Msemaji Mkuu wa Serikali ajibu hoja na maswali yote yanayokuhusu


Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa

Mahali: Iringa

Salaam.

Ndugu zangu waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa na ndugu Watanzania mnaofuatilia matangazo haya ya moja kwa moja ya taarifa ya Wiki ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Habari za Mchana!.

Ninayo furaha kuwepo hapa Iringa leo, kwa ajili ya jukumu hili la kutoa Taarifa ya Wiki ya Msemaji Mkuu wa Serikali. 
 
Wiki iliyopita hatukuwa na taarifa ya Wiki ya Msemaji Mkuu wa Serikali kwa sababu siku kama ya leo iligongana na matukio mengine ya Kitaifa na busara ikatuongoza tusogeze mbele. 
 
Naomba kuwashukuru wananchi wa Mwanza na viongozi wa Mkoa wa Mwanza wakiongozwa na Mkuu wa mkoa, Bw. Robert Gabriel kwa kutupokea na kutupa ushirikiano mkubwa tulipotoa taarifa ya wiki Jijini Mwanza.

Leo tupo hapa Iringa, hapa pia naomba niwashukuru ndugu zangu waandishi wa habari na pia niwashukuru viongozi wa mkoa wakiongozwa na Bi. Queen Cuthbert Sendiga kwa kunipokea mimi na timu yangu tangu tulipofika na kufanya maandalizi ya kutekeleza jukumu hili.

Kamwene Iringa, Mnoge yunye Vhanamtwa!!!! LEO ZAMU YA IRINGA (nafurahi kwamba sasa Watanzania wameanza kufuatilia kwa ukaribu taarifa hii ya Wiki ya Msemaji Mkuu wa Serikali kwa sababu inatoa nafasi kwao kujua nini kinafanywa na Serikali yao. Wengine wameanza kuita siku hii Msigwa Day. Bila shaka ni kwa sababu nimekuwa nikiwapa taarifa ambazo wanazihitaji.

Ndugu zangu waandishi wa habari na ndugu Watanzania, kama ilivyo kawaida ya taarifa ya Wiki ya Msemaji Mkuu wa Serikali, hii leo nitatoa taarifa ya kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika mkoa huu wa Iringa, nitatoa taarifa ya masuala machache ya Kitaifa, nitatoa majibu ya baadhi ya maswali ambayo niliulizwa mkoani Mwanza majuma mawili yaliyopita, nitapokea na kujibu maswali kutoka kwenu waandishi wa habari wa Iringa na nitapokea na kujibu maswali kutoka kwa wananchi watakaopiga simu kupitia namba 0733111111.

Kabla sijaanza taarifa yangu, naomba ndugu zangu wa Iringa mpokee salamu kutoka kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
 
Anawapongeza kwa kudumisha amani na utulivu, kwa kuendelea kuchapa kazi kwa lengo la kujenga Taifa na kujiongezea kipato na kwa kuendelea kushirikiana na Serikali yenu katika maendeleo. 
 
Mhe. Rais anasema ataendelea kuhakikisha mkoa huu unaongeza kasi ya maendeleo kwa kusimamia utekeleza wa mipango, sera na miradi mbalimbali ya hapa Iringa.

Sasa tuanze taarifa yetu;

MKOA WA IRINGA

Hali ya mkoa ni shwari, na wananchi wa Iringa wanaendelea kuchapa kazi za ujenzi wa Taifa na kujiongezea kipato. Hongera sana wana Iringa.

Mkoa huu ni moja ya mikoa 6 inayotegemewa kwa chakula hapa nchini, mnazalisha mahindi, maharage, mchele, viazi, ngano, mchele, njegere, karanga, kunde, karanga, ndizi ulezi na pia Iringa ni wazalishaji wa mazao ya mifugo hasa maziwa (natambua hapa Iringa kuna mwana Iringa anaitwa ASAS ambaye anazalisha maziwa na kuyafungasha kwa viwango vya kimataifa, amezalisha ajira kwa wananchi), hongera sana Asas na Serikali inatoa wito kwa wawekezaji wengine wa ndani kufanya kama anavyofanya Asas katika maeneo yenu ili Watanzania wanufaike na fursa zinazotokana na uwekezaji wenu.

Takwimu zinaonesha Iringa inazalisha tani 1,173,554 za chakula kwa mwaka ikilinganishwa na mahitaji yake ya tani 703, 206 zinazotosheleza wananchi 1,149,481.

Mfano, Mkoa wa Iringa msimu uliopita umezalisha ziada ya tani 470,348 za mazao ya chakula.

Kutokana na umuhimu huo, Serikali imeendelea kuhakikisha inaleta fedha kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika mkoa huu kupitia bajeti yake. Mwaka huu wa Fedha wa 2021/22 Serikali imepanga kuleta shilingi Bilioni 211.701 hapa Iringa.

Kati ya fedha hizo, shilingi Bilioni 61 zitaelekezwa kwenye maendeleo. Katika mwaka huu wa fedha ambao umeanza Julai 2021 hadi kufikia Oktoba hii Serikali imeshaleta hapa Iringa shilingi Bilioni 21.

Pengine wengi wangependa kujua tangu Mhe. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani na Serikali anayoiongoza ya Awamu ya Sita ameleta nini Iringa. 
 
Sasa naomba niwaambie Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anaupenda sana Mkoa wa Iringa na katika kipindi cha tangu aingie madarakani Serikali imeshaleta hapa Iringa shilingi Bilioni 36 na Milioni 210. Hizi zote zimekuja kuendeleza na kuanzisha miradi mipya ya maendeleo kwa ajili ya wana Iringa.

Pamoja na hilo Serikali imeamua Mkoa huu wa Iringa kuwa kituo (Hub) cha utalii katika Ukanda wa Kusini. Kwa hiyo kutokana na hilo imeamua kuelekeza nguvu nyingi kuimarisha vivutio vya utalii.

Mojawapo ni ujenzi wa uwanja wa ndege. Tunataka ndege zetu za Shirika la Ndege la ATCL na ndege zingine ziwawezeshe Watalii kuja hapa Iringa na watembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, waende Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa, Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, waje wapate historia ya Chifu Mkwawa na pia tuwawezeshe wafanyabiashara na wawekezaji kuja kuwekeza hapa Iringa.

