Uongozi wa Waziri Mchengerwa watoa suluhisho kilio cha miaka nenda rudi kwa wasanii nchini

NA JOHN MAPEPELE

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema wizara yake kupitia Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) itaanza kugawa mirahaba kwa kazi mbalimbali za wasanii zinazotumika kwenye redio kila baada ya miezi sita ili waweze kunufaika na kazi zao.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa utoaji wa tuzo za muziki na ugawaji wa mirahaba kwa wasanii Januari 28, 2022 kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe Mchengerwa amesema, wizara yake inakwenda kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta hizo katika kipindi kifupi kijacho ambapo amewataka watendaji wa Serikali kufanya kazi kwa kasi na weledi.

Ametoa muda wa wiki tatu kwa watendaji wa Wizara kuandaa App maalum itakayoitwa “Sema na Waziri wa Utamaduni" ambayo itatoa fursa kwa wadau mbalimbali wa sekta ya sanaa, utamaduni na michezo kuwasiliana moja kwa moja na yeye pindi wanapotaka kuwasiliana naye badala ya mfumo wa sasa uliozoeleka.
“Naomba niwaahidi hapa kuwa nitakuwa nanyi na milango itakuwa wazi wakati wowote ili kila mmoja wenu mwenye shida aweze kusaidiwa kikamilifu, hii wizara ni kwa ajili yenu inapaswa mfaidike nayo,” amesisitiza Mhe. Mchengerwa.

Amelielekeza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuhakikisha kuwa linafanya kazi yake ya kukuza, kuendeleza na kuwasaidia wasanii wa Tanzania kwa weledi na waache mara moja kufanya kazi kwa mazoea, ambapo amesisitiza kuwa waanze kujipanga kwa ajili ya kuandaa tuzo kubwa za kimataifa.

Akizungumzia mchakato wa utoaji wa Tuzo za Muziki ambazo kilele chake kitakuwa Machi 26, 2022 ameitaka BASATA kuhakikisha inatenda haki ili kupata kazi zenye viwango bora.
"Natambua huko nyuma kumekuwa na malalamiko naomba niwaonye, mimi katika kipindi changu hakutakuwa na tuzo za msongo,"amesisitiza Mhe Mchengerwa.

Amewashauri wasanii wawe na mazoea ya kujisajili COSOTA ili kazi zao ziweze kutambulika na waweze kunufaika na kazi hizo.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Pauline Gekul amesema sekta za utamaduni, sanaa na michezo zina umuhimu mkubwa kwa taifa ndiyo maana kutokana na umuhimu huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliamua kuziundia wizara hiyo huku akitoa sekta ya habari.
Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt. Hassan Abbasi amesema Serikakli imefufua tuzo za muziki baada ya miaka saba kutokuwepo hivyo wadau wa sanaa kwa kushirikiana na Serikali wana wajibu wa kuzilinda na kuzienzi ili ziendelee kuwanufaisha.
Naibu Katibu Mkuu, Saidi Yakubu amesema sekta ya sanaa inagusa maisha ya wananchi wote wa Tanzania kwa namna moja au nyingine hivyo wizara itahakikisha inaandaa mazingira bora ili wasanii waweze kunufaika na kuboresha maisha yao.
Katika tukio hilo Mhe. Mchengerwa amewaongoza mamia ya wadau waliohudhuria hafla hiyo kuimba wimbo wa hongera mwanangu wa Bibi Titi Mohamed huku akifafanua kwamba toka enzi za ukoloni muziki ulitumika katika ukombozi wa Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news