Royal Supermarket yawekeza Bilioni 25/- kiwanda cha mikate, kuzalisha mikate 100,000 kwa siku, RC Kunenge apokea kilio chao

NA ROTARY HAULE

MKURUGENZI wa kiwanda cha kutengeneza Mikate cha Royal Supermarket kilichopo katika eneo la Viwanda la Zegereni Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Jesca Nkwabi amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge kuwasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika kiwanda hicho.
Amesema, changamoto ya ukosefu wa maji kwao ni kikwazo kikubwa cha uzalishaji wa mikate hiyo, lakini endapo watapata maji itawasaidia kufanya uzalishaji kwa wakati.

Nkwabi ametoa ombi hilo mbele ya Mkuu wa Mkoa Abubakar Kunenge alipotembelea Januari 27,2022 kiwandani hapo kwa ajili ya kuona maendeleo ya kiwanda hicho pamoja na kujua changamoto zake ili aweze kuwasaidia.

Amesema, kiwanda hicho ambacho uwekezaji wake umegharimu kiasi cha sh. Bilioni 25 kinatarajia kuanza uzalishaji Aprili, mwaka huu ambapo kwa siku kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mikate 100,000 itakayouzwa ndani na nje ya nchi.

Aidha,Nkwambi amemueleza mkuu wa mkoa kuwa ili watimize malengo ya kuanzisha uzalishaji ni lazima wapate maji ya uhakika ambayo ni salama na yasiyokatika mara kwa mara.
Kutokana na ombi hilo Kunenge ameahidi kushughulikia kero hiyo ambapo amemueleza Mkurugenzi huyo kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameahidia kushughulikia vikwazo vya uwekezaji ambavyo ni pamoja na huduma ya maji, umeme na barabara.

Kunenge amesema kuwa, Rais wa Awamu ya Sita Mama Samia tayari ameweka mipango mizuri ya kutatua kero hiyo ya maji pamoja na kero nyingine na kwamba yeye ni msaidizi wa Rais ambaye yupo kwa ajili ya kuwasaidia kutatua kero hizo.

"Mimi nimekuja hapa kujua maendeleo ya kiwanda hiki lakini mmenipa changamoto ya ukosefu wa maji lakini nataka niwaambie leo nimekuja na majibu mazuri ya changamoto hizi kuwa zitatatuliwa haraka iwezekanavyo,"amesema Kunenge.

Kunenge amesema, Rais Samia anatambua umuhimu wa wawekezaji nchini ndio maana ameweka mazingira rafiki kwa wawekezaji ili waweze kuzalisha kwa wingi ili kuweza kuongeza pato la Taifa na hata wananchi kiujumla.

Kuhusu miundombinu ya barabara amesema, tayari zipo fedha zaidi ya sh bilioni 18 ambazo zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara Kilomita 12.5 inayoelekea eneo la Viwanda la Zegereni.

"Changamoto zote ikiwemo ya maji,umeme na barabara zinakwenda kumalizika muda mfupi ujao na kwa upande wa barabara tayari fedha zipo na inaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ambayo itawasaidia wawekezaji kusafirisha bidhaa zao,hii yote ni kazi ya Rais Mama Samia, kwa hiyo ni vyema tukapongeza juhudi zake,"amesema Kunenge

Kunenge amewataka wawekezaji hao kuendelea kuwekeza kwa kufanya uzalishaji mkubwa kwakuwa wapo salama na Serikali inawalinda huku akitaka wawekezaji wengine wajitokeze zaidi.

"Waambieni wawekezaji wengine waje wasiogope Mkoa wa Pwani una maeneo ya kutosha ya uwekezaji na sisi kama Serikali kazi yetu ni kuwaandalia mazingira mazuri, lakini na nyinyi wawekezaji hakikisha mnafuata sheria na sera za uwekezaji,"amesema
Hata hivyo, Kunenge amewaomba wawekezaji hao kuhakikisha wanatoa huduma za jamii kwa wananchi waliopo karibu na maeneo yao ya uwekezaji ili waone umuhimu wa kuwepo wa viwanda hivyo katika maeneo hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news