Lakini nyote mtakumbuka kuanzia bajeti hii ya mwaka huu, Serikali ilianzisha tozo maalum kwa ajili ya kuharakisha baadhi ya mambo (Tozo katika miamala ya simu). Na kwa sababu jambo hili limefanyika kwa uwazi ningependa pia wananchi wa Iringa mjue tozo hizi zimewanufaishaje.Mpaka sasa Mkoa huu wa Iringa umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 1 na Milioni 825 za tozo ambazo zimeelekezwa kuharakisha ujenzi wa miradi.Fedha hizi zinakwenda kujenga maboma ya madarasa 26 katika shule za Sekondari, Vituo vya afya 6 vitajengwa katika halmashauri za Mkoa wa Iringa.

Pia kuna fedha ambazo hivi karibuni nchi yetu imezipata kutoka Shirika la fedha Duniani (IMF) Kiasi cha Shilingi Trilioni 1.3 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko 19. Mkoa huu wa Iringa nao umepata mgao wa shilingi Bilioni 8 na Milioni 680. Fedha hizi tutazitumia kujenga Madarasa, ICU, X-ray mashine na pia tutajenga nyumba za watumishi.

LAKINI ukiondoa hiyo ipo miradi mikubwa iliyopokea fedha na ambayo imelenga kutatua kero za wananchi.

Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 Mkoa unatekeleza miradi mikubwa yenye thamani ya jumla ya Shilingi Bilioni 101.7 kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 22.6 zimepokelewa hadi kufikia mwezi Oktoba, 2021.

Baadhi ya miradi inayotekelezwa ni;
Ukarabati wa Uwanja wa Ndege Iringa;
Ujenzi wa barabara za lami
Mradi wa ujenzi Hospitali ya Wilaya ya Kilolo.
Ukarabati wa Mradi wa Maji Isimani – Kilolo.
Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Iringa.
Ujenzi wa Jengo la Utawala la Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya Mufindi.
Ujenzi wa Jengo la Utawala la Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya Iringa.
Ujenzi wa Chuo cha VETA – Pawaga na
Ujenzi wa Daraja la Tosamaganga.

Na hapa labda nifafanue baadhi ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Mamlaka ya Maji Mijini na Vijijini (RUWASA).

Ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Iringa (Nduli) – Kazi inatarajiwa kugharimu shilingi Bilioni 41 na Milioni 126. Fedha hizi zote zimeidhinishwa katika bajeti hii ya mwaka huu.

Hadi sasa ujenzi wa mradi huu umefikia asilimia 30, mkandarasi yupo nyuma ya muda kidogo lakini Serikali inaendelea kumsimamia ili akamilishe mradi kwa wakati. Mradi huu umepangwa kukamilika mwisho mwa mwezi Machi 2022.

Ukarabati wa mradi wa maji wa Isimani – Kilolo. Mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 9 na Milioni 270, mpaka sasa Mkandarasi ameshalipwa shilingi Bilioni 4 na Milioni 200 na kazi inaendelea. Natambua kuwa mradi huu pia upo nyuma ya muda na Serikali inaendelea kutia msukumo ili mkandarasi aukamilishe mwezi Juni 2022 kama ilivyopangwa. Tunatarajia mradi huu uongeze lita Milioni 7 kwa siku kwa wananchi wa Isimani na Kilolo na maji yatayozalishwa yatosheleze mahitaji kwa miaka 15 ijayo.

Kwa upande wa Barabara na Madaraja – kazi zinaendelea kuimarisha barabara za lami na changarawe pamoja na kujenga madaraja katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huu. Mifano michache;

Barabara ya Kidabaga – Bomalang’ombe (km 18.3), ujenzi utagharimu shilingi Bilioni 8 na Milioni 167 hadi kukamilika kwake Januari mwakani 2022. Mpaka sasa kazi hii imefikia asilimia 75.
Barabara ya lami ya Sawala – Mkonge – Iyegeya (km 30.3), ujenzi utagharimu shilingi Bilioni 7 na Milioni 174 hadi kukamilika kwake Juni 2022. Mpaka sasa mradi huu umefikia asilimia 50.
Tunajenga daraja la Tosamaganga. Ujenzi huu utagharimu Shilingi Bilioni 1 na Milioni 398. Daraja hili limejengwa kwa awamu tofauti, awamu ya kwanza na awamu ya pili (tumetumia shilingi Bilioni 1 na Milioni 406) na sasa umeidhinishiwa shilingi Bilioni 1 na Milioni 398 na unatarajiwa kukamilika mwisho wa mwaka huu.
Tumeanza kujenga barabara ya mzunguko ya hapa Iringa (Iringa Bypass) inayoanzia kule Igumbilo kuzunguka mlima hadi kutokea huku jirani na Uwanja wa Ndege wa Nduli Kilometa 7.5. Tayari tumejenga nusu kilometa na kazi inaendelea kidogokidogo. Lengo magari yanayokwenda Dodoma yasilazimike kuingia hapa Mjini na kusababisha msongamano usio wa lazima.
Tumekamilisha usanifu wa barabara ya Iringa – Msende kilometa 105 (kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha) na sasa mazungumzo yanaendelea na wadau wa maendeleo ili tukijaaliwa mwezi Juni mwakani 2022 tutangaze zabuni na kupata mkandarasi atakayejenga barabara hii.

Haya ni baadhi tu ya mambo yanayofanyika hapa Iringa, kazi pia zinafanyika katika sekta ya uzalishaji mazao ya kilimo na mengine ambayo siwezi kuyataja hapa kwa sababu ya muda.

Baada ya kuungalia Mkoa wa Iringa, naomba sasa nitoe taarifa katika maeneo machache ya Kitaifa.

Ziara za Viongozi

Viongozi wetu Wakuu yaani Mhe. Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wameendelea kufanya ziara katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kwa lengo la kutembelea miradi ya maendeleo na kuzungumza na Watanzania

Hivi navyozungumza nanyi Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo Glasgow, Scotland ambako anahudhuria mkutano wa 26 Umoja wa Mataifa (COP26) kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Mkutano huu unawakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali 130 kutoka Duniani kote na wanakutana kujadili athari ambazo dunia inazipata kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ongezeko la joto duniani, hewa ukaa na kuharibika kwa mazingira.

