RC SENYAMULE: BILIONI 9.2/- ZA GGML ZILETE HESHIMA

NA ROBERT KALOKOLA, Geita

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule ameziagiza halmashauri mbili za Geita Mjini na Wilaya ya Geita kutumia vizuri fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 9.2 zilizotolewa na mgodi wa kuchimba dhahabu wa Geita (GGML ) kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ili ziweze kubadili maisha ya wananchi, ili utajiri wa madini ya dhahabu uonekane kwa wananchi kumletea mwananchi heshima.
Viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Geita , Halmashauri ya Wilaya ya Geita na GGML wakisaini hati ya makubaliano ya GGML kutoa sh.Bilioni 9.2 kutekeleza miradi ya maendeleo. (NA ROBERT KALOKOLA).
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahra Michuzi (katikati) akitoa saini makubaliano ya kutekeleza miradi ya CSR ya sh.Bilioni 4.9 kwenye halmashauri yake , mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita John Wanga (kulia) akisaini makubaliano ya Bilioni 4.3 na Mkurugenzi Mtendaji wa GGML Richard Jordinson (kushoto) baada ya kutia saini. (NA ROBERT KALOKOLA).

Ametoa agizo hilo katika hafla ya kutia saini makubaliano ya kutekeleza miradi ya maendeleo baina ya Halmashauri ya mji wa Geita, Halmashauri ya Wilaya ya Geita na GGML kupitia mpango wake wa wajibu wa kampuni kwa jamii( CSR) .

Senyamule amesema baadhi ya miradi itakayo tekelezwa ni ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira ambao amesema kuwa ukikamilika utaongeza thamani ya mji wa Geita na mkoa kwa ujumla hivyo ndiyo maana ya dhahabu kuleta heshima kwa wananchi kupitia miradi hiyo.

Ameitaka GGML , Halmashauri ya mji wa Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kufanya kazi kwa pamoja na karibu zaidi ili kutatua tatizo la kuchelewa kwa vifaa vya ujenzi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita, Constantine Morandi amewataka wazabuni wanaopata kazi za kusambaza vifaa vya ujenzi kufikisha vifaa kwa wakati ili miradi isichelewe kukamilika.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Geita, Zahra Michuzi (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Richard Jordinson (kushoto) wakibadilishana hati za makubaliano baada kusaini makubaliano ya miradi ya Bilioni 4.9 katika Halmashauri ya mji wa Geita. (NA ROBERT KALOKOLA).

Amesema kuwa, kwa kipindi cha miaka minne sasa GGML imeshirikiana bega kwa bega na Halmashauri hiyo na fedha zinazotolewa kupitia tozo ya huduma na mpango wa CSR imekuwa mkombozi mkubwa katika kutekeleza miradi mingi katika Halmashauri hiyo

Naye Makamu Rais wa Mgodi wa GGML, Simon Shayo amesema mgodi huo umetoa fedha Bilioni 9.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo hasa kwenye sekta za Afya,elimu, mazingira,utamaduni,utafiti na miundombinu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule (katikati mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa GGML na Halmashauri ya mji wa Geita baada kusaini makubaliano ya fedha za CSR Bilioni 9.2 kutekeleza miradi katika halmashauri mbili. (NA ROBERT KALOKOLA).

Amesema kuwa, GGML inafarijika kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na serikali na inaendelea kutimiza wajibu wake kama kampuni kinara katika ulipaji kodi nchini,kinara katika CSR na kinara katika kutunza mazingara na kuwezesha wazawa.

GGML imetoa shilingi Bilioni 9.2 ambazo zitatekeleza miradi mbalimbali katika Halmashauri mbili ambazo Halmashauri ya mji wa Geita itanufaika na Bilioni 4.9 na Halmashauri ya Wilaya ya Geita itanufaika na Bilioni 4.3.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news