DORIA YA KUFUKUZA TEMBO KUANZA LEO WILAYANI NACHINGWEA

Na Happiness Shayo, WMU

Doria ya Askari wa Wanyamapori kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inatarajiwa kuanza leo ili kufukuza tembo waliovamia Kijiji cha Mbute na Ngulichile wilayani Nachingwea mkoani Lindi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (kulia) akisiliza kero za wananchi wa kijiji cha Ngulichile wilayani Nachingwea mkoani Lindi ambapo ameagiza doria za askari wa wanyamapori kuanza leo ili kufukuza tembo waliovamia makazi ya wananchi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kusikiliza changamoto za wananchi iliyofanyika leo wilayani Nachingwea.

“Ninawaagiza askari wa wanyamapori kuhakikisha mnaweka kambi katika vijiji hivi na kuanzia leo mfanye doria ya kuangalia tembo walipo ili kuwarudisha katika maeneo yao ya hifadhi,” Mhe. Masanja amefafanua.

Amesema, doria hizo zitakuwa mwarobaini wa kutatua tatizo la tembo waliovamia makazi ya wananchi katika vijiji hivyo.

“Kambi hii a askari wa wanyamapori katika maeneo haya iwe ya kudumu lakini naelekeza askari waje leo kufukuza tembo ili wananchi waishi kwa amani,” amesisitiza mhe. Mary Masanja.

Mhe. Masanja amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea pamoja na wananchi wa Wilaya hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha ili kukamilisha zoezi hilo.

Aidha, Mhe. Mary Masanja amewaagiza wananchi hao kuanza utamaduni wa kufuga nyuki ili kukabiliana tembo.
Wananchi wa Kijiji cha Ngulichile wakielezea kero yao ya tembo waliovamia makazi yao kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (kulia) wakati wa ziara yake a kikazi ya kusikiliza kero za wananchi wilayani Nachingwea Mkoa wa Lindi.

“Nawaagiza watakapokuja wakufunzi kutoka Wizarani kuwafundisha mbinu mbalimbali za kukabiliana na tembo, mkubali njia hii ya kufuga nyuki kwa sababu nyuki ni adui wa tembo, sehemu ambayo nyuki yupo tembo hawezi kukaa,” Mhe. Mary Masanja ameongeza.

Amefafanua kuwa, ufugaji nyuki utasaidia kurutubisha mazao yao korosho wanayolima ili yaweze kukua vizuri.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya tembo, Diwani wa Kata ya Ngulichile, Mhe. Said Mwakayola amesema kuwa wananchi wanaogopa kwenda kwenye maeneo yao ya shughuli za kila siku kama kisimani na mashambani kutokana na tatizo hilo la tembo.

“Zoezi hili la kufukuza tembo naomba lianze haraka iwezekanavyo kwa sababu watu wanashindwa kwenda hata kwenye mashamba ya mikorosho kuangalia mazao yao kwa sababu ya tembo hawa,” amefafanua Mhe. Mwakayola.

Pia, Mhe. Mwakayola ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa askari wa wanamapori watakaoanza zoezi hilo la kukabiliana na tembo.

Ziara hiyo ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ni mwendelezo wa ziara zake za kikazi za kutatua changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kama tembo wanaovamia makazi ya wananchi katika sehemu mbalimbali nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news