Inawezekana baadhi yetu tusielewe lugha hizi za mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la hewa ukaa, lakini Tanzania nayo inaathirika kutokana na madhara ya mabadiliko ya Tabia nchi.

Miongoni mwa athari tunazozipata ni pamoja na kuongezeka kwa mvua kunakoleta athari katika uzalishaji, mazingira na makazi, kuongezeka kwa kina cha maji katika Maziwa na bahari (wote tumeona kilichotokea ziwa Victoria mwaka jana na kuzama kwa baadhi ya visiwa vyetu katika bahari ya Hindi na maziwa), kuyeyuka kwa theruji katika Mlima wetu Kilimanjaro na mengine mengi.

Sasa madhara ya athari hizi ni ya kidunia, huwezi ukajifungia nyumbani kwako na kupanga mipango ya pekee yako kukabiliana nazo, zinahitajika juhudi za pamoja dunia, ndio maana Wakubwa wa Dunia nzima wanakutana huko Glasgow, Scotland na Mhe. Rais wetu ameona aende huko akatupiganie Watanzania.

Tayari kulikuwa na mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo nchi zimeridhia. Tanzania nasi tulisharidhia Mkataba wa Kyoto (mwaka 2002) ambao pamoja na mambo mengine unaagiza nchi 37 zinazozalisha hewa ukaa nyingi kupunguza uchafuzi huo kwa asilimia 5, na Mkataba wa Paris ambao tumeridhia mwaka 2018 unaotaka nchi zenyewe kuchukua hatua za kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Ni katika mikutano huu, ndiko wakubwa hawa ambao nchi zao zina maendeleo makubwa ya viwanda na ndio wanaozalisha hewa nyingi walikubaliana nchi hizo zichangie Dola za Marekani Bilioni 100 kwa ajili ya kuwezesha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Fedha hizi ni kwa ajili ya kupelekwa katika nchi mbalimbali kupitia taasisi zinafanya jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabia Nchi. Moja ya Taasisi hizo ni GCF (Global Climate Fund) ambao wote mtakumbuka hivi karibuni imetoa fedha kwa benki ya CRDB kiasi cha Dola za Marekani Milioni 100 (sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 230) kwa ajili ya kuwakopesha Watanzania watakafanya shughuli za kilimo zinazosaidia katika utunzaji wa mazingira.

Benki ya CRDB nayo imeongeza kiwango kama hicho hicho kuongeza uwigo wa kutoa mikopo hiyo na sasa kuna kiasi cha takribani shilingi Bilioni 460 ambazo zitawanufaisha wakulima takribani Milioni 6 hapa nchini.

Kwa hiyo kupitia dirisha hili kuanzia mapema mwakani wakulima wataweza kupata mikopo itakayowawezesha kuongeza tija katika uzalishaji kwa kulima eneo dogo na kupata mazao mengi, kutumia teknolojia za kisasa katika kilimo zinazoepusha uharibifu wa ardhi, matumizi sahihi ya viuatilifu, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kurutubisha ardhi, kuongeza kipato cha watu nakadhalika.

Sasa madirisha kama haya yapo mengi, na ni katika Mkutano huu ambapo Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anakwenda kukutana na Mwenyekiti wa taasisi hii ya GCF na taasisi zingine zinazotoa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

LAKINI katika ziara hii pia Mhe. Rais Samia atakuwa na mikutano mingine na atakutana na viongozi mbalimbali wakiwemo Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Scotland ambao wanataka kuja kuwekeza hapa nchini kwetu na atakutana na Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Boris Johnson ambaye watazungumzia uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Uingereza.

Pia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amealikwa kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa nchi 30 tu, kati ya wote 130 wanaohudhuria Mkutano huu na atahutubia.

Kadhalika Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan atahudhuria Mkutano wa viongozi wanawake (Women Leadership) ambao umeitishwa na First Minister wa Scotland (ni kama Waziri Mkuu wa Scotland) na huko watazungumzia ushiriki wa wanawake katika masuala ya mazingira na Mhe. Rais anatarajiwa kuhutubia katika Mkutano huu.

Kwa upande wa Waziri Mkuu, leo yupo Dodoma ambako anaweka jiwe la msingi katika sehemu ya mradi wa ujenzi wa nyumba 1,000 za kuishi watu katika maeneo ya Chamwino na Iyumbu. Nyumba hizi zinajengwa katika juhudi za Serikali kukabiliana na changamoto ya uhaba wa makazi katika Jiji la Dodoma hasa baada ya Serikali kuhamia Dodoma.

Serikali iliamua kutoa mkopo wa shilingi Bilioni 20 kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ajili ya kuutumia kama mfuko maalum wa mzunguko (Revolving Fund) kwa ajili ya kujenga nyumba na kuziuza ama kupangisha.

Kwa hiyo katika kutekeleza mradi huu, ujenzi unafanyika kwa awamu tatu, awamu ya kwanza ujenzi wa nyumba 400 (100 zinajengwa Chamwino na 300 zinajengwa Iyumbu) Awamu ya pili zitajengwa nyumba 375 na awamu ya tatu zitajengwa nyumba 225.

Mhe. Waziri Mkuu ametoa wito kwa taasisi mbalimbali za kifedha kuunga mkono juhudi hizi za kutatua changamoto ya makazi kwa Watanzania wote sio tu kwa Jiji la Dodoma kwa kuwatumia NHC ama Watumishi Housing kujenga nyumba za gharama nafuu ambazo Watanzania watamudu kuzinunua.

Na hapa Iringa, Mhe. Waziri Mkuu anatarajiwa kufanya ziara tarehe 13 Novemba, 2021 ambapo atafungua kongamano kuhusu mazao ya misitu litakalofanyika Mafinga na kujumuisha wageni wa ndani na nje ya nchi.

Uwekezaji wa Serikali katika mashirika ya umma.

