Mihambwe wamuunga mkono Rais Samia chanjo ya UVIKO-19

NA MWANDISHI MAALUM

Wakazi wa Tarafa ya Mihambwe wamehamasika vilivyo kwa hiyari yao kupata chanjo ya UVIKO-19 mara baada ya kuelimishwa na huduma kusogezwa jirani na wananchi.
"Nashukuru sana kupata chanjo ya Corona, niwaombe Watanzania wenzangu tuendane na Dunia ilivyo, na sidhani kuna Mtanzania ama kiongozi yeyote yule anataka kuwatesa Wananchi. Tuchanje ili kupunguza madhara ya ugonjwa huu,"amesema Ndaile Abdallah Ulaya mkazi Kijiji cha Dinyeke.

Muuguzi Asha Kasembe amewahimiza akina Mama na Wananchi wote wapate chanjo kwani ni salama na inaimarisha kinga za mwili na kupunguza vifo na inapunguza makali.

Pia Afisa Tarafa ya Mihambwe, Emmanuel Shilatu ameungana na Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan kupambana na ugonjwa huu kwa kuwapa elimu wananchi, kuwahamasisha na wanaoridhia wanapata chanjo bure.

"Dunia ipo kwenye mapambano ya UVIKO-19 nasi Tarafa ya Mihambwe tunaungana na Rais Samia kupambana na ugonjwa huu kwenye vijiji na vitongoji kuwaelimisha, kuwahamasisha na tumeona watu wengi wamejitokeza kwa hiyari yao kupata kinga kutokana na huduma ya chanjo kuwafikia jirani nao. Nazidi kusisitiza wananchi wa Tarafa ya Mihambwe tuendelee kuchukua tahadhari ya ugonjwa huu wa Corona kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa vitakasa mikono, kuepuka mikusanyiko na kupata chanjo ya sindano ya Corona,"alisisitiza Gavana Shilatu.

Katika zoezi hilo mamia ya wananchi wamejitokeza kupata chanjo ya Corona na zoezi hilo litakuwa endelevu ndani ya Tarafa ya Mihambwe.

Post a Comment

0 Comments