Rais Samia ampongeza António Guterres kwa kuchaguliwa UN tena

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amempongeza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kwa kuchaguliwa tena katika nafasi hiyo kubwa duniani kwa kipindi cha pili,Anaripoti GODFREY NNKO.
António Guterres (kulia) akila kiapo cha kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha pili mbele ya Rais wa Mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Volkan Bozkir Juni 18, 2021. (Picha na Eskinder Debebe/UN).

"Hongera Mheshimiwa Katibu Mkuu, António Guterres kwa kuchaguliwa kwako tena kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Kujitolea kwako kwa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi duniani kunastahili kupongezwa sana,"ameeleza Rais Samia kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Juni 18, 2021, Mheshimiwa  António Guterres ameapishwa kuendelea na wadhifa huo wa Ukatibu Mkuu kwa kipindi cha pili.

Mheshimiwa Guterres ameahidi kusaidia Dunia kuondokana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) kwani kwa sasa ndio kipaumbele chake muhimu.

Ameyasema hayo baada ya kula kiapo katika Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mbele ya Rais wa baraza hilo, Volkan Bozikir na wawaklishi wa nchi wanachama.

Mheshimiwa Guterres amesema, anatambua dhamana kubwa aliyobeba katika kipindi hiki muhimu zaidi duniani.

“Hakika tuko katika njiapanda, tukikabiliwa na maamuzi yatakayokuwa na athari kwetu. Mienendo inabadilika. Kanuni za awali zinabadilishwa,tunaandika historia yetu wenyewe kwa maamuzi tunayopitisha hivi sasa.

"Inaweza kuwa pande zozote kuvunjika na kusongesha majanga au kusonga na kuleta matumaini kwa mustakabili usioharibu mazingira na bora kwa kila mtu. Kuna sababu za kuwa na matumaini,”amesema Mheshimiwa Guterres.

Bw.Guterres alikuwa mgombea pekee kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa. Awamu yake ya kwanza ilianza mwezi Januari mwaka 2017.

Aliteuliwa na nchi yake Ureno na kupitishwa kwa kauli moja na Baraza Kuu kabla ya idhinisho kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kushika wadhifa huo kwa awamu ya pili kuanzia Januari 2022 hadi Desemba 2026.

Pia Guterres amechambua jinsi virusi vya Corona vimesababisha vifo, vimesambaratisha mbinu za kujipatia kipato huku ikifichua ukosefu wa usawa.

Aidha, amesema kuwa licha ya changamoto hiyo kubwa duniani, nchi nyingi zinakabaliwa na changamoto kama vile mabadiliko ya tabianchi na kupotea kwa bayonuai.

Amesema, ni muhimmu sana kuondoakana na janga la Corona na wakati huo huo mwelekeo wa kujikwamua kiuchumi na kijamii unapaswa kufanyika katika misingi ya haki.

“Changamoto yetu kubwa ambayo wakati huo huo ni fursa kubwa zaidi ni kutumia janga hili kubadili mwelekeo, kusonga kuelekea Dunia iliyojifunza na inayosongesha haki, uchumi usioharibu mazingira kwa kuimarisha ushirikiano fanisi wa kimataifa na kushughulikia changamoto za kimataifa,”amesema Guterres.

Ameelezea imani yake kwamba yanaweza kutekelezwa kwa mafanikio makubwa kutokana na mambo kadhaa ikiwemo kujituma kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa duniani kote, lakini kukiambatana na umuhimu wa kuboresha kile wanachofanya sasa, kufanya uchambuzi wa kina wa takwimu na kupunguza urasimu usiokuwa wa lazima.

Hata hivyo, ametoa wito kwa nchi kutumia fursa ya sasa ya mabadiliko wakati akisisitiza pia umuhimu wa kujumuisha sauti za makundi mengine kwenye meza ya mazungumzo yakiwemo mashirika ya kiraia, sekta binafsi na vijana.

Post a Comment

0 Comments