Kama wote mnavyojua, Serikali inamiliki mali katika kupitia mashirika na taasisi mbalimbali ama kwa umiliki wa asilimia 100 ama kwa ushirika na wabia. Serikali inasimamia mali hizi kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Hadi Juni 30, 2021 Ofisi ya Msajili wa Hazina ilikuwa inasimamia mashirika ya umma 287 yanayojumuisha kampuni za biashara, taasisi 40 zinazomilikiwa na Serikali na kampuni za nje ya nchi kama 10 hivi.

Kwa ujumla hali ya uwekezaji wa Serikali katika mashirika haya ni nzuri na mali ya Watanzania ipo salama na inaendelea kukuongezeka thamani kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji na faida inayotokana na gawio na makusanyo ya mapato yasiyo ya kikodi.

Takwimu za Ofisi ya Msajili wa Hazina zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita uwekezaji katika mashirika hayo umeongeza thamani ya mali ya Serikali kutoka Shilingi Trilioni 64.45 hadi kufikia shilingi Trilioni 67.06 (Hili ni ongezeka la asilimia 4). Ongezeko hili kwa sehemu kubwa limetokana na kutekelezwa kwa sheria ya madini namba 7 ya mwaka 2017 kifungu cha 10 na kanuni za madini za mwaka 2020 ambazo zimetoa nafasi kwa Serikali kumiliki asilimia 16 ya hisa katika migodi ya madini. Tayari tuna umiliki huo katika kampuni za North Mara Gold Mine Ltd, Bulyanhulu Gold Mine ltd, Pangea Minerals Ltd, Twiga Minerals.

Sababu nyingine ni kuongezeka kwa ziada inayotokana na kurejea kwa uthaminishaji wa mali pamoja na kukua kwa malimbikizo ya faida na ziada ya taasisi na amshirika ya umma pamoja na umiliki wa hisa chache.

LAKINI PIA Ofisi ya Msajili wa Hazina pia hukusanya mapato yasiyo ya kikodi, ambayo hukusanywa kutokana na michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi ya taasisi na mashirika (kwa mujibu wa sheria ya fedha), kuna mawasilisho ya asilimia 75 ya mapato yatokanayo na mtambo wa uhakiki wa mawasiliano ya simu (TTMS) pamoja na asilimia 70 ya mapato ya ziada inayozalishwa na taasisi na mashirika ya umma.

Sasa mapato haya pamoja na mengine yasiyo ya kodi, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea kuimarisha ukusanyaji ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita yamepanda kutoka shilingi Bilioni 425.47 za mwaka 2015/2016 hadi kuwa zaidi ya shilingi Bilioni 637.66. (Kuna baadhi ya miaka yalifika mpaka zaidi ya shilingi Bilioni 885.64.)

Hata kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita kuna dalili njema kabisa za usimamizi mali hizi za Serikali kwani takwimu zinaonesha kati ya Aprili na Septemba mwaka huu 2021 shilingi Bilioni 299.14 zimekusanywa ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hiki ambapo makusanyo hayo yalikuwa shilingi Bilioni 227.32.

Inawezakana kuna baadhi yetu hatuelewi kuhusu umiliki wa Serikali katika kampuni hizi na hapa nitatoa mifano michache
Kiwanda cha Sukari Kilombero, Serikali inamiliki hisa kwa asilimia 25. Na hivi tunavyozungumza Serikali kwa kushirikiana na mbia wake tunafanya upanuzi wa kiwanda hiki kwa kuwekeza shilingi Bilioni 571.6 ili kupanua uzalishaji kutoka tani 127,000 kwa mwaka hadi kufikia tani 271,000 katika kipindi cha miaka 3 ijayo.

Hapohapo Kilombero, Serikali imeamua kununua shamba kuzalisha miwa la Mngeta kwa asilimia 100. Na hivi navyozungumza shamba hili limekabidhiwa kwa Shirika la Suma JKT kwa ajili ya kuendeleza uzalishaji na kuwasaidia wananchi.

Kiwanda cha kuzalisha dawa cha Keko (Keko Pharmaceuticals Ltd). Serikali ilikuwa inamiliki hisa kwa asilimia 40, lakini kutokana na kusuasua katika uzalishaji mwaka 2019 iliamua kuongeza umiliki wake hadi kufikia asilimia 70.

Uwekezaji mkubwa umefanyika katika kiwanda hiki kwa mwaka mmoja tu, ambacho kilikuwa kinazalisha dawa aina 1 na sasa kinazalisha dawa aina 10. Uwezo wake wa kuzalisha vidonge umeongezeka kutoka vidonge 1,500,000 kwa siku hadi kufikia vidonge 6,000,000 kwa siku.

Sasa hivi Keko Pharmaceuticals Ltd inazalisha vidonge mbalimbali mbali kama vile Paracetamol, Metronidazole, Erthromycin, Ampicilin, Pen V, Amoxicilin, Co-trimoxazole, Griseofulvin, Ciprofloxacin na Diclofenac.

Uwekezaji huu pamoja na kutusaidia kuongeza uhakika wa upatikanaji wa dawa na kupunguza gharama za dawa pia kwa mwaka mmoja tu ambao kiwanda hiki kimefanya uzalishaji baada ya uwekezaji wa shilingi Bilioni 7.5 kimezalisha faida ya shilingi Bilioni 1.4.

Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru

Kama nyote mnavyojua mwaka huu nchi yetu inatimiza miaka 60 tangu ipate Uhuru wake. Tutatimiza miaka 60 tarehe 9 Desemba, 2021.

Hili sio tukio dogo na Serikali imeamua kutoa umuhimu wa kipekee kwa tukio hili mwaka huu. Tunataka Watanzania wapate nafasi ya kutosha ya kujua juhudi mbalimbali zilizofanywa na nchi yetu kwa miaka 60, changamoto zilizojitokeza na jinsi tulivyokabiliana nazo mpaka leo.

Kutokana na hilo, kuanzia kesho shughuli za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru zitaanza. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenyeulemavu Mhe. Jenister Mhagama atakuwa na mkutano na waandishi wa habari Jijini Dodoma katika ukumbi wa PSSSF kuelezea namna shughuli za kuelekea maadhimisho haya zitakavyofanyika.

Naomba kutoa wito kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari kufuatilia matukio haya yote, kurusha taarifa mbalimbali zitakazohusu maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wetu.

