Kocha Ole Gunnar Solskjaer kichwa kinamuuma, Watford watembeza kichapo cha 4-1 kwa vijana wake EPL

NA GODFREY NNKO

LICHA ya awali Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer kujigamba kuwa,wapo imara na mashabiki wa timu hiyo wataona mabadiliko ya kiuchezaji kwenye timu hiyo kuanzia kwenye mechi ya Novemba 20,2021 dhidi ya Watford, wamejikuta wakiondoka kwa kipigo dimbani.
“Wachezaji, viongozi, mimi mwenyewe na klabu inafanya kazi kwa ushirikiano kuhakikisha tunarudi kwenye njia zetu za ushindi. Tutakwenda kufanya vema,"amesema.

Pengine maneno hayo yamegeuka shubiri kwao, baada ya Watford kuwapa kipigo cha magoli 4-1 katika mtanange wa Ligi Kuu England (EPL).

Mtanange huo umepigwa Novemba 20,2021 katika dimba la Vqcarage Road.

Matokeo hayo yanampa wakati mgumu kocha Ole Gunnar Solskjaer, huku ikionekana wazi kuwa bado kikosi chake ni butu.

Magoli ya Watford ambayo kabla ya mchezo huo walikuwa hawajawai kushinda nyumbani yaliwekwa kimiani na Joshua King, Joao Pedro, Emmanuel Dennis na Sarr.

Aliyeanza kupeleka kicheko kwa mashabiki wa Watford ni King baada ya dakika ya 28 kuzichakaza nyavu za Manchester United, kabla ya kwenda mapumziko dakika ya 44 Sarr aliwanyanyua mashabiki wa Watford tena.

Kipindi cha pili kilianza kwa pande mbili kusomana. Hatua ambayo iliwezesha Donny van de Beek ndani ya dakika ya 50 kuwanyanyua mashabiki wa Manchester United akimalizia mpira wa staa wa klabu hiyo, Cristiano Ronaldo.

Ingawa kasi yao ilipungua baada ya Maguire ndani ya dakika ya 69 kupewa kadi nyekundu.

Wakiwa pungufu Manchester United, waliendelea kutafuta namna ya kujinasua, hadi dakika ya tisini, nyongeza ya dakika iliwagharimu Manchester United, kwani Pedro wa Watford ndani ya dakika ya tisini na ushee aliachia bao lingine, bao ambalo lilidumu dakika chache ambapo Dennis aliongeza kilio kwa Manchester United kwa kuweka kimiyani bao la nne.

Hata hivyo, kipigo hicho kinaifanya Manchester United kwa sasa kubakia nafasi ya saba na alama 17 wakati Watford wakiwa nyuma ya United kwa tofauti ya alama nne katika nafasi ya 16 ya Msimamo wa Ligi Kuu England.

Post a Comment

0 Comments