Maagizo ya Waziri Prof.Ndalichako kuhusu mafanikio ya Sekta ya Elimu nchini

NA MWANDISHI MAALUM

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka Maafisa Mawasiliano wa Wizara hiyo na Taasisi zilizo chini ya Wizara kutangaza mafanikio ya Sekta ya Elimu ili wananchi waweze kufahamu namna Serikali ilivyowekeza fedha nyingi katika kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu nchini.
Baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Maafisa Mawasiliano wa Taasisi hizo wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano hao kinachofanyika mkoani Morogoro.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo mkoani Morogoro wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa hao kilichowashirikisha Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ambapo amesema mafanikio makubwa katika sekta ya elimu si ya kificho, hivyo ni vyema yakawa yakitolewa kwa wananchi ili waweze kufahamu ni namna gani Serikali yao ilivyowekeza katika kuhakikisha Watanzania wanapata elimu bora.

Amesema ameshuhudia mara nyingi Maafisa Mawasiliano hao wamekuwa wakijielekeza zaidi katika kutangaza matukio ya viongozi wanapokuwa na shughuli mbalimbali katika taasisi zao na baada ya matukio hayo hakuna kinachoendelea. Amewataka Maafisa hao kubadili utaratibu huo na kujikita zaidi katika kutangaza mafanikio makubwa ya uboreshwaji wa mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

“Nimefurahi kwamba katika mafunzo haya wakuu wa Taasisi wameshiriki, naamini ushiriki wenu utaleta mabadiliko na kuwa wepesi wa kutoa habari fasaha na kwa wakati. Tuepuke urasimu, yapo mambo yanatokea kwenye vyombo vya habari na mitandao lakini mmekuwa wazito kutoa mrejesho kwa wananchi, ni vizuri kufanyia kazi ili kuepuka mkanganyiko,” amesema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano wa Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara kinachofanyika mkoani Morogoro.

Kiongozi huyo amesema kikao kazi hicho kimekuja wakati muafaka ambapo nchi inaelekea kuadhimisha miaka ya 60 ya uhuru na kwamba katika sekta ya elimu kuna mafanikio mengi ambayo yanaweza kuandikwa na kutangazwa pamoja na kuunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa nguvu zote.

Akizungumza katika kikao hicho Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe amesema lengo la kikao kazi hicho ni kutathmini utekelezaji wa majukumu ya Mawasiliano katika Wizara na Taasisi zilizo chini yake, kupanga mikakati ya pamoja ya kuboresha utendaji kazi kimkakati pamoja na kupata mafunzo yanayoendana na kada hiyo kutokana na mabadiliko ya kisayansi, kiteknolojia, kisiasa, kijamii na kiuchumi ili kuendelea kuboresha utendaji kazi kimkakati.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano wa Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara (hawapo pichani) kinachofanyika mkoani Morogoro.
Baadhi ya Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara na Maafisa Mawasiliano wa Taasisi hizo wakifuatilia mada kutoka kwa mwezeshaji Primus Innocent Mungy katika kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano hao kinachofanyika mkoani Morogoro.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Wizara na Taasisi, Maafisa Mawasiliano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo mara baada ya ufunguzi wa kikao kazi cha kuwajengea uwezo katika utendaji kazi Maafisa Mawasiliano hao kinachoendelea mkoani Morogoro.

Prof. Mdoe ametoa rai kwa maafisa hao kuendelea kufanya kazi kwa karibu na vyombo vya habari ili kuendelea kutangaza mafanikio ya Sekta ya elimu.

Akizungumza kwa niaba ya Viongozi wa Taasisi walioshiriki kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, Dkt. Amosi Nungu amemuahidi Waziri Ndalichako kuwa wataendelea kutangaza mafanikio hayo kwa ukubwa wake ili fedha zinazotolewa na Serikali matokeo yake yaweze kuonekana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news