Natambua kuwa vyombo vya habari vingi vimeanza kutangaza masuala mbalimbali yanayohusu miaka 60 ya Uhuru, naomba na vyombo vingine vijitokeze kufanya hivyo kwa sababu hili ni jambo la kizalendo kwa ajili ya nchi yetu. Huu ni wakati wa kuionesha Dunia kwamba sisi Tanzania ni Taifa imara, ni Taifa lililofanya udhubutu na likaweza kwa mambo mengi na zaidi ya hapo ni Taifa ambalo pamoja na kujipigania lenyewe limetoa mchango mkubwa Barani Afrika na kwingineko Dunia katika kupigania ukombozi, uhuru na fikra.

Maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Ndugu zangu Waandishi wa Habari na Watanzania, Serikali inatambua kuwa kuwa dunia ipo katika mapinduzi ya 4 ya viwanda, na kama ilivyo kauli mbiu ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa “Tanzania lazima iende pamoja na Dunia” Nchi yetu imeamua kuchukua hatua madhubuti ya kuwekeza katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kujenga mazingira ya shughuli na huduma mbalimbali kutolewa kidigitali.

Moja ya hatua ambazo zimechukuwa ni kuwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kuiwezesha kwa rasilimali nyingi ili kufanikisha dhamira hii.

Katika mwaka huu wa Fedha Serikali iliamua kuongeza bajeti ya maendeleo ya Wizara hii kutoka shilingi Bilioni 11 za mwaka jana 2020/21 hadi shilingi Bilioni 241.

Moja ya maeneo ambayo fedha hizo zimeelekezwa ni katika kupanua Mkongo wa Taifa na kuongeza uwezo wake. Kwenye Mkongo wa Taifa ambako Serikali imewekeza zaidi ya shilingi Bilioni 677. Sasa kwa miaka yote Serikali imekuwa ikitoa shilingi Bilioni 8 kwa mwaka kwa ajili ya kupanua Mkongo wa Taifa lakini mwaka huu imeamua kuongeza fedha hadi shilingi Bilioni 170.

Lengo ni kuongeza kasi ya usambazaji wa mkongo na kuongeza uwezo wake. Tangu mwaka 2009 tulipoanza kusambaza Mkongo wa Taifa tumejenga kilometa 8,319 (kwa miaka 9), LAKINI kwa bajeti tuliyoitenga mwaka huu tunakwenda kujenga kilometa 4,442 kwa mwaka mmoja. Tunakwenda kuongeza uwezo wa mkongo mara nne ya uwezo uliopo sasa yaani kutoka 200G hadi 800G, hii itawezesha watoa huduma yaani hizi kampuni za simu kuwasambazia huduma Watanzania wengi zaidi ya huduma zenye kasi zaidi.

Lakini pia tunapanua uwezo wa kuhudumia nchi majirani ambazo zinatumia ama zinaweza kutumia Mkongo wetu, tumeshafikisha huduma Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Msumbiji na sasa tunajiandaa kwenda Congo DRC.

Kwa hiyo uwekezaji huu licha ya kwamba unatuimarisha kutumia huduma za kidijitali lakini pia ni biashara kubwa ambayo nchi yetu inaipata. Siku moja nitakuja kuwajulisha tunavuna mapesa kiasi gani kutokana na uwekezaji huu mkubwa.

Lakini tukirudi kwenye dhamira yetu ya kujiimarisha katika TEHAMA kama wote mtakumbuka Wiki iliyopita, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliadhimisha kongamano la 5 la Taifa la TEHAMA lililofanyika katika Jiji la Arusha.

Kwenye kongamano hili Wataalamu wa TEHAMA takribani 845 walikutana na kampuni 27 zilifanya maonesho. Lengo likiwa ni kujadili maendeleo ya TEHAMA katika nchi yetu, uwekezaji, usalama wa mtandao, kuangalia ajira kwa vijana na mengine.

Kongamano hili limefanyika kwa mafanikio makubwa na Wataalamu hawa wameweka maazimio kadhaa yakiwemo kuweka mazingira rafiki ya kisera, sheria, tozo na kodi kwa vijana wanaojiajiri kupitia TEHAMA wakiwemo wale wanaotengeneza mifumo mbalimbali ya biashara na huduma, kushirikisha wadau, kuimarisha mifumo ya ufundishaji TEHAMA, kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za TEHAMA, kuvutia wawekezaji katika sekta hii na kujenga mazingira ya kuvutia ukuaji wa biashara mtandao.

Sasa Serikali inafanya nini ?

Inahamasisha wawekezaji mbalimbali kuwekeza katika viwanda vya kuzalisha bidhaa za TEHAMA kama vile simu, vishikwambi, computer na vinginevyo
Imeondoa kodi kwa bidhaa hizo ili Watanzania wazipate kwa gharama nafuu.
 
Kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Serikali imetenga takribani shilingi Bilioni 19 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Kituo cha Taaluma ya TEHAMA (ICT Professional Center). Kituo hiki kitaanza kujengwa mwaka huu pale Njedengwa Dodoma na matarajio yetu kikamilike Juni mwaka 2023 au kabla ya hapo.

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa Serikali itajenga chuo kikubwa cha TEHAMA hapa nchini. Chuo hiki kitakuwa kikubwa kuliko vyote katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Kwa haya yote lengo letu ni kuhakikisha Tanzania inapika vijana kubobea katika masuala ya Tehama.

Mradi wa Kuendeleza Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (Resilient Natural Resources Management for Tourism and Growth – REGROW).

Ndugu zangu Waandishi wa Habari na Watanzania, Sote tunatambua kuwa moja ya maeneo yanayochangia fedha nyingi katika Pato la Taifa letu ni Utalii. Utalii unachangia kwa asilimia 17.2 katika pato la Taifa, unaajiri watu Milioni 1.6 na unachangia fedha za kigeni kwa asilimia 25.

Tanzania ni nchi ya pili Duniani kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, ikitanguliwa na Brazil. Hata hivyo vivutio vyetu vimekuwa havitunufaishi kwa kiwango kichastahili.

