Wafuasi 27 wa CHADEMA wafutiwa kesi

Leo Mei 5, 2021 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imefuta kesi ya kufanya mkusanyiko na kuvunja geti la Gereza la Segerea inayowakabili wafuasi 27 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI.
Miongoni mwa wafuasi wa CHADEMA walioachiwa huru. (Picha na DW/Maktaba).

Uamuzi huo umefikiwa baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuleta mashaidi mahakamani hapo ambapo washtakiwa ni pamoja na wabunge wa viti maalumu Halima Mdee (41) Mbunge Ester Bulaya (40) na Jesca Kishoa (36).

Wengine ni aliyekuwa Meya wa Ubungo, Boniface Jakobo, Patrick Assenga, Henry Kilewo,Yohana Kaunya, Kedmony Mhembo, Mshewa Karua, Khadija Mwago, Pendo Raphael maarufu kama Mwasomola na mkazi wa Bonyokwa, Cesilia Michael, Happy Abdalla; Stephen Kitomari na Paul Makali, Edgar Adelinj na Reginald Masawe.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi amesema chini ya kifungu cha 225(5) cha Makosa ya Jinai (CPA), baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani.

"Kesi hii imeshakuwa na maahirisho kwa muda mrefu, kwa hiyo naifuta chini ya kifungu cha 225(5)," amesema Hakimu Shaidi.

Hata hivyo, kifungu hicho hakizuii washtakiwa hao kushtakiwa tena pale ushahidi utakapokamilika na kesi kufunguliwa.

Kabla ya kesi hiyo kufutwa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mkunde Mshanga akisaidiana na Wakili wa Serikali, Ester Martin walidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa, lakini hawana shahidi hivyo wanaomba Mahakama kuipangia tarehe nyingine ya kusikilizwa.

Katika kesi hiyo, upande wa utetezi umewakilishwa na Wakili Peter Kibatala na Edson Kilatu, ambapo mara kwa Mara waliomba Mahakama ifute kesi hiyo kwa sababu upande wa mshtaka umeshndwa kuleta mashahidi mahakamani hapo.

Washtakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashtaka saba yakiwemo ya kutoa lugha ya kuudhi kuharibu mali, kufanya mkusanyiko usio kuwa wa halali na kutokutii amri halali iliyowekwa na Jeshi la Magereza na shambulio.

Ilidaiwa kuwa Machi 13, 2020 , eneo la Gereza la Segerea, lililopo wilaya ya Ilala, kwa makusudi washtakiwa walikaidi amri halali ya kuondoka eneo la gereza kwa amani ili eneo hilo libaki wazi, amri hiyo iliyotolewa na askari mwenye namba B 3648, Sajenti John ambaye ni mlinzi wa Geti la gereza hilo.

Katika shtaka pili ambalo ni la kufanya mkusanyiko, washtakiwa wanadaiwa kukusanyika isivyo halali kwenye geti la Gereza la Segerea na kusababisha hofu iliyokuwa inapelekea uvunjifu wa amani na utulivu.

Pia washtakiwa hao wanadaiwa kuharibu geti kuu la kuingilia na kutokea katika Gereza la Segerea mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanznia huku, Mdee, Bulaya na Jacob wakidaiwa kutoa lugha ya matusi kwa askari Magereza mwenye namba B 3648, Sajenti John.

Hata hivyo,mshtakiwa Jacob pia anadaiwa kumshambulia askari Magereza Sajente John kwa kumvuta shati na kumchania, wakati akiwa katika utekeleza wa majukumu yake ya ulinzi kwenye geti kuu la gereza la Segerea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news