'Msithubutu kutafuna fedha zilizotolewa na Rais Samia'

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Madiwani na Watendaji wa Serikali mkoani Tabora wametakiwa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia ipasavyo fedha zote anazotoa kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maendeleo.

Rai hiyo imetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora, Ramadhan Kapela katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri.

Kapela amesema kuwa,katika kipindi kifupi tu cha utawala wake, Rais Samia ametoa fedha nyingi kwa halmashauri hiyo ambazo hazikuwemo hata kwenye bajeti yao ya maendeleo, hivyo kuchochea kasi ya utekelezaji miradi mingi ya maendeleo.

Alisisitiza kuwa ni jukumu la madiwani na watendaji wa halmashauri ni kuhakikisha fedha hizo zinazitumika kwa lengo lililokusudiwa na si vinginevyo, alionya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa mtu yeyote atakayezitumia vibaya.

"Rais Samia anafanya kazi kubwa sana, naomba tumuunge mkono kwa kusimamia ipasavyo miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za Serikali ya Awamu ya Sita zaidi ya sh. bilioni 1.5 tulizoletewa ili kazi iendelee kwa kasi kubwa,"amesema.

Mstahiki Meya amebainisha kuwa kasi na utendaji wa Rais Samia unawarahisishia kazi Madiwani na Wabunge na kuongeza kuwa miradi inayotekelezwa kama itasimamiwa vizuri uchaguzi wa mwaka 2025 utakuwa mwepesi kwao.

Aidha katika kuhakikisha fedha zilizoletwa na Mheshimiwa Rais zinatumika ipasavyo aliomba Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Dkt . Peter Nyanja kuitisha kikao cha haraka cha madiwani, watendaji na wakuu wa shule ili kila mmoja awe makini na fedha hizo, wala asizichezee.

Dkt.Peter Nyanja amebainisha kuwa fedha zote zilizoletwa na Mheshimiwa Rais zitatumika ipasavyo kwa miradi iliyokusudiwa na hakuna hata senti moja itakayoibiwa, aliwataka wakuu wa Idara wote kutokaa maofisini bali waende kufuatilia mapato na kuangalia miradi inayotekelezwa.

Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Dkt.Yahaya Nawanda amesema haijawahi kutokea katika kipindi cha miezi mitatu tu Rais amewaletea shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara na shilingi bilioni moja kwa ajili ya elimu, hivyo wanampongeza Rais kwa hatua hiyo na watahakikisha zinafanya kazi tarajiwa kwa wakati.



Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news