Shaka:Tathimini inaonesha Muhambwe, Buhingwe CCM itashinda kwa kishindo

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema tathimini ya awali katika uchaguzi mdogo kwenye majimbo mawili ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma imeonesha chama hicho kitashinda kwa asilimia 80, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka akizungumza leo Mei 13, 2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari amesema CCM itashinda Buhingwe na Muhambwe kwa haki, amani na utulivu mkubwa.

Kampeni za CCM katika Majimbo yote mawili zinatarajiwa kufungwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Philip Isdor Mpango Mei 14 na 15,2021 katika uwanja wa Taifa kwa Jimbo la Muhambwe na uwanja wa shule ya Mayama kwa jimbo la Buhigwe.

Shaka amesema, wananchi wa majimbo hayo wanatakiwa kuhakikisha wanawachagua wagombea ubunge wa Chama hicho ili waendelee kutekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo na kusimamia Ilani.

Amesema, pamoja na yote sababu kubwa za ushindi wa chama hicho ni imani kubwa walionayo wananchi kwa Rais Samia Suluhu Hassan na CCM.

"Chini ya uenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan tutaendelea kuvilea vyama vya siasa nchini ili viendelee kufanya siasa safi na yenye tija kwa Taifa baada ya kufanya siasa za danadana, kwani sote tunajenga nyumba moja hakuna sababu kugombeana fito,"amesema na kuongeza;

"Ikumbukwe kuwa tokea siasa za nchi hii kuanzia TANU hatimaye CCM Chama chetu hakijawahi kufanya makosa katika mambo ya msingi yanayohusu maslahi ya Taifa tunakumbusha kuwa uchaguzi wa Buhingwe na Muhambwe umebeba maslahi mapana ya Taifa kwa maana unakwenda kuzalisha wabunge wanaokwenda kumuunga mkono Rais Samia,"amesema.

Pia amesema, CCM imejipanga kuhakikisha wanachama wao waliojiandikisha wanajitokeza kwa wingi katika vituo vya kupiga kura na kuwachagua wabunge wanaotokana na Chama chao pendwa cha CCM katika kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na kisiasa hivyo hatuwezi kufanya makosa.

Shaka ametoa wito kwa vyama vingine na wananchi kwa ujumla kuendelea kudumisha amani, usalama na utulivu ambao umekuwepo wakati wote wa kampeni zetu.

Akizungumzia mwenendo wa uchaguzi kwenye majimbo ,Shaka amesema chama hicho kilifanya uzinduzi wa kampeni za ubunge katika jimbo la Muhambwe Mei 4, 2021 na Jimbo la Buhigwe Mei 5, 2021 ukiongozwa na Waziri Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, Kassim Majaliwa.

Pia amesema,wamefanya tathimini fupi ya kampeni za uchaguzi mdogo wa marudio katika majimbo hayo ya Muhambwe na Buhigwe kwa lengo kubwa la kampeni za CCM ni kutangaza sera na Ilani ya CCM, kuwaeleza wananchi jinsi tulivyojipanga kuwaletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

"Kwa Jimbo la Buhigwe wananchi wenyewe wanataka kumpa ahsante, Rais Samia kwa kumteua Makamu wa Rais aliyekuwa mbunge wao Dkt Philip Mpango.

CCM imedhihirisha kivitendo uwezo wake mkubwa wa kuwatumikia wananchi katika awamu zote za uongozi. Kazi kubwa ya kisera na utekelezaji wa miradi, kuondoa kero imefanyika chini ya CCM kwenye majimbo ya Muhambwe na Buhigwe hivyo ushindi wa CCM ni jambo lisilo na shaka wala wasiwasi,"alisema..

"Wakati wote wa kampeni wananchi wamejitokeza kwa wingi kuhudhuria katika mikutano yetu ya Kampeni jimboni humo na kuonesha matarajio yao kwa mgombea wa CCM ,Dkt. Samizi Kavejuru amefanya kampeni katika Kata zote 20, na kukutana na wananchi katika Vijiji 44 sawa na asilimia 100 ya vijiji vyote na anaendelea kumalizia kampeni katika vitongoji vinane vilivyobaki kati ya 192,"amesema Shaka.

Ameongeza kwamba, mikutano mikubwa imefanywa kimkakati katika viwanja vya Shule ya Msingi Buhigwe, Munanila, na Muyama maeneo hayo yana wakazi wengi waliojiandikisha katika kupiga kura Mikutano midogo 62 aliyoifanya Mgombea wa CCM Ndugu Kavejuru pamoja na mazungumzo mahsusi na makundi ya kijamii yamemkutanisha na kumpa uhakika zaidi wa kupata ushindi .

Hata hivyo, amesema chama chao kimezishirikisha jumuiya zake zote katika kampeni za majimbo ya Muhambwe na Buhigwe pamoja na kuwatumia makada wake mbali mbali ambao wote wakiwa na lengo moja la kupata ushindi.

Post a Comment

0 Comments