Wakulima wa pamba wachekelea, RC Kafulila ataja sababu za faida kubwa

Na Derick Milton, Meatu

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila amesema kuwa wakati msimu wa ununuzi wa pamba mwaka huu ukielekea ukingoni, bei ya zao hilo imepanda kutoka sh.1,050 kwa kilo ambayo ilitangazwa na Serikali kupitia Bodi ya Pamba hadi sh.1,800.

Mwezi Mei 10, 2021 Bodi ya Pamba ilitangaza bei elekezi ya ununuzi wa zao hilo kuwa ni sh.1,050, ambapo mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa kupanda kwa kiwango kikubwa cha bei hiyo sababu kubwa siyo bei kupanda katika soko la Dunia pekee.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Kisesa katika Kijiji cha Mwaukoli, Kafulila amesema kuwa kwa mwaka huu bei imepanda kwa kiwango kikubwa kuliko misimu mingine yote tangu zao hilo limeanza kuzalishwa nchini.

Amesema kuwa, kwa mara ya kwanza wakulima wa zao la pamba mkoa wa Simiyu wameuza pamba yao kwa sh.1,800, huku akieleza kuwa sababu kubwa imetokana na jitihada za Rais Samia Suruhu Hassan kudhibiti mbinu chafu zilizokuwa zikifanywa na wanunuzi wa pamba.

“Bei nzuri ya pamba nchini mwaka huu ni matokeo uongozi thabiti wa Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu, wanaodhani sababu ni ongezeko la bei kwenye soko la Dunia pekee hawako sahihi.

“Watu wanapaswa kufahamu kuwa bei ya soko la Dunia kwa sasa ni dola senti 90, hata mwaka 2018, 2013 bei ilikuwa hiyo hiyo kwenye soko la dunia, lakini kwa bei ya ndani haijawahi kufikia kiwango cha sh.1,800 kwa kilo,” amesema Kafulila.

Amesema kuwa, Rais Samia ameweza kudhibiti mbinu chafu za wanunuzi wa pamba ikiwemo kukomesha umachinga katika zao hilo hali ambayo imechangia bei ya mwaka huu kuvunja rekodi ya bei kwa karibu miaka 20.

Baadhi ya wananchi katika kijiji hicho, wamekiri kuuza pamba yao kwa sh.1,800 kwa kilo huku wakibainisha kuwa haijawahi kutokea bei ya pamba kupamba kwa kiwango hicho.

Wananchi hao wameipongeza Serikali kwa kusimamia suala la bei ya pamba, hali ambayo imesababisha wengi wao kuhamasika kulima zaidi zao hilo katika msimu mpya wa zao hilo mwaka huu.

“Ni kweli mkuu wa mkoa, kama ambavyo ulisema, hapa kwenye kijiji kwetu wengi tumenunua kwa bei hiyo mpya, tunaishukuru sana serikali, tunaiomba bei hii iendelee kuimarika, lakini isishuke kutoka hapa, tunamshukuru Rais Samia amesababisha wengi tuwe na matumaini na pamba,”amesema John Maduhu mwananchi.

Mkoa wa Simiyu katika msimu wa mwaka 2021/22 umepanga kuzalisha tani laki tano, ambapo mkakati huo umelenga kuwawezesha wakulima kupata pembejeo kwa wakati ikiwa pamoja na kufundishwa njia bora za kilimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news