MBOWE: CHADEMA TUPO IMARA, NIPO TAYARI KUPATA MRITHI

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

"Natangaza kuwa mwaka 2023 utakuwa mwaka wa uchaguzi mkuu wa chama chetu (Chama cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA) katika ngazi zote kuanzia ngazi ya shina, tawi, wilaya, mkoa hadi Taifa kwa nchi nzima na Mwenyekiti wa Taifa atachaguliwa mwezi Desemba 2023;
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe huku akibainisha kuwa, uchaguzi huo utawezesha kupata viongozi watakaokiongoza kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2025.

Mheshimiwa Mbowe alikuwa akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho Kanda ya Magharibi katika mkutano uliofanyika mkoani Tabora.
Mheshimiwa Mbowe amesema kuwa,licha ya changamoto za hapa na pale wanazokumbana nazo katika kupigania demokrasia hapa nchini bado wapo imara na wameendelea kuungwa mkono na wananchi wengi hususani vijana nchini.

Pia amewapongeza watangulizi wake akiwemo Mwasisi wa chama hicho, Mzee Edwin Mtei kwa kukijengea msingi imara na kubainisha kuwa amekitumia kwa muda mrefu sana na sasa kina watu makini wenye maono mapya wanaoweza kukiongoza kwa mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Mbowe amefafanua kuwa, chama hicho kinapendwa na watu wengi na kina wasomi wazuri wenye maono na uwezo mkubwa hivyo akatoa wito kwa yeyote anayetaka kugombea kuanzia sasa ajiandae huku akibainisha kuwa yuko tayari kuondoka katika nafasi hiyo.

Mheshimiwa Mbowe amesisitiza kuwa, dhamira ya chama chochote cha siasa ni kushika dola hivyo akaeleza kuwa dhamira yao ya kuingia Ikulu bado ipo pale pale na milango iko wazi kwa mtu yeyote anayetaka kujiunga na chama hicho ili kuongeza nguvu.

"Sina tatizo na mtu yeyote mwenye maono mapya ya kimaendeleo atakayejitokeza kunirithi, tunataka damu mpya, niko tayari kumpa ushirikiano, tunataka kukijenga upya kwa kasi ya ajabu na kukifanya kuwa cha kidigitali zaidi,"ameongeza Mheshimiwa Mbowe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news