Serikali yapokea taarifa ya mapendekezo ya maboresho ya sheria katika Sekta ya Habari nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limekabidhi serikalini mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali zinazogusa sekta ya habari nchini.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kulia) akipokea taarifa ya mapendekezo ya maboresho ya Sheria zinazogusa Sekta ya Habari kutoka kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Deodatus Balile (kushoto), jijini Dodoma. Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula na kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi.

Mapendekezo hayo yanagusa sheria na/au baadhi ya vifungu vya sheria ambavyo kwa mtazamo wa wadau wa habari nchini, vinakwaza kwa namna moja au nyingine uandishi wa habari na vyombo vya habari katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mapendekezo hayo yamepokewa leo Novemba 16, 2021 jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Ashatu Kijaji kutoka kwa Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balile amesema, muhtasari uliowasilishwa unalenga kuiwezesha Serikali kuzingatia mapendekezo ya wadau wa habari katika mchakato wa marekebisho ya sheria husika, kabla ya kupelekwa bungeni kwa ajili ya kupata baraka za Bunge.

“Sheria zilizochambuliwa katika muunganisho huu ni Sheria ya Huduma za Habari, 2016, Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa, 2016 na ile ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta; (Maudhui ya Mtandaoni) Kanuni, 2020 na Sheria ya Uhalifu wa Mtandao,2015,”amesema Balile.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) akionesha taarifa ya mapendekezo ya maboresho ya Sheria zinazogusa Sekta ya Habari mara baada ya kuipokea kutoka kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Deodatus Balile (hayupo pichani), jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula na kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi.

Ametaja baadhi ya mambo ambayo wadau wanaomba kufanyiwa marekebisho au kubadilishwa katika Sheria hizo kuwa ni pamoja na mamlaka ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) ambayo inaweza kufungia vyombo vya habari vinapodhaniwa au kutuhumiwa kuwa vimekosea, bila suala au makosa husika kufikishwa katika vyombo vya kisheria vya kiuamuzi kama Mahakama.

“Wadau tunaona kuwa kifungu kama hiki kinamnyima mtuhumiwa nafasi ya kujitetea na kinakiuka kanuni ya msingi ya chombo kusikilizwa kabla kuhukumiwa,” amesema Balile.

Mwenyekiti huyo wa Jukwaa la Wahariri ametaja suala jingine kuwa ni Sheria ya Huduma za Habari (MSA) kuanzisha vyombo vinne vya kusimamia sekta ya habari, tofauti na sekta au taaluma nyingine ambako masuala husika husimamiwa na chombo au mamlaka moja.

“MSA inaanzisha Accreditation Board (Bodi ya Ithibati), Mfuko wa kusomesha waandishi wa habari na Independent Media Council (Baraza Huru la Habari), sisi katika hili tunapendekeza kuwapo kwa chombo kimoja pekee cha kuratibu sekta badala ya kuwa na vyombo vingi,”amesema.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula (kushoto) na kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi mara baada ya Waziri huyo kuwakabidhi taarifa ya mapendekezo ya maboresho ya Sheria zinazogusa Sekta ya Habari kwa ajili ya utekelezaji aliyoipokea kutoka kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Deodatus Balile (hayupo pichani), jijini Dodoma.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kulia) akimsikiliza Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Deodatus Balile (kushoto) baada ya kukabidhi taarifa ya mapendekezo ya maboresho ya Sheria zinazogusa Sekta ya Habari kwa Waziri huyo jijini Dodoma. Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula na kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi.

Amesema, mchakato mzima wa kupata maoni na mapendekezo yaliyowasilishwa, umezingatia ushirikishwaji wa wadau wengine wa habari kupitia Umoja wa Haki ya kupata taarifa (CORI) (ambao TEF ni mwanachama wake), ukiunganisha taasisi 11 chini ya Uenyekiti wa Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Pamoja na TEF, wengine ni Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tawi la Tanzania (MISA – TAN), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Kituo cha Taarifa kwa Wananchi (CIB), Twaweza, SIKIKA na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Amesema, katika mchakato huo pia kulikuwa na fursa ya kupata maoni ya Wahariri na baadhi ya wawakilishi wa Vilabu vya Waandishi wa Habari vya mikoa (Regional Press Clubs), katika kusanyiko lililoitishwa na TLS mjini Dodoma.

“Tulipata pia fursa ya kupata mawazo ya watu wenye uzoefu wa masuala ya habari na taarifa kama Jenerali Ulimwengu na Mkurugenzi wa Jamii Media, Maxence Mello,”amesema Balile.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (kushoto) akizungumza mara baada ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Deodatus Balile (hayupo pichani) kukabidhi taarifa ya mapendekezo ya maboresho ya Sheria zinazogusa Sekta ya Habari kwa Waziri wake Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) baada ya kumkabidhi Katibu Mkuu huyo kwa ajili ya utekelezaji jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (kushoto) akizungumza mara baada ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Deodatus Balile (hayupo pichani) kukabidhi taarifa ya mapendekezo ya maboresho ya Sheria zinazogusa Sekta ya Habari kwa Waziri wake Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kulia) baada ya kumkabidhi Katibu Mkuu huyo kwa ajili ya utekelezaji jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi. Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala Teddy Njau na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa.

Akizungumza baada ya kupokea Muhtasari wa mapendekezo hayo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Kijaji amesema Serikali itayafanyia kazi mapendekezo hayo kwa lengo la kuiwezesha sekta ya habari kuwa rafiki kwa wadau wake, hususan waandishi wa habari.

“Lengo la serikali ni kuhakikisha kwamba sekta ya habari inakuwa rafiki na ni dhamira yetu sote kupiga hatua na kufikia malengo ya ufanisi utakaokuwa na faida kwa kila mmoja. Hatua ya leo ni mwanzo mzuri na ninaamini tutapiga hatua kwa faida ya taifa letu,”amesema Dkt.Kijaji.

Baada ya kupokea mapendekezo hayo, waziri huyo ameyakabidhi kwa Katibu Mkuu wake, Dkt.Zainab Chaula pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Jim Yonazi kwa ajili ya kuanza kuyafanyiwa kazi.

“Kazi ndiyo imeanza, hakuna kusubiri, kwa hiyo baada ya kuyapokea naomba na mimi nikukabidhi Katibu Mkuu kwa ajili ya kuyafanyia kazi,”amesema Dkt.Kijaji.

Post a Comment

0 Comments