RC PWANI AWATOA HOFU WAWEKEZAJI WA VIWANDA, ASEMA SERIKALI YA AWAMU YA SITA IMEJIPANGA KUTATUA CHANGAMOTO ZAO,ATAKA WATANZANIA KUTUMIA BIDHAA ZA NDANI

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewatoa hofu wawekezaji wa viwanda waliopo mkoani kwake juu ya changamoto zinazowakabili kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan imejipanga vizuri katika kuwasaidia wawekezaji.

Aidha,Kunenge amesema Serikali ya Mkoa wa Pwani tayari imejipanga katika kutatua changamoto hizo kwa kuwa wawekezaji hao wamekuwa na msaada mkubwa hususani katika kutoa ajira kwa watanzania na hata kuongeza pato la Taifa.
Kunenge amesema hayo katika ziara yake ya kutembelea na kukagua viwanda vilivyopo Mjini Kibaha ambapo lengo kubwa la ziara hiyo ni kujionea namna vinavyofanyakazi sambamba na kupokea changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji hao ili ziweze kufanyiwa kazi.

Mapema Januari 27, 2022 Mheshimiwa Kunenge alianza kutembelea kiwanda cha KEDS Tanzania Limited kinachotengeneza sabuni za kufulia na kuogea pamoja na taulo za watoto (Pampers) ambapo alipokea changamoto ya kuwepo kwa umeme mdogo ambao haukidhi mahitaji wakati wa uzalishaji.
Akiwa kiwandani hapo Kunenge,ameeleza kufurahishwa na uwekezaji huo mkubwa huku akisema Serikali itaendelea kushirikiana na kiwanda hicho ili kutatua changamoto zake na hata kusaidia katika masuala mengine muhimu.

"Nimefika hapa nimeona uwekezaji huu mkubwa wenye mashine za kisasa lakini nimpongeze Rais Samia kwa kuweka mazingira mazuri ya wawekezaji na tayari ametoa maelekezo kwamba hataki kuona vikwazo kwa wawekezaji,"amesema Kunenge.

Kunenge amesema kuwa, kuwepo kwa viwanda hivyo ni faida kwa Taifa kwa kuwa Serikali inapata mapato na vijana wanapata ajira ambapo hata hivyo alitoa wito kwa Watanzania kutumia bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo ili kuunga mkono juhudi za wawekezaji hao.
"Kiwanda hiki cha Keds ni kikubwa ndani ya Afrika Mashariki na kinazalisha bidhaa zenye ubora kwahiyo kikubwa ni kukiunga mkono kwakuwa bidhaa zake ni nzuri lakini kuhusu changamoto ya umeme nimeichukua na itafanyiwa kazi,"amesema Kunenge.

Kunenge ameongeza kuwa, kama wanataka kupanua kiwanda hicho waombe ardhi na watapata kwa kuwa Serikali itawasaidia huku akiwasisitiza kuendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu kwa maslahi ya Watanzania.

Kwa upande wake meneja utawala wa kiwanda hicho, Nasib Noor,amesema kuwa kiwanda chake kinazalisha sabuni aina zote pamoja na taulo za watoto huku akisema soko kubwa lipo katika sabuni ya unga.
Noor amesema mpaka sasa kiwanda hicho kimeajiri zaidi ya Watanzania 800 na kwamba ajira zitaendelea kutolewa kadri mahitaji yatakapoongezeka huku akisisitiza kutatuliwa kwa changamoto ya umeme.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news