RAIS SAMIA ASHUSHA NEEMA KILOSA

Na Munir Shemweta-WANMM Kilosa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameshusha neema kwa wananchi wa Kilosa kwa uamuzi wa kufuta jumla ya mashamba 11 yenye ukubwa wa ekari 24,119 katika wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro na kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji na uwekezaji.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa Kimamba wakati akitangaza maamuzi ya Rais Samia Suluhu Hassan kufuta mashamba 11 yenye ukubwa wa ekari 24,119 wilayani Kilosa mkoani Morogoro leo tarehe 7 Juni 2021.

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia ufufuaji wa mashamba 49 yenye ukubwa wa ekari 45,788.5 yaliyotaifishwa miaka ya nyuma huku na wananchi wakiwa hawana uhakika nayo ambapo Mhe. Rais ameelekeza sehemu kubwa ya mashamba hayo kutumiwa na wananchi kwa shughuli za kilimo. 

Uamuzi huo wa Rais Samia Suluhu Hassan unetangazwa leo tarehe 7 Juni 2021 wilayani Kilosa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza kwa nyakati tofati na viongozi, watendaji na wananchi wa kijiji cha Kimamba wilayani Kilosa wakati wa ziara yake mkoani Morogoro. 

Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema pamoja na kufutwa mashamba hayo haimaanishi kama yako huru kwa kila mtu kujichukulia bila utaratibu na timu maalum imeundwa kwa ajili ya kupanga matumizi ya ardhi katika mashamba hayo na kutahadharisha asitokee mtu yeyote kuzuia timu hiyo kufanya kazi yake.
Baadhi ya wananchi wa Kimamba wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi (hayupo pichani) wakati wa kutangaza kufutwa mashamba 11 yenye ukubwa wa ekari 24,119 wilayani Kilosa mkoani Morogoro tarehe 7 Juni 2021.

“Lazima tupange matumizi ya mashamba yaliyofutwa na utaratibu utaelekezwa na viongozi wa mkoa na wilaya na isitokee mtu kuja kujigawia mashamba na kila kipande cha ardhi kitapangwa na lazima ijukikane nani anamiliki,”alisema Lukuvi. 

Akielezea zaidi kuhusiana na mashamba 49 yenye ukubwa wa ekari 45,788.8 yaliyofufuliwa, Waziri Lukuvi alisema ekari 30,672.2 kati ya hizo lazima zirudi kwa wananchi na ekari 15,116.3 zilizobaki zipangiwe kwa ajili ya matumizi ya uwekezaji. 

Kwa mujibu wa Lukuvi, wananchi watakaopewa mashamba ni wale wasiokuwa na ardhi kabisa na asingependa ardhi itolewe kwa watu wenye nia ya kujilimbikizia maeneo na kusisitiza anachotaka ni mashamba yasaidie wale wananchi wa kilosa kwa kujipatia kipato na kuinua maisha. 

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shighela alimshukuru Mhe Rais kwa uamuzi wa kufuta na kufufua mashamba katika wilaya ya Kilosa na kueleza kuwa sasa mkoa wake unaenda kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa upangaji matumizi ya mashamba hayo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na viongozi wa wilaya ya Kilosa pamoja na watendaji wa vijiji vya Kimamba, Mvumi na Ilonga wakati akitangaza maamuzi ya Rais Samia Suluhu Hassan kufuta mashamba 11 yenye ukubwa wa ekari 24,119 wilayani Kilosa mkoani Morogoro leo tarehe 7 Juni 2021.

Alisema, hatasita kuchukua hatua kwa viongozi wa ngazi za vijiji watakaohusika kwa namna moja ama nyingine kuondoa utulivu wakati wa zoezi la kupanga matumizi ya mashamba yaliyofutwa na hatua hizo zitachukuliwa hata katika ngazi ya chama kwa watakaohusika. 

Naye Mbunge wa jimbo la Kilosa ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi mbali na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi aliyoyachukua kufuta mashamba 11 na kuridhia sehemu kutolewa kwa wananchi, alisema uamuzi uliofanywa na Rais unawagusa wana Kilosa hasa wana Kimamba na kuwataka kumuumga mkono kwa juhudi anazofanya kuwatumikia wananchi.  

Baadhi ya mashamba yaliyofutwa ni pamoja na Sumagro Ltd lililopo Madoto na lenye ukubwa wa ekari 7,712, Bumagro Ltd Kivungu ekari 5660, M/S Sino Development (T) Ltd lililopo Kimamba ekari 6,945, Abdalah Islam lililopo eneo la Dodoma Isanga ekari 307, Mifugo Magairo la Magole lenye ukubwa wa ekari 489 na shamba la MS Masoni Company lililopo Magole ekari 466. 

Mengine ni Mitibora (T) Ltd ekari 511 eneo la Magoli, Abdalah Islam ekari 307 Isanga Dodoma na Ibrahim Magairo mwenye shamba lenye ukubwa wa ekari 516 lililopo eneo la Magole. 

Katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya mashamba 123 yalihakikiwa katika wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro DC na kati yake mashamba 11 yenye ukubwa wa ekari 24,119 yalibatilishwa na Mhe. Rais kutokana wamiliki wake kukiuka taratibu za uendelezaji.

Post a Comment

0 Comments