TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MAONESHO YA KIKANDA YA UTALII YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI MWEZI OKTOBA 2021

Na Lusungu Helela, WMU

Tanzania inatarajia kuwa Mwenyeji wa Maonesho ya Kikanda ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ( EAC Regional Tourism EXPO) yatakayofanyika mwezi Oktoba mwaka huu jijini Arusha.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza kwenye Mkutano wa Kisekta wa Baraza la Mawaziri wa Utalii na Wanyamapori wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya Mtandao jana akiwa jijini Arusha ambapo amewaeleza Mawaziri hao kuwa Tanzania ipo tayari kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Kikanda wa Utalii wenye lengo la kutangaza kwa pamoja fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika ukanda huo, mkutano huo utafanyika mwezi Oktoba mwaka huu Jijini Arusha.

Akizungumza jana Jijini Arusha kwenye Mkutano wa Kisekta wa Baraza la Mawaziri wa Utalii na Wanyamapori wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya Mtandao, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro aliwaeleza Mawaziri hao kuwa Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa Maonesho hayo huo.

Waziri Ndumbaro alilitoa ombi hilo mara baada ya Burundi aliyetakiwa kuwa mwenyeji wa Maonesho hayo kutokuwa tayari kuyafanya kwa mwaka huu na hivyo kuahidi kuwa atakuwa tayari mwakani, hali hiyo ikailazimu Tanzania kuomba na kisha kukubaliwa kuwa Mwenyeji wa Maonesho hayo.

Alisema, lengo la Maonesho hayo ambayo ni ya kwanza kufanyika kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ni kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika nchi hizo.

Alisema, makubaliano hayo ya kuanzisha maonesho hayo ni hatua mahsusi kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kujitangaza baadala ya kutegemea makampuni makubwa ya utalii kutoka nje kutangaza vivutio vilivyopo katika Jumuiya hiyo kwa namna yanavyotaka yenyewe.

Akizungumza katika mkutano huo, Dkt.Ndumbaro amewaelezea Mawaziri hao kuwa maonesho hayo ya Utalii nchini Tanzania kufanyika kwake itakuwa ni hatua muhimu ya kuwatia nguvu sekta binafsi ya kuona namna ya kujipanga upya kurudi katika biashara ya utalii kutokana na ugonjwa wa UVIKO kuitikisa vibaya sekta hiyo.

Alisema, athari za ugonjwa wa UVIKO 19 umedumaza Makampuni binafsi yanayojihusisha na utalii na hivyo kupelekea kupunguza idadi ya wafanyakazi wa sekta na hivyo kuongeza tatizo kubwa la ajira nchini

"Kwa vile Burundi imeonesha kutokuwa tayari, Sisi Tanzania tupo tayari kufanya Maonesho hayo kwa mwaka huu ikiwa lengo letu kutuma ujumbe kwa mataifa makubwa kuwa tupo tayari kuwapokea na kuwahudumia watalii," alisisitiza Dkt.Ndumbaro.

Katika hatua nyingine Tanzania imeendelea kushikilia msimamo wake wa kuomba muda zaidi wa kujiandaa kujiunga kwenye Visa ya pamoja ya Utalii.

Akifafanua katika mkutano huo, Waziri Dkt.Ndumbaro aliwaeleza Wajumbe hao kuwa suala viza ya pamoja ya utalii kwa Tanzania ni suala nyeti na linahusisha mamlaka zaidi ya moja katika kufanya maamuzi hivyo inaomba ipewe muda zaidi kwa ajili ya kuweza kufikia maafikiano na mamlaka zingine hususana mamlaka ya uhamiaji na usalama.

Alisema,  suala la visa ya pamoja ya utalii linahitaji makubaliano ya ndani kwanza kabla Tanzania haijaamua kujiunga nayo suala ambalo mjadala wake wa kuitaka Tanzani kujiunga liliungwa mkono kwa nguvu sana na Mawaziri wa kutoka nchini Kenya pamoja na Uganda

Licha ya mjadala huo kuchagizwa na Mawaziri hao, Dkt.Ndumbaro alisema suala la viza ya pamoja ni muhimu kibiashara lakini linagusa usalama wa nchi na hivyo aliwashauri Mawaziri hao liache liamuriwe na mamlaka zingine ikizingatiwa kuna Tanzania bara na Tanzania Visiwani.

Katika Mkutano huo ulihudhuriwa na Mawaziri wote wenye dhamana ya utalii na wanyampori kutoka nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kutoka Tanzania, Kenya Uganda, Sudani pamoja na Rwanda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news