DC Dkt.Ningu arejesha tabasamu kwa wanavijiji Namtumbo

Na Yeremia Ngerangera, Namtumbo

MKUU wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Dkt.Julius Keneth Ningu amepewa jina la Baba Namtumbo katika Kijiji cha Mchomoro wakati wa mkutano wa hadhara wa wananchi wa Kata ya Mchomoro kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia majawabu.
Akiongea baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara, mwananchi wa Kijiji cha Mchomoro, Adija Kapata alisema, kwa namna mkuu wa wilaya huyo alivyosikiliza kero zao na kuzipatia majawabu wananchi wa Kata ya Mchomoro wanamwita Baba Namtumbo.

Dkt.Ningu alifanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Mchomoro kusikiliza kero zilizowasilishwa kwake kutoka kijiji cha Songambele,Masuguru,Mchomoro na Kilimasera kuhusu migogoro inayoendelea kati ya wafugaji na wakulima katika kata hiyo.

Katika mkutano huo Ningu alitoa nafasi kwa wananchi upande wa wakulima na wafugaji kutoa kero zao kwa kutoa ushahidi wa kuthibitisha kero wanazotoa na mara baada ya kusikiliza pande zote, Dkt. Ningu alitoa majawabu ya kero zao.

Issa Kandimwa ambaye ni mkulima wa Kijiji cha Masuguru alimthibitishia mkuu wa wilaya na kumuonesha majeraha ya mikuki aliyokuwa amepigwa na wafugaji wakati akipambana na wafugaji hao kulisha mifugo yao katika mazao yake na kutoa ushahidi wa kuripoti kituo cha polisi bila kupatiwa ushirikiano.

Naye Saidi Hasani Kinombo kutoka kitongoji cha Mingwea Kijiji cha Mchomoro alimwambia mkuu wa wilaya ya Namtumbo kuwa, wananchi ya Kata ya Mchomoro hawapo tayari kuona maeneo yao ya kilimo yakiharibiwa na mifugo na wao kushindwa kuendesha shughuli za kilimo kama huko nyuma kwa sababu ya wafugaji.

Aidha, Kinombo aliongeza kuwa kama sivyo ndivyo wananchi wa Kata ya Mchomoro wahamishwe na Serikali wapelekwe sehemu yoyote katika nchi hii ambayo wanaweza kuendesha shughuli zao za kilimo bila kugombana na wafugaji na Kata ya Mchomoro wabaki wafugaji hao.

Baada ya kauli hiyo, Christina Nangai alionesha kutokwa na machozi na kumuomba mkuu wa wilaya kuwa sio wafugaji wote ni wakorofi bali wapo wachache na hata wakulima wengine nao ni wakorofi, sio wote hivyo akamuomba kujenga mahusiano ili wafugaji hao wasiondolewe katika maeneo wanayokaa.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo alisema migogoro katika wilaya ya Namtumbo kati ya wafugaji na wakulima inazidi kuongezeka kutokana na wafugaji kuthamini zaidi mifugo yao kuliko mazao ya wakulima na hilo linajitokeza kutokana na malalamiko mengi katika ofisi yake ni wafugaji kulisha mazao ya wakulima na kwa kuwa wilaya haikutenga eneo la kulisha mifugo hiyo, hilo ndilo tatizo lililopo kwa sasa.

“Wafugaji ni raia wa Tanzania na wana haki ya kuishi popote katika nchi hii ilimradi hawavunji sheria, wapokeeni wafugaji wanaotaka kuishi katika vijiji vyenu, lakini hakuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kulisha mifugo yao katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo,”alisema Dkt.Ningu.

Kutokana na kuepuka migogoro inayotokea na inayotarajia kutokea kwa sasa kama hali hii ikiendelea wilaya ya Namtumbo kuanzia Septemba 11, mwaka huu itaendesha zoezi la kuondoa mifugo iliyopo katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Mkutano wa hadhara huo ulifanyika katika kiwanja cha ofisi ya Kijiji cha Mchomoro ambapo wakulima na wafugaji katika Kata ya Mchomoro walipewa nafasi ya kuuliza maswali yao,kero zao,maombi yao na baada ya kuhitimisha mkutano huo walimpa jina mkuu wa wilaya huyo, Baba Namtumbo kwa namna alivyoweza kuwapa majawabu ya kero zao za muda mrefu.

 

MUHIMU

UNATAMANI DIRAMAKINI BLOG TUWE HEWANI SAA 24 KUKUPA HABARI ZA KINA KILA DAKIKA, TUNAOMBA UTUUNGE MKONO KWA KUCHANGIA GHARAMA ZA MAWASILIANO NA INTANETI KWA WAANDISHI WETU POPOTE WALIPO NDANI NA NJE YA TANZANIA; TUNAPOKEA MCHANGO WAKO KUPITIA 0719254464 (Tigo Pesa-Godfrey Nnko) AU UKIHITAJI NAMBA YA BENKI TUJULISHE. MUNGU AKUBARIKI SANA KWA SAPOTI YAKO. ASANTE

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news