Maagizo ya Waziri Nape kwa viongozi Mkoa wa Pwani kuhusu anuani za makazi

NA ROTARY HAULE

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amefungua mafunzo ya kujenga uelewa wa anuani za makazi kwa viongozi wa Mkoa wa Pwani huku akitoa maagizo kwa viongozi hao kuhakikisha wanatekeleza mpango huo kwa muda uliopangwa.
Mheshimiwa Nape amesema ifikapo mwezi Mei mwaka huu Wizara yake inatarajia kumkabidhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan taarifa kamili ya kukamilika kwa anuani na makazi.

Nape ametoa maagizo hayo leo alipokuwa akifungua mafunzo ya kujenga uelewa wa anuani za makazi kwa Wakurugenzi wa Halmashauri,Wakuu wa Wilaya, wataalamu na viongozi wa CCM yaliyofanyika Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani Mjini Kibaha. 

Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kutekeleza mradi huo kurahisisha mawasiliano kwa wananchi wake lengo Ni kuhakikisha kunakuwa na anuani za makazi na kwamba Wizara yake itasimamia ipasavyo ili ukamilike kwa wakati.
Amesema,mradi huo wa anuani za makazi ulitakiwa kufanyika kwa miaka mitano lakini kwa sasa utatakiwa kukamilika Mei 22 baada ya kuonekana ni muhimu kusaidia zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti.

Kwa mujibu wa Waziri Nape, Pwani ni kati ya mikoa ambayo viongozi wake tayari wamepatiwa mafunzo, lakini hadi sasa utekelezwaji wake ni asilimia moja ambapo ni kata tatu pekee kati ya 139 ambazo zimeanza kutekeleza mradi huo.

"Tumekuja kukaa na Mkuu wa mkoa ili waone namna ya kufanya, kujipanga na kutekeleza mradi huu kwa muda uliowekwa hakuna kuongeza muda na ninasema hatutashindwa Wizara yangu itakabidhi mradi kwa wakati,"amesema.

Amesema,mradi huo unahusisha uwekaji wa nguzo na vibao kwenye mitaa ambapo kwa mkoa huo nguzo 75,392 na vibao 912,640 vinahitajika kufanikisha zoezi hilo.

Nape alimtaka mkuu wa mkoa wa Pwani,Abubakar Kunenge kuweka mipango ya namna ya kutekeleza mradi huo na wakuu wake wa wilaya na wizara iko tayari kutoa ushirikiano kwa ajili ya kuhakikisha mpango huo unakamilika kwa wakati.

"Kikubwa ni mipango mizuri ya kuweza kulitekeleza hili kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya , sisi kule Wizarani tumeweka utaratibu wa kupata taarifa kila baada ya wiki mbili tujipange kuanzia vijijini na kwenye mitaa,"amesema.
Amesema, kukamilika kwa mradi huo wa anuani za makazi itaongeza ajira,uchumi na utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo husika.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mkurugenzi wa Mawasiliano,Clarence Ichwekeleza amesema anuani za makazi zinarahisisha kufika kwenye maeneo kwa urahisi.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge , amesema suala la anuani za makazi litarahisisha kuelewa kila mmoja anakaa wapi.

Kunenge amesema, kufanyika kwa mradi huo mkoa utakuwa na manufaa hususani upande wa viwanda ambapo wanaohitaji kufika kupata bidhaa watapata urahisi na hata huduma nyingine zitafanyika.
"Anuani za makazi zikikamilika itarahisisha kama mtu anataka kufika kiwanda fulani inakuwa rahisi kwake kwenda kufuata bidhaa anayoitaka mimi na time yangu ninaahidi ushirikiano kwa Wizara kufanikisha hili," amesema Kunenge.

Hata hivyo, Kunenge amemuahidi Waziri kuwa atasimamia mpango huo kikamilifu kwa kushirikiana na timu yake ili uweze kukamilika katika muda uliopangwa na Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news