Prof.Manya awataka wakulima wa chumvi kuwa na takwimu za uwekezaji wao

Na Nuru Mwasampeta-WM

WAKULIMA wa chumvi nchini wametakiwa kuweka vizuri kumbukumbu zao za uwekezaji na biashara ya chumvi ili kuwasaidia wanapohitaji kuomba mikopo kutoka benki na taasisi za kifedha nchini, kwa ajili ya kuendeleza miradi yao.
Wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti na Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya kwa wachimbaji alipofanya ziara ya siku tano katika mikoa ya Lindi na Mtwara na kukutana na changamoto hiyo kwa wachimbaji wa chumvi.

Prof. Manya alisema, ili uweze kuaminiwa na taasisi za kifedha na kukopesheka inakupasa kwanza uwe na leseni ya uchimbaji, uwe na taarifa za mauzo na uoneshe faida inayopatikana kutokana na biashara yako ndipo watu wa benki wakuamini na kukupa pesa.

"Hoja ya takwimu kwa wachimbaji wadogo ni ngumu, je? Ni sababu ya kukwepa tozo. Kuficha ukweli? Au ni nini?alihoji Prof. Manya.

"Mimi naweza kuwa mpiga debe wenu, lakini kama takwimu hazipo itakuwa ngumu kinyume cha hapo hata mimi sitazishawishi benki kuweka pesa hapo," alisisitiza Prof. Manya.

Prof. Manya aliendelea kueleza kuwa, Wizara ya Madini inajivunia kwa kufanikiwa kuifungamanisha Sekta ya Madini na Taasisi za Kifedha ambapo Benki ya CRDB ipo mbioni kutoa kiasi cha dola za Marekani milioni 20 kwa ajili ya kuwekeza kwenye mradi wa kuchimba madini ya kinywe utakaogharimu dola za Kimarekani milioni 30 mpaka kukamilika kwake.

Akizungumzia changamoto ya soko kwa wakulima wa chumvi,Prof. Manya alieleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini ilikaa na Mwekezaji wa Kampuni ya Kneel Salt na aliridhia na kuahidi kuwa atanunua chumvi inayopatikana nchini, "Kama hafanyi hivyo, basi tutamwita na kuzungumza naye kujua shida ipo wapi,"amebainisha.

Aidha, Prof. Manya amemwagiza Kamishna wa Madini kupitia mwakilishi wake wakati wa ziara hiyo, Mhandisi Deogratius Oreku kufanya utafiti na kubaini sababu zilizopelekea kupotea kwa soko la nje la chumvi ambapo alibainisha kuwa awali chumvi ilikuwa ikiuzwa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Burundi.

Kuhusu changamoto ya tozo wanayokutana nayo wachimbaji wa chumvi, Prof. Manya alimwelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Jeremiah Hango kutafuta na kuwasilisha kwa wakuu wa wilaya andiko lililoondoa tozo zingine zote kwa wachimbaji wa chumvi ili wasimamie tozo zinazokubalika pekee.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Salma Kikwete alitaja kazi ya chumvi kuwa ni pamoja na kuungia vyakula na kusema bila chumvi huwezi kuhisi ladha.

Alionesha umuhimu huo wa chumvi na kuiomba Wizara ya Madini kuwafanya wakulima wa chumvi wajione kuwa sawa na wakulima wa korosho na wachimbaji wengine kwa kuwawekewa mazingira rahisi ya kufanya biashara yao kwa manufaa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shahibu Ndemanga aliipongeza Wizara na kusema "Wizara mnatutendea haki sana, hata kukiwa na maswali tuna uhakika wa kujibu sababu mnatuwezesha kujibu".
Akiwasilisha hoja kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Ndemanga alisema, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack anaiomba wizara kusitisha utoaji wa vibali vya kuingiza chumvi kutoka nje ya nchi kwani katika maghala ya chumvi wilayani kwake kuna chumvi ya kutosha kulisha ndani na nje ya nchi.

"Kwa nini chumvi iagizwe nje wakati huku maghala yamejaa chumvi? Chumvi ipo na inaongezeka siku baada ya siku, nadhani suala la kuagiza chumvi lifike mwisho mpaka itakapofaa kufanya hivyo," alisisitiza Ndemanga.

Aliongeza kuwa, chumvi inaajiri watu wengi na kubainisha endapo chumvi itapata soko la uhakika changamoto ya ajira kwa wananchi wa Lindi itakuwa historia.

Kwa upande wao, wakulima wa chumvi waliwasilisha maombi yao ikiwemo kusimamisha uagizaji wa chumvi kutoka nje ya nchi, kutafutiwa soko la uhakika la chumvi inayozalishwa, kutafutiwa fursa ya mikopo kwa riba nafuu na kubwa zaidi kuwezeshwa kupata elimu ya kilimo cha chumvi ili waweze kuzalisha chumvi kwa ubora unaotakiwa.
Mkulima wa Chumvi, Abubakari Maguo akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Shukrani Manya (hayupo pichani) alipokutana na kuzungumza nao katika kijiji cha Mchinga Wilaya ya Lindi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news