Mheshimiwa Othman ampa pole Rais Dkt.Mwinyi kufuatia kifo cha shangazi yake

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, leo Januari 31, amefika na kutoa mkono wa pole kwa Familia ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi, kufuatia kifo cha Shangazi yake Bi.Hamisa Hassan Mwinyi, aliyefariki na kuzikwa leo huko Yombo jijini Dar es Salaam.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 31, 2022 na Kitengo cha Habari Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Marehemu Bi Hamisa Hasan Mwinyi ambaye ni Dada wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Ali Hassan Mwinyi na shangazi wa Dkt. Mwinyi amefariki leo katika Hospitali ya Mloganzila na kuzikwa kwake Yombo.
Mapema Mhe. Othman aliungana na familia, wananchi na waumini wa kiislamu kutoka maeneo mbalimbali, wakiongozwa na Mhe.Dkt. Mwinyi katika sala na dua ya kumuombea marehemu na baadae kumsindikiza katika safari yake ya milele kwenye makaburi ya eneo lililopo jirani na alipokua anaishi huko Yombo majira ya alasiri.

Marehemu Bi.Hamisa alizaliwa mwaka 1946 na hadi anafariki alikuwa na umri wa miaka 76. Mungu ailaze mahala pema peponi roho ya marehemu. Amen.

Post a Comment

0 Comments