Mohamed Jumaa mbaroni kwa kuwaua walinzi wawili baada ya kuwagonga

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia Mohamed Jumaa (37),Mkazi wa Kariakoo kwa tuhuma za mauaji ya walinzi wawili waliofahamika kwa majina ya Eliakim Morali(30), Mkazi wa Mbezi Beach, Mlinzi wa Kampuni ya LOCK FORT SECURITY na Saunkoo Bakari(35) mkazi wa Buguruni ambaye ni mlinzi binafsi (baunsa).
Hayo yamebainishwa leo Agosti 27,2021 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,Muliro Jumanne Muliro.

Amesema,tarehe 26 Agosti, 2021 majira ya saa 12 jioni huko eneo la Tungi Wilaya ya Kigamboni katika kituo cha kuuzia mafuta cha JM PETROL STATION, mtuhumiwa aliwaua walinzi hao kwa kuwagonga kwa makusudi na gari lenye namba T 176 CVP aina ya DAF lori lililokuwa na tela ambalo halina namba za usajili.

“Mtuhumiwa alifika katika kituo hicho cha kuuzia mafuta cha JM PETROL STATION alichokuwa ana kimiliki kwa ajili ya kuhamisha mali zake, lakini alichukua gari lake na kutoka nje ya kituo na ghafla alirudi nalo kwa kasi huku likiwa halina tela.

"Na kuwagonga walinzi hao waliokuwa getini na kupelekea kufariki dunia papo hapo na kuwajeruhi watu sita ambao walikimbizwa hospitalini kwa matibabu,”amesema.

“Mtuhumiwa huyo alikuwa na kesi ya madai namba 118/2018 Mahakama Kuu iliyofunguliwa na ACCESS Bank baada ya kushindwa kulipa mkopo kwa muda muafaka aliochukua katika benki hiyo na mtuhumiwa alishindwa Mahakamani licha ya kukata rufaa mara kadhaa na hatimaye Mahakama ilitoa amri ya kuuzwa kwa kituo chake cha kuuzia mafuta maarufu kama JM PETROL STATION kilichopo Kigamboni,”amesema.

Aidha, amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linaendelea na uchungunguzi wa kina juu ya tukio hili na mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani hivi karibuni kujibu tuhuma zinazomkabili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news