Wasomea chini ya miti,wakosa sehemu za kurekebishia tai

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

CHAMA cha Walimu nchini (CWT) Wilaya ya Kilolo kimeabainisha kuwepo kwa changamoto ya miundombinu katika Sekta ya Elimu ikiwemo ukosefu wa vyumba vya kutosha vya madarasa, hali inayowalazimu baadhi ya wanafunzi kusomea chini ya mti, jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya elimu katika wilaya hiyo.
Katibu wa Chama CWT Wilaya ya Kilolo, Anton Mangw`alu akiongea na walimu wakati wa mafunzo ya walimu mahali pa kazi.

Akizungumza wakati mafunzo kwa walimu wawakilishi mahali pa kazi yanayoendeshwa na CWT Wilaya ya Kilolo, Katibu wa Anton Mangw`alu amesema kuwa wilaya ya hiyo ina na changamoto lukuki kama vile uhaba wa vyumba wa kusomea wanafunzi,shule kuwa na kitabu kimoja cha hisabati jambo linalozorotesha ufanisi kwa walimu.

Amesema kuwa, baadhi ya shule kama Shule ya Msingi Kidabaga na Shule ya Msingi ya Lyamko iliyopo kata ya Bomalang’ombe zinakabiliwa na uhaba wa vitabu vya kufundishia masomo wanafunzi ambao shule zote hizo zina kitabu kimoja kimoja cha hisabati kwa kila darasa jambo linalozorotesha ufanisi kwa walimu.

Mwalimu Mangw`alu amesema, kukosekana kwa vitabu vya kutosha katika shule nyingi zilizopo Wilaya ya Kilolo kunachangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi wengi kushindwa kufaulu mitihani ya taifa kutokana na wanafunzi wengi kushindwa kuwafundisha vizuri na walimu kwa ajili ya ukosefu wa vitabu husika.

Amesema kuwa changamoto nyingine ni kukosekana kwa vyumba vya madarasa jambo ambalo linachangia wanafunzi wengine kusomea chini ya miti jambo ambalo sio sawa kabisa kwa wakati uliopo kwa mfano Shule ya Msingi Lukoga haina vyumba vya madarasa kabisa na wanafunzi wake wanasomea chini ya miti na shule ya msingi Kitelewasi hakuna kabisa vyoo vya walimu jambo ambalo linawaweka katika mazingira magumu walimu wakati wa kufundisha.

“Kwa mazingira kama hayo ndugu zangu waandishi wa habari lazima walimu watakuwa na wakati mgumu wakati wa kufundisha wanafunzi hawana vyoo,hakuna vyumba vya madarasa,maslahi yao bado duni,hivyo ni lazima Serikali ya Wilaya ya Kilolo ihakikishe inatafuta namna ya kutatua changamoto hizo,”amesema mwalimu Mangw`alu.
Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Kilolo, Mtemi Mgalula akiongea na walimu wakati wa mafunzo mahali pa kazi.

Mwalimu Mangw`alu amesema, licha ya changamoto hizo bado walimu wa Wilaya ya Kilolo wamekuwa wakitumia jitihada binafsi na kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri kwenye mitihani yao na kufanya vizuri kitaifa.

Aidha, Mwalimu Mangw`alu ameiomba serikali ya wilaya hiyo kuboresha mazingira ya walimu
wawapo kazini na kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo pamoja na zile zinazohusu maslahi ya waalimu ili kusaidia ukuaji wa taaluma na ubora.

Licha ya changamoto hizo CWT Wilaya ya Kilolo wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwapandisha madaraja na kuongeza ajira za walimu kwa kipindi kifupi ambacho yupo madarakani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Kilolo, Mtemi Mgalula amesema kuwa, wanafunzi wa baadhi ya shule wamekuwa wanakumbana na changamoto ya kufanya mitihani kwenye vyumba vya madarasa ambavyo havina madirisha wala milango hivyo ukitokea upepo wanafunzi wanakuwa kwenye mazingira magumu.