Yapo maeneo mengi ambayo kuna vivutio vingi vya utalii lakini havitunuishio kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutufunguliwa kwa miundombinu ya kuvifikia na kutokuwepo kwa huduma kwa Watalii.

Eneo la Kusini mwa Tanzania ni mojawapo ya maeneo ambayo yanahitaji kufunguliwa kwa utalii. Ni kutokana na sababu hii Serikali imeamua kuja na mradi huu uitwao REGROW.

Kupitia mradi huu Serikali imeamua kuimarisha miundombinu na huduma za utalii katika hifadhi za Taifa za Ruaha, Nyerere, Mikumi na Udzungwa ambayo yana kilometa za mraba 56,339. Utagusa mikoa ya Iringa, Pwani, Mbeya, Dodoma, Njombe na Morogoro. Kuna vijiji 61 vitakavyonufaika katika Wilaya za Kilolo, Iringa Vijijini, Rufiji, Kisarawe, Chamwino, Morogoro Vijijini, Mbarali, Kilombero, Kilosa, Mvomero.

Fedha zilizotengwa ni Shilingi Bilioni 345 kwa ajili ya;
Kujenga miundombinu ya barabara kilometa 2,000, majengo zaidi ya 80, viwanja vya ndege vya hifadhini 14. Usanifu wa miradi hii unaendelea.
Kununua magari 44 kwa ajili ya doria, usimamizi wa mradi, huduma za utalii nk. Magari haya yameshanunuliwa.
Mitambo 16 ya kutengenezea miundombinu ndani ya hifadhi imeshanunuliwa na imeanza kazi.
Kuna mkandarasi yupo kazini katika skimu ya Madibila anaendelea na kazi ya kuboresha miundombinu ya mradi huu.
Mchakato wa kuanza ujenzi wa kituo cha pamoja cha masuala ya utalii (One Stop Center) umeanza. Jengo hili litajengwa pale Kihesa Kilolo kuanzia Juni mwakani 2022 kwa gharama ya shilingi Bilioni 16 na Milioni 590.

Lengo hiki kiwe kituo cha kisasa ambacho kitahudumia ukanda wote huu wa Kusini. Matarajio yetu hatua hizi zitasaidia kuongeza idadi ya watalii na kuongeza pato la Taifa la nchi yetu.

Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19.

Nyote mnafahamu kwamba nchi yetu inatakiwa itekeleze miradi mbalimbali yenye thamani ya shilingi Trilioni 1.3 katika kipindi cha miezi 9 tu.

Naomba kuwajulisha kuwa utekelezaji unaendelea, fedha zimeshagawanywa kwenda katika sekta mbalimbali za utekelezaji ambako wananchi katika maeneo husika wanatumia utaratibu Force Account yaani kupata mkandarasi mmoja kwa haraka atakayetekeleza mradi badala ya utaratibu wa siku zote wa kutangaza zabuni na ikapita mchakato wote.

Kwa wiki nzima iliyopita, mmeona jinsi Mawaziri walivyotoa taarifa za namna mgawanyo wa fedha hizi ulivyofanyika na labda kwa kujuisha ni kwamba Serikali imepeleka fedha hizi katika sekta mbalimbali kama ifuatavyo;
Tumepeleka shilingi Bilioni 466.9 katika sekta ya afya
Shilingi Bilioni 367.6 katika sekta ya elimu
Shilingi Bilioni 302.7 katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Shilingi Bilioni 231 kwa ajili ya Zanzibar (zimeshapelekwa)
Shilingi Bilioni 139 katika sekta ya maji
Shilingi Bilioni 90.2 kwa ajili ya sekta ya utalii
Shilingi Bilioni 64.9 katika Wizara ya Elimu
Shilingi Bilioni 5.5 katika Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
Shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya kuwawezesha vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya uratibu na utawala katika ngazi za Wizara, Mikoa na Serikali za Mitaa.

Hivi ninavyozungumza nanyi kazi za ujenzi na michakato ya ununuzi wa vitu mbalimbali imeanza. Kwenye maeneo yanayohitaji ujenzi, wajenzi wameanza kupelekwa katika maeneo ya miradi baada ya kukamilisha mazungumzo ya kuanza kwa ujenzi.

Mfano, fedha za ujenzi wa madarasa 15,000 zote zimeshapelekwa kwenye akaunti za shule husika (kiasi cha Shilingi Bilioni 304) na tayari ujenzi katika baadhi ya maeneo umeanza.

Serikali inaendelea kuwakumbusha viongozi katika ngazi mbalimbali kusimamia utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa kwa fedha hizi, na wananchi kutosita kuhoji utekelezaji wake na kutoa taarifa kwa viongozi pale watakapobaini vitendo vya kuhujumu miradi hii.

MUHIMU; Watanzania tuna kila sababu ya kumpongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Mhe. Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa juhudi kubwa walizozifanya kupata fedha hizi.

Nataka kuwaambia ndugu zangu haikuwa Rais, wamepambana sana hawa viongozi hadi wamefanikiwa, wamezungumza na wakubwa hawa wamepeleka maandiko, wamekwenda kuyatetea mpaka tumefanikiwa.

Mimi nipo huku ndani naona, kama wangekuwa na mioyo myepesi tusingepata. Na Fedha hizi zinakwenda kuleta mageuzi makubwa sana kwenye huduma zetu za kijamii na katika uchumi.

Fedha za msaada

Wiki hii nchi yetu imepata msaada wa shilingi Bilioni 119 kutoka Serikali ya Ujerumani.

Fedha hizi zitaelekezwa katika masuala ya uhifadhi, tutazitumia kununua magari kwa ajili ya kuwezesha shughuli za kukabiliana na ujangili, kuweka mifumo ya kidigitali ya kufuatilia magari yanaingia hifadhini pamoja wanyamapori wakubwa hasa walio hatarini kutoweka, kuwezesha shughuli za utunzaji wa mazingira na kuboresha miundombinu ndani ya hifadhi ikiwemo ujenzi wa mabwawa ya maji ya wanyama pamoja na kujenga viwanja vya ndege vidogovidogo.

Halikadhalika zitatumika kuimarisha huduma za afya hifadhini ikiwemo vituo vya upimaji wa Uviko-19 na huduma nyingine.

