Umoja wa Afrika kuipatia Tanzania chanjo dozi milioni 17 za Corona

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Umoja wa Afrika umeitengea Tanzania dozi milioni 17 za chanjo za UVIKO- 19 kupitia mpango wa umoja huo wa kuzisaidia Nchi wanachama kupata chanjo kwa ajili ya Wananchi wake.
Rais wa Ethiopia Mhe. Sahle – Work Zewde akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula(Mb). Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi za Rais Zewde, Addis Ababa, Ethiopia 11 Agosti,2021. (Picha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki).
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameyasema hayo Addis Ababa nchini Ethiopia alipokutana kwa mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania waishio Nchini Ethiopia (Diaspora) waliotaka kufahamu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na UVIKO -19 ikiwa ni pamoja na suala la chanjo.

Aidha, Balozi Mulamula amewataka Watanzania wanaofanya kazi katika Mashirika na Taasisi mbalimbali za Kimataifa kusaidia upatikanaji dozi nyingine za chanjo ya UVIKO 19 ili kuwawezesha Watanzania wengi kupata chanjo hiyo kutokana na mwamko wa Watanzania kuongezeka mara baada ya kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Ethiopia Mhe Sahle – Work Zewde Addis Ababa nchini Ethiopia ambapo Tanzania na Ethiopia zimekubalina kuendelea kutumia ndege za shirika la Ethiopia kutangaza vivutio na kusafirisha Watalii kutoka mataifa mbalimbali kuja Tanzania.

Aidha, Balozi Mulamula amemhakikishia Rais Sahle – Work Zewde kuwa Tanzania itaendelea kutekeleza maeneo yote ya ushirikiano ambayo Rais Zewde alikubaliana na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa ziara ya Rais huyo Chato nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na suala la kuwarejesha Nchini Ethiopia wahamiaji wanaoshikiliwa katika magereza mbalimbali.

Kwa upande wake Rais wa Ethiopia Mhe. Sahle – Work Zewde amesisitiza kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Nchi hiyo hususani katika kutatua changamoto zinazozuia maendeleo miongoni mwa Mataifa hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news