“Ukipiga upepo karatasi zile ni kukimbiza nazo kwa kuwa darasa hayana madirisha,fremu wala milango kwa kuwa hakuna kitu ambacho kina uwezo wa kuzuia upepo katika madarasa hayo,”amesema Mgalula.

Alisema kuwa, wamekuwa wakipokea malalamiko mara kwa mara juu ya changamoto ya miundombinu ambavyo imekuwa ikiwaweka walimu katika mazingira magumu ya ufundishaji kwa wanafunzi husika.

Mwalimu Mgalula alisema kuwa bado walimu wa wilaya hiyo wanadai madai ya uhamisho ambayo hadi sasa hawajalipwa mfano ya walimu waliohamishwa kutoka shule ya sekondari kwenye shule ya msingi jumla walimu 99 walihamishwa na walimu 26 tu ndio waliolipwa stahiki zao, lakini wote waliobaki bado hawajalipwa madai yao.

Aidha, Mwalimu Mgalula alisema kuwa zoezi la sensa ni muhimu sana kwa taifa kujua idadi ya wakazi kwa ajili ya kupanga mipango ya kuleta maendeleo kwa wananchi hivyo jukumu la walimu kumuunga mgono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kufanikisha zoezi hilo kwa asilimia 100.

Alisema kuwa, walimu wanapaswa kuendelea kutoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia kwenye jamii ambazo wanaishi nazo huku ili kuwa na kizazi ambacho kitakuwa na maadili bora nakutomeza kabisa masuala yote ya ukatili wa kijinsia.

Mwalimu Mgalula alisema, walimu wanatakiwa kuendelea kuwa na maadili bora ili kuwasaidia wananchi wengine kuiga mfano wao kwa namna ya kufanya kazi kwa kujituma na kulijenga taifa kiuchumi na kielimu.

Alisema kuwa, rushwa ni adui wa maendeleo ya wananchi wote hivyo walimu wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanapinga vitendo vyote vyenye viashiria vya rushwa.

Naye mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kilolo ambaye aliwakilishwa na Afisa Tarafa ya Mazombe, Silvanus Kingu’ung’e aliwataka walimu kuwa mabalozi wa kukemea vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi yao ikiwemo kujihusisha kingono na wanafunzi kwani tabia hiyo inadhalilisha taaluma yao.

Kingu’ung’e amesema kuwa, walimu wenye maadili ni lazima wajikite kwenye uzalendo na uadilifu ili kuwa mfano bora kwa jamii.

Amesisitiza kuwa, viongozi wa CWT wanatakiwa kuweka mikakati ya kuwabaini walimu wanaojihusisha kimapenzi na wanafunzi ili kukomesha tabia hiyo ya unyanyasaji na ukatili unaokatisha ndoto za wanafunzi hasa wa kike

Kingu’ung’e amesema kuwa, ni aibu kusikia mwalimu ana uhusiano wa kingono na mwanafunzi
jambo hilo limekuwa likiitia doa kada ya ualimu kwa vitendo amvyo vinafanywa na baadhi ya walimu kwa wanafunzi.

Alisisitiza kuwa, walimu wote wanatakiwa kuwa mfano bora wa kuigwa na jamii kwa kukemea vitendo vya ukatili na mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Picha pamoja baadhi ya walimu na viongozi wa serikali walipofika wakazi wa ufunguzi wa mafunzo hayo

Kingu’ung’e alimtaka mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kilolo kuhakikisha anazitatua mara moja changamoto za walimu kwa kuwa walimu wana mchango mkubwa kwenye maendeleo ya taifa la Tanzania.

Alikiri uwepo wa uhaba wa vitendea kazi na kuahidi kulifanya kazi jambo hilo na kulitatua mara moja tatizo hilo kwa ajili ya maendeleo ya elimu kwa wanafunzi wa Wilaya ya Kilolo.

Kingu’ung’e aliwataka walimu kuendelea kufundisha kwa moyo wote huku serikali ikiendelea kutatua changamoto ambazo zimekuwa zinawakumba walimu wa wilaya ya Kilolo kuanzia miundombinu,mazingira ya shule na kuboresha maslahi ya walimu kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu katika wilaya hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news