Mapambano ya Uviko-19

Juhudi za kupambana na Uviko-19 zinaendelea. Wataalamu wetu wanaendelea kutoa elimu kupitia majukwaa mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, kwenye maeneo yenye watu wengi n.k

Serikali inaendelea kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari zote ambazo Wataalamu wanatuelekeza yaani kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, kuepuka misongamano isiyo ya lazima, kuvaa barakoa, kula chakula cha lishe, kufanya mazoezi na kupokea chanjo, kwa kuwa Uviko-19 au ugonjwa wa Korona bado upo, Watanzania wenzetu bado wanapata maambukizi, wale ambao hawajachanjwa ndio wanaopatwa na ugonjwa mkali na wengi wao ndio wanaopoteza maisha.

Utoaji wa chanjo unaendela nchi nzima, awali Serikali ilileta dozi 1,058,400 aina ya JJ ama Jansen ambazo zimekwisha, na sasa Watanzania wanaendelea kuchoma dozi aina ya Sinopharm kutoka nchini China ambazo mtu anapaswa kuchoma dozi mbili. Chanjo aina ya Sinopharm zimekuja Dozi 1,065,600.

Kesho tutapokea dozi nyingine 500,000 aina ya Sinopharm kutoka China, kuna zile dozi nyingine 500,000 za aina ya Pfizer ambazo tuliahidi zingefika mwisho wa mwezi huu Oktoba, kulitokea changamoto kidogo ya usafiri lakini wakati wowote hivi sasa zitaingia nchini.

Serikali inaendela kufanya juhudi nyingine za kupata chanjo zingine ili Watanzania wengi zaidi wachome chanjo hizi na kujihakikishia zaidi usalama dhidi ya Uviko-19.

Chanjo hizi zote zinaletwa nchini kwetu chini ya mpango wa Shirika la Afya Dunia uitwao Covax Facility ambao unatoa bure chanjo kwa idadi ya hadi asilimia 20 ya wananchi wa nchi husika, na hivyo hapa Tanzania tunatarajia kupata dozi 11,800,000 kupitia dirisha hilo/mpango huo.

Hali ya Uchanjaji inakwenda vizuri, baada ya kuisha dozi za chanjo aina ya JJ au Jansen sasa hivi uchanjaji unaendelea kwa chanjo aina ya Sinopharm, takwimu za hadi Juzi tumeshatumia asilimia 5.5 ya chanjo yaani watu 58,703 wamechanjwa tangu uchanjaji wa chanjo hizi ulipoanza tarehe 12 Oktoba, 2021.

Mikoa mitano inayofanya vizuri zaidi ni Mtwara, Mbeya, Dodoma, Kagera na Ruvuma. Na inafuatiwa na Mikoa mingine 5 ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Songwe na Pwani.

Serikali inatoa wito kwa wananchi ambao hawajapata chanjo kujitokeza kupata chanjo hizi kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya virus vya korona. Viongozi katika mikoa ambayo uchanjaji hauna kasi ya kutoshwa wameagizwa kuongeza kasi ya uhamasishaji wananchi na kuhakikisha chanjo zinapelekwa kwa wananchi katika maeneo walipo.

Lakini pia wananchi mnaopata chanjo aina ya Sinopharm na mtakaopata chanjo aina ya Pfizer mnakumbushwa kuhakikisha mnarejea kupokea dozi ya pili baada ya wiki tatu kama inavyoelekezwa na wataalamu. Na kwa kutumia cheti ulichonacho kama haupo pale ulipochanjwa unaweza kwenda kwenye kituo kingine chochote ukapate dozi ya pili ili ukamilishe kinga yako.

Majibu ya maswali ya Wananchi na Waandishi wa Habari wa Mwanza.

Sasa Ndugu zangu Waandishi wa Habari wa hapa Iringa na Ndugu Watanzania, kama nilivyosema majuma mawili yaliyopita nilikuwa Mkoani Mwanza ambako pamoja na kutoa taarifa ya Wiki nilipokea maswali kutoka kwa Wananchi na Waandishi wa Habari. Yapo niliyoyajibu palepale Mwanza nay apo ambayo nitayajibu leo kwa sababu yalihitaji kufanyiwa kazi zaidi.

Kuna Mwandishi wa Habari aliuliza kuhusu changamoto ya miundombinu ya barabara katika Jiji la mwanza inayosababisha msongamano wa magari hasa katika barabara ya nyerere na kenyata.

Ni kweli Jiji la Mwanza ambalo ni Jiji la pili kwa ukubwa hapa nchini likitanguliwa na Dar es Salaam linakabiliwa na changamoto ya Msongamano mkubwa wa magari.

Kwa kutambua changamoto hiyo Serikali inachakua hatua zifuatazo;

Barabara ya Mwanza – Usagara, njia 4 inafanyiwa upembuzi yakinifu na kazi hiyo itakamilika kufikia Mei 2022 ikiwa ni maandalizi ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Upanuzi wa barabara hiyo utaondoa msongamano katika barabara ya Kenyatta.

Barabara ya Mwanza – Nyanguge, njia 4 inafanyiwa upembuzi yakinifu na kazi hiyo itakamilika kufikia Disemba 2021. Upanuzi wa barabara hii utapunguza msongamano katika barabara ya Nyerere.

Ujenzi wa Barabara ya Buhongwa – Kishiri kwa kiwango cha Lami inafanyiwa usanifu na utakapokamilika kazi ya ujenzi itaanza.

Kuna Mwandishi wa Habari ambaye alitaka kujua kuhusu kikokotoo, wafanyakazi hawajui hatima yao.

Majibu ni kwamba; Serikali inaendelea kutafakari suala hili lakini kwa sasa malipo ya pensheni kwa Wastaafu yanaendelea kufanywa kwa utaratibu ule ule wa zamani kama ambavyo kila mfuko wa hifadhi ya Jamii ulivyokuwa unawahudumia wanachama wake. Kazi inayoendelea Serikali ikikamilika kwa kushirikiana na vyama vya wafanyakazi mtajulishwa.

Kulikuwa na swali la Mwandishi wa Habari wa Mwanza kuhusu msongamano wa magari yanayoingia bandari ya Mwanza Kaskazini pale Jijini Mwanza.

