Ni Simba tena, wengine wasukumwa nje, Yanga SC yabakizwa nyuma

NA GODFREY NNKO

Didier Gomes Da Rosa ambaye ndiye Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC ameweka wazi kuwa msimu huu kikosi hicho kimekuwa bora si Tanzania pekee bali Afrika Mashariki nzima.

Amesema, uimara huo ndiyo umewawezesha kung'ara zaidi hadi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya nne mfululizo. Misimu hiyo ni pamoja na 2017/18 ,2018/19, 2019/20 na 2020/21.
Kocha Gomes amesema kikosi ni bora kulinganisha na vingine ndani ya ukanda huu na ndiyo sababu iliyochangia kushinda mitanange mingi huku wakikusanyia magoli ya kutosha.

Ubora huo umempa nguvu zaidi, Kocha Gomes huku akimpongeza uongozi wa klabu chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Bilionea Mohamed Dewji (Mo Dewji).

Sambamba na Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez kwa kumuwekea mazingira mazuri ya kufanya kazi kwa muda wote tangu atue nchini hivyo kuwezesha kuongeza ari na ufanisi wa kufanya kazi.

Amesema, ni matarajio yake baada ya muda watacheza fanali ya Afrika, kwani ubora walio nao ni wa viwango vya hali ya juu.

Kocha huyo amesema, ana matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo wa Fainali ya Azam Sports Federation Cup dhidi ya Yanga SC utakaopigwa Julai 25, 2021 kwenye dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

BOCCOOOOOO!!!

Naye nahodha wa Simba SC, John Raphael Bocco amewapongeza wachezaji wenzake ndani ya klabu hiyo kwa ushirikiano aliopata hasa kutoka kwa washambuliaji Medie Kagere na Chris Mugalu.

Bocco amesema ulikuwa msimu bora kwao kama washambuliaji pamoja na wachezaji wote na kila aliyepata nafasi alifunga na ni moja ya chachu iliyosababisha ubingwa wa msimu huu.

Nahodha huyo ameongeza kuwa ushirikiano baina ya wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki umechangia mafanikio ya msimu huu.

“Kwa dhati niwapongeze washambuliaji wenzangu Kagere na Mugalu kwa ushirikiano walionipa hadi leo, ilikuwa aliye kwenye nafasi anapewa pasi na anafunga.

“Tulikuwa na msimu mzuri, ushirikiano ulikuwa mkubwa kuanzia wachezaji viongozi hadi mashabiki na hilo limechangia pakubwa kufanikisha hili,” amesema Bocco.

Bocco amemaliza akiwa kinara wa ufungaji kwa kutupia nyavuni mabao 16 akifuatiwa na Mugalu mwenye 15 huku Kagere akifunga 13.

WENGINE WAAGA LIGI KUU

Wakati huo huo, Ihefu kutoka Mbeya ambao waliweka mipango mingi kipindi cha mwishoni mwa ligi badala ya kuanza mapema wamehitimisha mbio zao.

Timu hiyo imeshuka daraja msimu huu baada ya kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 na KMC kwenye mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu uliopigwa Julai 18, 2021 kwenye dimba la Uhuru lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Charles Ilamfya kupitia bao alilofunga dakika ya 81 lilipoteza matumaini ya Ihefu kubaki Ligi Kuu kwa msimu ujao kwani ilihitaji ushindi ili kugombea nafasi ya kucheza mechi za mtoano, lakini mambo yaliwaendea kombo.

Aidha, ikiwa ni msimu wake wa kwanza kushiriki Ligi Kuu Bara, Ihefu imeshuka tena na kurudi Ligi Daraja la Kwanza baada ya kumaliza ligi ikiwa na alama 35 ambapo inaungana na Mwadui FC na Gwambina FC ya Mwanza kushuka daraja.

Simba SC katika mchezo wa Julai 18, 2021 walikabidhiwa kombe lao la ligi baada ya kuwa mabingwa wa ligi hiyo kwa kujikusanyia alama 83 katika michezo 34 huku mahasimu wao Yanga wakishika nafasi ya pili wakiwa na alama 74.

Walionogesha ushindi huo ni mshambuliaji wao Meddie Kagere dakika 19 ya mchezo kipindi cha kwanza na bao la pili lilifungwa na Chris Mugalu ambaye alifunga mabao mawili dakika ya 24 na dakika ya 67.

Nahodha wa klabu hiyo John Bocco aliingia kipindi cha pili na kuweza kufunga bao la nne kwa mkwaju wa penati dakika ya 94 na kumuwezesha kuibuka kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo ambayo ilikuwa yakuvutia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news