NHIF yaja kidigitali zaidi, yawaita Watanzania kupata bima

Na Godfrey Nnko

WATANZANIA wametakiwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wote.
Pia mfuko huo umesisitiza kuwa,umejipanga kuhakikisha unaendelea kuwa imara zaidi ikiwemo kutoa huduma bora kwa wanachama wake popote walipo nchini.

Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa mfuko huo, Charles Lengeju wakati wa mkutano wa waandishi wa habari nchini unaotathmini na kujadili miaka 20 toka NHIF ianzishwe.

Mkutano huo umefanyika Septemba 24, 2021 kwenye Ukumbi wa LAPF jijini Dodoma ambapo amesisitiza kuwa, wameendelea kuimarisha mifumo ya huduma katika vituo mbalimbali nchini ili kumuwezesha kila mwanachama aweze kufurahia huduma anayopatiwa.
Lengelu amesema kuwa, NHIF ambayo ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria Sura 395 na kuanza utekelezaji wake Julai Mosi, 2001 umeendelea kuwa mkombozi kwa wanachama wake ambao wamekuwa wakipatia huduma mbalimbali za matibabu katika vituo vya afya.

"Kuanzishwa kwa mfuko huu ni matokeo ya maboresho katika sekta ya afya yalianza miaka ya nyuma kwa lengo la kusimamia upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watumishi wa umma na wategemezi wao na baadaye kujumuisha makundi mengine ya wananchi wanaojiunga kwa hiari.

"Wakati mfuko unaanzishwa, sheria ililenga kundi la watumishi wa umma peke yake huku sekta binafsi na isiyo rasmi ikiachwa, ndani ya kipindi cha miaka 20, mfuko huu umefanikiwa kufanya maboresho mbalimbali ikiwemo kujumuisha makundi mengine ya wananchi kutoka sekta binafsi rasmi na isiyo rasmi ambayo sasa yananufaika na mfuko huu,"amesema.

Ameyataja makundi hayo kuwa ni pamoja na makampuni binafsi ambayo yanajiunga kwa utaratibu wa mwajiri, kundi la watoto chini ya umri wa miaka 18, wanafunzi kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vya elimu ya juu, wakulima kupitia vyama vyao vya ushirka vya msingi vilivyosajiliwa katika Mpango wa Ushirika Afya.

Lengeju aliyataja makundi mengine kuwa ni pamoja na wananchi katika makundi ya kijamii ya kiuchumi yakijumuisha kundi la wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga), boda boda, mama lishe, familia au mtu mmoja mmoja kupitia mpango wa vifurushi na wengine.
"Ujumuishaji wa makundi haya unalenga kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na fursa ya kujiunga kwa gharama nafuu na hivyo kuwa na uhakika wa matibabu kwa kutumia bima ya afya,"amefafanua.

Mbali na hayo amewapongeza waandishi wa habari kwa kuendelea kuwa daraja muhimu ambalo limekuwa likiwaunganisha wananchi na mfuko kwa kuwapasha taarifa za mara kwa mara juu ya faida zitokanazo na kuwa na bima ya afya.

Amesema, mkutano huu ambao ni wa 14 tangu kuanzishwa kwa mfuko huo umeendelea kuwa na matokeo chanya, hivyo wataendelea kudumisha umoja, ushirikiano kwa lengo la kuhakikisha vyombo vya habari vinazidi kuwa mstari wa mbele kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na bima za afya.

Amesema, mfuko umeendelea kufanya maboresho makubwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo ulipaji wa madai kwa njia ya mtandao ili kuweza kuepukana na udanyanyifu.

Aidha,maboresho mengine ni kushirikiana na benki kuwawezesha wananchi kujiunga na mfuko huo kwa kulipia kwa kudunduliza, hatua ambayo wananchi wengine wameweza kunufaika na hivyo kuweza kuondoka na vikwazo ambavyo vilikuwa vikiwakumba awali.
Wakati huo huo, mfuko huo umeeleza kuwa,umeboresha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuweza kuwasaidia watoa huduma kulipwa madai yao moja kwa moja kutoka Hhspitalini kwa lengo la kuondoa ucheleweshwaji wa malipo.

Mkurugenzi wa Huduma na Wanachama wa NHIF,Christopher Mapunda wakati akiwasilisha mada ya miaka 20 ya mfuko ulipotoka,walipo na wanakoelekea wakati wa mkutano huo wa waandishi wa habari nchini na NHIF.

Mapunda amesema, wamefikia hatua hiyo kwa sababu moja ya changamoto kubwa zilikuwa zinaletwa na watoa huduma ni kuchelewa kwa malipo.

Amesema, kwa sasa kupitia mfumo huo hakutakuwa na ucheleweshwaji kwa malipo huku akieleza pia wameboresha mifumo ya TEHAMA ambayo inawawezesha kufanya usajili wa wanachama kupitia mtandao na mwisho kuweza kulipia michango yao.

Mapunda amesema,kwa sababu madai yatakuwa yakichakatwa kila siku na mwisho wa siku mfumo umewezesha kulipa madai hayo ndani ya siku 14 tangu kuwasilishwa kwake, hivyo watoa huduma watakuwa na kila haja ya kuwahudumia wanachama kwa sababu wanapata fedha zao kwa urahisi zaidi.
Pia amesema,mwezi Oktoba, mwaka huu watafanya kilele cha miaka 20 ya mfuko huo na watazindua programu tumishi ya Taarifa App, hivyo wenye simu za kisasa wataweza kupata taarifa yoyote iwe ni michango,kituo,aina ya dawa kabla ya kwenda kwenye kituo na hivyo kuweza kupunguza malalamiko kwa wanachama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news