NEC YATANGAZA UCHAGUZI MDOGO MAJIMBO YA KONDE,USHETU

Na Mwandishi Maalum, Dodoma

TUME ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza kuwepo kwa nafasi mbili za Ubunge katika majimbo ya Konde mkoa wa Kaskazini Pemba na Ushetu mkoani Shinyanga.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Njedengwa jijini Dodoma leo Tarehe 27 Agosti, 2021.

Akizungumza na Vyombo vya habari leo tarehe 27 Agosti 2021, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera amesema uchaguzi huo mdogo wa marudio umepangwa kufanyika Oktoba 9,2021.

“Ratiba ya uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba na Jimbo la Ushetu Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga ipo tayari,”alisema Dkt. Mahera.

Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye Kumb. Na. CEA.137/400/02/111 ya tarehe 16 Agosti 2021, akiitaarifu kuhusu kuwepo kwa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Ushetu Mkoani Shinyanga.

Nafasi hiyo inatokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Elias John Kwandikwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Dkt.Mahera amesema taarifa hiyo ya Spika ni kwa mujibu wa kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

Aidha, kwa upande wa Jimbo la Konde, Dk Mahera amesema mnamo tarehe 2 Agosti, 2021 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa taarifa kwa umma kuhusu kuwepo wazi kwa Jimbo la Konde lilipo katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba kutokana na mbunge mteule wa jimbo hilo, Sheha Mpemba Faki kujiuzulu.

“Tume ilipokea barua yenye Kumb. Na. CMM/T.40/Vol.I/72 ya tarehe 2 Agosti, 2021 kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikitoa taarifa kuwa Mbunge Mteule wa Jimbo la Konde, ameandika barua, kueleza kwamba hakuwa tayari kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Konde kutokana na changamoto za kifamilia,”alisema Dkt. Mahera na kuongeza kuwa kutokana na hatua hiyo, Tume ililitangaza jimbo hilo kuwa wazi kwa kuwa Mbunge huyo Mteule alikuwa bado hajatangazwa katika Gazeti la Serikali kwa mujibu wa kifungu cha 81(c) (iii) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

Awali mnamo tarehe 18 Julai, 2021 Tume iliendesha Uchaguzi mdogo katika Jimbo la Konde kujaza nafasi iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Khatibu Saidi Haji kupitia chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT –WAZALENDO)

Maandalizi kwa ajili ya uchaguzi huo yameshafanyika na kazi ya utoaji fomu za uchaguzi kwa wagombea inaanza Septemba 13 hadi 19,2021 huku uteuzi wa wagombea watakao wania nafasi hizo ukifanyika Septemba 19 mwaka huu.

Aidha, Dkt Mahera amesema kampeni za uchaguzi katika majimbo hayo ya Ushetu na Konde utaanza Septemba 20, 2021 na zitafikia ukomo wake Oktoba 8 mwaka huu na uchaguzi kufanyika 9 Oktoba ,2021.

Dkt. Mahera amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi inavikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yatakayotolewa na Tume katika kipindi cha Uchaguzi mdogo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news