DC NYANG'HWALE: WANAFUNZI WATORO, WAZAZI WAFIKISHWE MAHAKAMANI

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Wilson Shimo ameziagiza mamlaka zinazosimamia elimu wilayani humo,kuwafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria wanafunzi watoro pamoja na wazazi wao ikiwa ni kupambana tatizo la utoro katika Wilaya hiyo, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale Wilson Shimo akimkabidhi zawadi ya fedha 250,000 mzazi ambaye mtoto wake alipata daraja la kwanza kidato cha nne mwaka 2020. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).

Amesema kuwa, katika mwezi mmoja katika shule moja na katika darasa moja amepata taaifa za kuwepo wanafunzi watoro zaidi ya 50 jambo ambalo amesema halikubaliki katika juhudi za kuinua elimu katika Wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya ametoa agizo hilo katika hafla iliyofanyika katika shule ya sekondari Msalala iliyoandaliwa kwa ajili ya kutambua na kutoa zawadi kwa wanafunzi waliofaulu vizuri zaidi katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2020.

Pamoja na wanafunzi waliopata madaraja ya kwanza na pili, pia walimu ambao masomo yao yalipata madaraja ya A,B na C walipewa zawadi pamoja na wazazi wa wanafunzi ambao walipata daraja la kwanza(division one).

Halmashauri ya wilaya ya Nyang'hwale ilianzisha mpango mahsusi wa kuboresha ufaulu wa wanafunzi unaojulikana Performance Improvement Project (PIP) kwa matokeo ya kidato ,ambao unafadhiliwa na kampuni ya uchimbaji wa dhahabu ya Barrick kupitia fedha za kusaidia jamii (CSR).

Mpango huo unajumuisha ununuzi wa vitabu vya kiada, chakula Cha wanafunzi kuishi kambini kwa ajili ya masomo ya ziada pamoja na zwwadi Kama motisha kwa makundi ya wanafunzi wanaofaulu vizuri ,wazazi wao, walimu pamoja na shule Bora.

Tangu kuanzishwa kwa mradi huo kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kidato cha nne kimeongezeka kutoka asilimia 77.1 kwa mwaka 2019 hadi asilimia 84.7 kwa mwaka 2020.


William Bundala Mwakilishi wa mgodi wa Bulyanhulu akizungumza katika hafla ya PIP Nyang'hwale. (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).

Kwa upande wake William Bundala ambaye ni Mwakilishi Meneja Mgodi Bulyanhulu unaomilikiwa na Barrick amesema kupitia kamati ya maendeleo ya jamii ya mgodi huo (CDC) ilitenga milioni 50 kwa ajili ya mradi huo wa PIP.

Amesema kuwa mgodi huo umetoa vitabu zaidi ya 1,300 kwa masomo mbalimbali kwa shule 10 za sekondari Wilayani humo,wamekabidhi tuzo kwa wanafunzi bora 1,500,000/ Wazazi wa wanafunzi bora 1,500,000/ walimu ambao masomo yao yalipata alama za juu zaidi 2,858,000/ shule zilizo fanya vizuri kwa uwiano wa kijinsia 1,000,000/ na shule zilizoshika nafasi ya juu zaidi katika Wilaya 900,000/.

Barrick kupitia mgodi wake wa Bulyanhulu mwaka huu kupitia fedha za CSR itatekeleza miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale yenye thamani ya 1,265,000,000.

Mariam Chaurembo Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Nyang’hwale amesema Mpango huo wa PIP umeonya mafanikio makubwa kwasababu matokeo ya kila mwaka ya kidato Cha nne yamekuwa yakipanda ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Amesema kuwa Halmashauri hiyo imewekeza nguvu kubwa katika sekta ya elimu na zaidi ya milioni 800 zimeelekezwa katika elimu.

Ameongeza kuwa juhudi kubwa zinafanywa ili kuendeleza kuboresha kiwango Cha ufaulu mzuri kwa kuzingatia pia maslahi ya walimu.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale, Wilson Shimo (wa kwanza kulia) na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale, Mariam chaurembo ( mwenye kitambaa kichwani) wakiwa na baadhi ya wadau wa maendeleo Wilayani humo(picha na Robert Kalokola).

Amesema kwa maelekezo ya serikali kuu,mwaka huu wanapandisha madaraja walimu wote wanaostahili kupanda na kulipa madeni yao yote.

Wilaya ya Nyang'hwale imeingia mwaka wa pili tangu kuanzishwa kwa PIP ili kuboresha ufaulu na mkakati uliopo ni kuboresha zaidi mpango huo ili uweze kuwa na tija zaidi.

Post a Comment

0 Comments