Mkuu wa Wilaya ya Lushoto achana hadharani taarifa ya Kituo cha Afya Gare

Na Yusuph Mussa, Lushoto

MKUU wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Kalisti Lazaro amechana hadharani taarifa ya ujenzi wa Kituo cha Afya Gare kwa kutoonesha thamani halisi ya fedha za ujenzi wake ikiwa ni pamoja na kutobainisha nguvu za wananchi na michango yao waliyotoa.
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro (wa pili kushoto) akiwa ameshika taarifa ya ujenzi wa Kituo cha Afya Gare huku akiangalia majengo yanayojengwa hapo. Baadae aliichana taarifa hiyo hadharani baada ya kutoridhishwa na taarifa hiyo aliyodai ni batili sababu haikuwa na uhalisia wa kazi zinazofanyika hapo. Wengine ni Katibu wa CCM Wilaya ya Lushoto Ramadhan Mahanyu (kushoto), Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi 'Bosnia' (katikati), Diwani wa Kata ya Gare Ernest Sempeo (wa pili kulia) na Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Gare ambaye pia ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Yamba Charles Najigwa (kulia). (Picha na Yusuph Mussa).

Lakini pia taarifa hiyo ambayo ilionesha majengo matano ambayo yapo kwenye hatua mbalimbali huku thamani yake ikionesha ni sh. milioni 61, haikuandaliwa na uongozi wa kijiji, bali imeandikwa na Kaimu Ofisa Mtendaji Kijiji cha Gare Charles Najigwa.

Mkuu wa Wilaya ambaye alifika hapo Septemba 29, 2021 kukagua kituo cha afya hicho, pia alishangazwa kwenye taarifa hiyo kusomewa kuwa hiyo ni zahanati badala ya kituo cha afya, hivyo kuanza kumuhoji mtendaji huyo taarifa hiyo amepata wapi, na nani amemtuma kusema hiyo ni zahanati badala ya Kituo cha Afya Gare.

"Nani amekwambia hii ni zahanati na sio kituo cha afya? Kuna zahanati yenye majengo mengi hivi? Wewe unatumika? Nani amekutuma useme hivi? Hii taarifa imeandaliwa na nani? Nikuulize majengo yote haya yanaweza kugharimu sh. milioni 61 peke yake? Hii taarifa sio sahihi, kaandike taarifa nyingine ikiushirikisha uongozi wa kijiji," alisema Lazaro.

Akijitetea, Najigwa alisema mwanzo ilijengwa kama zahanati, lakini baadae ikabadilishwa na kuwa kituo cha afya.

Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa na Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi 'Bosnia' kwa kusema tangu mwanzo majengo hayo yalikuwa yanajengwa kama Kituo cha Afya Gare, na ndiyo maana wananchi walichangia nguvu zao na kujenga majengo hayo matano yakiwa kwenye hatua mbalimbali.

"Mkuu wa Wilaya, angalia ninavyohujumiwa! hapa tumekuja kukagua Kituo cha Afya Gare, lakini tunasomewa kuwa ni zahanati. Mkuu hizi ni hujuma za wazi wazi juu yangu. Nimepigwa vita sana kwenye kituo hiki cha afya hadi nikashitakiwa TAKUKURU kuwa najipendelea kwetu kwa kuleta fedha nyingi za Mfuko wa Jimbo sh. milioni 20 kwenye zahanati, wakati hiki ni kituo cha afya," alisema Shekilindi.
Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) kwenye Kituo cha Afya Gare. (Picha na Yusuph Mussa).

Shekilindi alidai ujenzi huo hadi sasa umegharimu zaidi ya sh. milioni 200 sababu kuna nguvu za wananchi na wahisani na watu wenye asili ya Kata ya Gare wanaoishi sehemu mbalimbali za nchi ikiwemo mikoa ya Dar es Salaam na Tanga, hivyo kusema ujenzi huo mpaka sasa umegharimu sh. milioni 61 ni kuwakatisha tamaa. Pia wamekuwa wakichanga wakijua hiki ni kituo cha afya, na sio zahanati.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Emmanuel Vuri alisema hicho ni kituo cha afya na sio zahanati. Na halmashauri imetoa sh. milioni 18 ili kukamilisha jengo la OPD (Wagonjwa wa Nje).

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, Lazaro ambaye aliwaita viongozi na wataalamu wote ngazi ya kata na vijiji mbele ya mkutano huo, aliwataka waache kudhulumu watu, kwani baadhi ya viongozi wa vijiji na kata hasa kwenye masuala ya ardhi na mirathi hawatoi haki.

Naye Shekilindi alisema umeme umefika kwenye baadhi ya vijiji na vitongoji kwenye kata hiyo, lakini bado haujawashwa, hivyo akamtaka Meneja wa TANESCO Wilaya ya Lushoto ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo atoe majibu.
Jengo la Mama na Mtoto linalojengwa kwenye Kituo cha Afya Gare kilichopo Kijiji cha Gare, Kata ya Gare. (Picha na Yusuph Mussa).

Shekilindi aliwaeleza wananchi kuwa wameanza kutekeleza ahadi zilizopo kwenye Ilani ya CCM ya 2020-2025, kwani Rais Samia Suluhu Hassan amewapa sh. bilioni tano za utengenezaji wa barabara Jimbo la Lushoto kwa changarawe na kiwango cha lami, na hata baadhi ya madaraja kwenye kata hiyo yamejengwa.

Meneja wa TANESCO Wilaya ya Lushoto Kassim Rajab alisema Novemba, mwaka huu watawasha umeme kwenye vitongoji viwili vya Mvumoi na Mgambo, huku vitongoji vingine 28 vilivyabaki kwenye kata hiyo ya Gare vitafikishiwa umeme mwaka ujao kwenye mpango wa vitongoji.

Post a Comment

0 Comments