, eneo la viwanda, Bandari ya matumizi mbali mbali, eneo la mji wa mkaazi pamoja na eneo la maghala.Aidha, Sheikh Tooqi alitumia fursa hiyo kumkabidhi zawadi mbali mbali Rais Dk. Mwinyi.

Viongozi mbali mbali wa Kitaifa walishiriki katika hafla hiyo ya kupokea Mpango wa Ujenzi wa Bandari ya Mafuta Mangapwani, akiwemo Balozi Mdogo wa Oman Sheikh Mohamed Ibrahim Al-Bulushi, Mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na watendaji kutoka taasisi na Idara mbali mbali za Serikali.

Post a Comment

0 Comments