Majibu ni kuwa; Hakuna njia ya moja kwa moja ya kuingia bandarini (North Mwanza) njia kuu inayotegemewa ni kupita katikati ya Kituo cha Polisi.

Na eneo hili limewekewa zuio kwa sababu za kiusalama, maana ikiruhusiwa maana yake tukiweka kituo cha polisi katika hatari ya uvamizi nan yote mnajua vituo vya Polisi vina silaha zinazotumika kuwalinda raia na mali zao. Wataalamu wa usalama wameona wakiruhusu njia hii kutumika kama ilivyokuwa zamani upo uwezekano wa watu wenye nia ovu kuvamia kituo.

Kulikuwa na swali la Mwandishi wa Habari wa Mwanza aliyetaka Serikali iseme kweli kuhusu kadi za NIDA (Vitambulisho vya Taifa), kwanini kuna ucheleweshaji wa kupata?

Majibu ni kuwa; Serikali haifichi chochote kuhusu utoaji wa vitambulisho vya NIDA.

Mpaka mwanzoni mwa Mwezi uliopita NIDA ilikuwa imesajili jumla ya watu 22,622,358 ambapo kati yake watu 19,036,378 walikuwa wamepatiwa namba za utambulisho.

NIDA ilikuwa tayari imeshasambaza vitambulisho 8,567,407 katika Wilaya 117. Kati yake kuna vitambulisho 1,322,649 vilikuwa vimepelekwa katika vituo lakini wahusika walikuwa hawajafika kuchukua vitambulisho vyao.

Kwa hiyo Serikali inatoa wito kwa Watanzania wote ambao wamesajiliwa na hawapata vitambulisho kwenda kwenye vituo walikoandikishwa wakafuatilie vitambulisho vyao na kama kuna tatizo walieleze ili lifanyiwe kazi. Kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya watu ambao taarifa zao zimeonekana kuwa na dosari na hivyo NIDA haiwezi kuendelea kuchapisha vitambulisho vya watu hao mpaka taarifa zao ziwekwe sawa.

HATA HIVYO; Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaendelea na uzalishaji na ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa mzunguko, utaratibu ulioanza Januari, 2021.

Kila mzunguko NIDA inazalisha asilimia 25-30 ya maombi ya Wilaya husika ili kuwa na usawa wa uzalishaji na ugawaji wa Vitambulisho nchi nzima.

Mpaka sasa jumla ya Wilaya 133 zimezalishiwa Vitambulisho kwa mzunguko wa kwanza.

Uzalishaji unaendelea na vitambulisho vinazalishwa na kupelekwa kwa Watendaji wa Mitaa na Vijiji.

Kwa upande wa Zanzibar uzalishaji na ugawaji umefanyika kwa zaidi ya asilimia 90 katika Wilaya zote 11 na uzalishaji unaendelea.

Serikali inatoa wito kwa waombaji wote wenye sifa za kupata Vitambulisho vya Taifa na ambao hawajapata Vitambulisho kuwa wavumilivu, kwa kuwa watapatiwa vitambulisho kuendana na uhakiki unavyofanyika na ratiba ya uzalishaji na usambazaji iliyowekwa

Kulikuwa na Swali la Mwandishi wa Habari wa Mwanza kwamba wafanyabiashara wadogo wa Mwanza wameondolewa katika maeneo waliyopangiwa na hawana mahali pengine pa kwenda.

Majibu ni kuwa; Ni kweli wafanyabiashara wadogo (Wamachinga) waliokuwa maeneo ya katikati ya Jiji la Mwanza hasa eneo la Makoroboi wameondolewa LAKINI sio kweli kwamba hawajapangiwa maeneo ya kwenda kufanya biashara.

Wamachinga walioondolewa wamepangiwa maeneo ya Mchafukoga ambapo panaweza kuwaweka wafanyabiashara zaidi ya 3,000. Wengine wamepangiwa Buhongwa (zaidi 3,000), Tambukaleli (zaidi ya 2,000), Soko la Igoma (takribani 1,000), eneo la Ukwaju-Igoma (nafasi ya wamachinga zaidi ya 6,000), eneo la Soko la Mbao Igoma (nafasi ya Wamachinga zaidi ya 500), eneo la Nyegezi karibu na Stendi ya mabasi inayojengwa (kuna nafasi ya wamachinga kama 1,000).

Haya maeneo yote yamewekewa huduma muhimu kama vile choo, maji, umeme. Katika eneo la Ukwaju hivi navyozungumza viongozi wa Mkoa wa Mwanza wapo eneo la tukio wanahakikisha huduma hizi muhimu zinawekwa ili wamachinga wakianza kupatumia wapate huduma.

Hata hivyo, Mwanza kumejitokeza changamoto, kwamba sasa hata watu ambao hawakuwa Wamachinga lakini kwa sababu wameona kuna ugawaji wa maeneo ya Machinga wamejitokeza kuomba kupatiwa nafasi. Jiji la Mwanza linakadiriwa kuwa na Wamachinga 10,000 lakini nafasi zilizopo ni zaidi ya idadi hiyo.

Kuna mwananchi aliuliza swali kuwa Watumishi wa umma wamepandishwa vyeo na wana malimbikizo wanadai kwa miaka mitatu sasa hawajalipwa. Hayo malimbikizo yatalipwa lini?

Majibu ni kuwa; Utaratibu wa kushughulikia madai ya malimbikizo ya mishahara huanzia kwa mwajiri ambapo mtumishi mwenye madai ya malimbikizo hujaza fomu ya madai ya malimbikizo na kuyawasilisha kwa mwajiri ambako hushughulikiwa na kuikamilisha ipasavyo na kuiwasilisha Ofisi ya Rais -UTUMISHI.

Hata hivyo, kuanzia tarehe 24 Mei, 2021 umeanzishwa utaratibu ambapo fomu za madai ya malimbikizo ya mishahara zinaingizwa na waajiri kupitia Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS).

Kwa sasa uhakiki wa madai ya Watumishi 24,210 yenye thamani ya shilingi bilioni 86.5 yaliyowasilishwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI unaendelea kufanyiwa kazi na ukikamilika watalipwa.

Post a Comment

0 Comments