UVCCM Kinondoni waandaa kongamano kubwa la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan

Na Anneth Kagenda, Diramakini Blog

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kinondoni (UVCCM) mkoani Dar es Salaam umeandaa kongamano kubwa la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke Tanzania na Rais wa 3 Afrika akiwa mwanamke pia.

Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu.
Akizungumza na DIRAMAKINI Blog ofisini kwake, Mwenyekiti wa UVCCM, Liliani Lwebangila amesema kuwa, kongamano hilo pia litakuwa ni kuwahamasisha wasichana kuwa wavumilivu na kuamini kwamba siku moja watakuwa viongozi tena wakubwa ndani ya nchi yao.

Amesema kuwa, wao wakiwa ni vijana wa chama hicho wanatambua jukumu kubwa alilonalo Rais Samia, hivyo wameona ipo haja ya kumpongeza na kuendelea kumtia moyo katika utendaji kazi yake.

Amesema, wakati wa kongamano hilo wanategemea pia kuwatambua viongozi wanawake waliopata nafasi za uongozi kwa kuwashinda wanaume wakati wa kinyanganyilo cha kutafuta uongozi husika.

"Mfano kuna viongozi wanawake ambao wamepita kwenye nafasi za wabunge wa Majimbo, Madiwani, viongozi wa Kata wa kuchaguliwa na kuwashinda wanaume, wenyeviti wa Chama pamoja na Makatibu," amesema Mwenyekiti Liliani.

Aidha, amesema kuwa itatolewa zawadi kwa Rais huku viongozi hao waliowashinda wanaume kwenye vinyang'anyiro hivyo wakitunukiwa vyeti.

Post a Comment

0 Comments