Machinga kwa nini mmekodisha maeneo yenu au kuyauza? Mmenisikitisha sana-DC Mtanda

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Serikali wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro imeelezea kusikitishwa kwake na baadhi ya wamachinga kukodisha maeneo waliyopewa kwa ajili ya kufanya biashara, badala ya kuyatumia wao wenyewe kama ilivyoelekezwa na Serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi,Mheshimiwa Said Mtanda ameyasema hayo mjini hapa ambapo amesema inasikitisha kuona baadhi ya machinga hao kuanza kwenda kinyume cha agizo la Serikali.

"Sisi kama Serikali ya wilaya tuliwapeleka katika soko la Memorial wamachinga takribani 700 na kuwaonesha maeneo ambayo wametengewa ili kufanya biashara zao cha kusikitisha kuna wengine wameanza kuwauzia wenzao, hili halikubaliki na tutaanza kulifanyia kazi,"amesema.

Mtanda amesema kwa upande mwingine baadhi ya machinga wameanza kuzoea mazingira hayo mapya ya kufanyia kazi, ambapo kwa upande wake Serikali inaendelea na mipango ya kuboresha miundombinu ya soko hilo.

"Serikali ya wilaya imeomba shilingi milioni 300 kwa ajili ya kurekebisha miundo mbinu muhimu katika soko la Memorial na tayari tumeuagiza uongozi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) kuhakikisha wanapeleka maji katika soko hilo,"amesema.

Aidha, amesema uongozi wa halmashauri ya Manispaa ya Moshi pia inaendelea na mpango wa kujenga vyoo vya kisasa katika soko hilo ambapo alisema ni sehemu ya kuboresha mazingira ya soko hilo kuwa bora kwa ajili ya matumizi ya wafanyabiashara na wateja wao.

Amesema kutengewa machinga eneo hilo kumelenga kuboresha mazingira ya mji wa Moshi, ambao una historia ya kuwa mji msafi kwa miaka mingi iliyopita na si kwa sababu nyingine yoyote.

"Mabadiliko haya yanalenga kuendeleza taswira njema ya mji wa Moshi ambao ni mji wa kitalii na kwa kufanya hivi kutazidi kuvutia wageni wengi wakiwemo watalii wenyewe na hata soko lenyewe litakuwa ni kivutio cha utalii kutokana na kuwa eneo lililotengwa kijografia kuwa la kibiashara,"alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Kilimanjaro, Aladin Kikoti ametoa ombi kwa Serikali pamoja kuona umuhimu wa kutenga baadhi ya barabara ili machinga wafanye biashara zao sehemu yenye mzunguko wa fedha ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news