NGOs zinazofanya kazi za mifukoni na kwenye simu zamchefua RC Kunenge

NA ROTARY HAULE

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amezipiga marufuku taasisi za kiraia (NGOs) zinazofanya kazi kwa maslahi yao binafsi na kutaka zibadilike haraka iwezekanavyo kinyume na hapo zitachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Aidha, Kunenge amesema kuwa kwa sasa hategemei kuwepo kwa asasi ambazo zinaendesha shughuli zake mifukoni,na kwenye simu na kwamba lazima walengwa wanufaike na asasi hizo.
Kunenge ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua kikao kazi cha mashirika yasiyo ya kiserikali kilichofanyika Mjini Kibaha kwa kuwashirikisha viongozi wa asasi hizo,Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Mwanasha Tumbo pamoja na sekretarieti ya mkoa huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Mwanasha Tumbo, akizungumza katika kikao kazi cha mashirika yasiyo ya Kiserikali kilichofanyika Oktoba 28 Mjini Kibaha chini ya maandalizi ya ofisi ya mkuu wa mkoa huo. (NA ROTARY HAULE).

Katika kikao hicho, Kunenge amesema kuwa, yapo mashirika mengine ambayo yanachafua wenzao kwa kuwa yanafanya kazi kinyume na utaratibu uliopangwa na hivyo kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Amesema kuwa,kazi ya mashirika hayo ni kuhudumia jamii hususani katika kutatua kero zinazowakabili kama ambavyo kanuni zinaeleza wakati wa usajili na badala yake ziache kufanya kazi kwa maslahi ya matumbo yao na familia zao.

"Nataka mashirika yafanye kazi kwa uwazi na matumizi ya fedha yawe wazi kama ilivyopangwa katika kusaidia wananchi na sitegemei kuwepo kwa NGOs za mifukoni na kwenye simu zinazofanya kazi kwa maslahi ya familia zao,"amesema Kunenge.

Kunenge ameongeza kuwa, wajibu wa Serikali ni kuzifanya asasi hizo kujua mipango ya Serikali ili zifanye kazi kwa mashirikiano mazuri ya kutoa huduma kwa jamii kwa kuwa Serikali haiwezi kufanya kila kitu pekee yake.

"Kama Rais alivyosema anataka mashirika yajue mipango ya Serikali na lazima ninyi wenyewe mjue mnafiti namna gani kwa kuwa haiwezekani Serikali inasema inakwenda kulia halafu wewe unakwenda kushoto, jambo ambalo ni tofauti,"ameongeza Kunenge.

Amesema,kwa upande wa Serikali ya Mkoa wa Pwani imeamua kuubadilisha mkoa kwa kuwa mkoa ni mkubwa na endapo watashirikiana na mashirika hayo anaamini wataweza kufanya makubwa ya kitaifa na hivyo kuweza kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan anayefanya kazi kubwa kwa maendeleo ya Taifa.

Mjumbe wa Baraza la Taifa la mashirika yasiyo ya Kiserikali, Gaidon Haule amesema mkoa huo una mashirika 390 na kati ya hayo 133 pekee ndio yamehakikiwa.

Haule alisema mashirika hayo yanakabiliwa na vikwazo mbalimbali vikiwemo vya kukosekana kwa muendelezo baada ya fedha za wafadhili kuisha pamoja na uwepo wa sheria, kanuni na taratibu kandamizi katika utekelezaji wa shughuli za NGOs.

Alieleza changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya mashirika kutofuafa sheria na taratibu ikiwemo uwasilishwaji wa taarifa za utekelezaji wa shughuli zao, mapato na matumizi na hata fedha kutoka kwa wafadhili.

Kwa upande wake ofisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Pwani, Asha Itelewe amesema kuwa, Serikali ina matarijio makubwa ya kupata taarifa mbalimbali kutoka mashirika yasiyo ya Kiserikali.

Itelewe alisema moja ya matarajio hayo ni kupata za utendaji kwa wakati huku taarifa za utekelezaji ziliwasilishwe katika ngazi ya halmashauri,wilaya na mkoa.

Matarajio mengine ni pamoja na kuhakikisha huduma wanazotoa zitambulike uwepo wa uwazi wa taarifa za fedha pamoja na kuzingatia kufanya kazi kulingana na andiko la mradi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news