Waziri Bashungwa ampa 'saluti' Rais Samia, atoa maagizo mazito

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Innocent Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kupitia fedha ambazo alizitafuta na kuzipata kutoka Benki ya Dunia ili ziwezeshe kupendezesha mitaa mbalimbali.
Vijana wakiwa kazini ujenzi daraja la juu maeneo ya Magomeni Mikumi, mradi huo unatarajiwa kukabidhiwa mwezi Machi, mwaka huu. Daraja hilo ni kiunganishi cha barabara ya Magomeni Mapipa- Urafiki (kilomita 7.31) ambapo inatarajiwa kupunguza msongamano.
Mheshimiwa Bashungwa ameyasema hayo leo Januari 27, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na fedha za mikopo kutoka Benki ya Dunia baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo Mradi wa Kuendeleza Miji Mkakati (TSCP), Mradi wa Ukuzaji na Uboreshaji wa Miji (ULGSP) na Mradi wa Uboreshaji na Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP).

Taarifa ambazo zimewasilishwa kwake na kikosi kazi kinachosimamia miradi hiyo inayotekelezwa kwa fedha hizo na kusimamiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

"Na katika hili Mheshimiwa Rais ametuagiza, jitihada kubwa za kuhakikisha majiji yetu yanakuwa safi, iendane na kuhakikisha mitaa inatengewa fedha kwa ajili ya kuboresha barabara za mitaa, kama mnavyoona Mwananyamala haikuwa hivi, lakini kwa jitihada kubwa ambazo Mheshimiwa Rais wetu anazifanya,ametenga fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha mawasiliano ya bararabara za mijini na vijijini.

"Na kama mmekuwa mkifuatilia kuna ziara nimekuwa nikifanya vijijini kuangalia kazi za TARURA wanazozifanya kwa ajili ya kuboresha barabara..kazi ni nzuri, na sasa hivi ninafanya ziara katika majiji kuangalia fedha ambazo Mheshimiwa Rais alituwezesha kama zimefanya kazi iliyokusudiwa

"Nimpongeze Mheshimiwa Mstahiki Meya, Mheshimiwa Mbunge Tarimba pamoja na Mkuu wa Wilaya (Wilaya ya Kinondoni) kwa kusimamia vema fedha ambazo alizileta Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara kwenye mitaa yetu,"amefafanua Mheshimiwa Bashungwa.

Pia amebainisha kuwa, kwa mujibu wa maelekezo ya Rais Samia ni kwamba barabara hizo zikiwekwa lami zitasaidia kupunguza msongamano wa foleni na kuwarahisishia wananchi kuwahi katika kazi zao za kila siku kwa haraka.

"Na maelekezo ya Rais ni kuhakikisha kuwa,tunazipa kipaumbele barabara ambazo zinapunguza msongamano wa watu na pia zinaunganisha miundombinu ya mwendokasi. Lakini pia, leo ni siku ya kuzaliwa kwa Mheshimiwa Rais wetu, nitumie nafasi hii kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, ninamuombea maisha marefu ili azidi kuliongoza Taifa letu na tunaona namna ambavyo maendeleo yanakuja kwa kasi,"amesema Waziri Bashungwa.
Aidha, amesema kuwa watasimamia ipasavyo maelekezo ambayo amewapatia na wataendelea kuhakikisha fedha ambazo anazileta kwa wingi kuhakikisha mawasiliano ya barabara katika majiji, manispaa, halmashauri za miji pamoja na halmashauri zinasimamiwa ipasavyo.

Mpango Kabambe

Pia, Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,Innocent Bashungwa amesema uhitaji wa kuwa na Mpango Kabambe (Master Plan) kwa sasa ni wa halmashauri zote na sio zile zenye mradi tu nchini.

Kwa nini Mpango Kabambe

Ripoti za kitafiti zinaelea kuwa,miji ikiwa na makazi yasiyopimwa na holela ni kichocheo moja wapo cha kuchelewesha maendeleo ya kijamii, kiuchumi, kimazingira katika miji na vitongoji vyake.

Hivyo, suluhisho la hayo yote ni kuwa na Mpango Kabambe ambao ni nyenzo muhimu katika kuokoa gharama nyingi ambazo Serikali imekuwa ikipoteza ukiwemo muda pale inapotaka kutekeleza miradi ya maendeleo.

Kwa mujibu wa UN-Habitat (2003), maeneo yaliyojengwa ovyo ovyo yanafahamika kwa kukosa maji salama, usafi wa mazingira na miundombinu mingine, msongamano, hali ya makazi isiyo salama na ujenzi wa nyumba wa kiwango cha chini. 

Serikali ya Tanzania inaamini kuwa, utekelezaji wa Mpango Kabambe kwa kila halmashauri nchini utawezesha upimaji wa maeneo ambao utaendana pamoja na uendelezaji wa miundombinu na huduma muhimu katika maeneo yanayopimwa ikiwemo maji, umeme na barabara.

Waziri Bashungwa

Akipokea taarifa hiyo, Mheshimiwa Bashungwa amesema, "katika taarifa yenu nimesikia kuwa Mpango Kabambe (Master Plan) imeandaliwa kwenye halmsahuri zilizonufaika na mradi tu kwenye miji 18, majiji na manispaa pamoja na halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam, lakini kwa namna miji yetu inavyokua kwa kasi Mpango Kabambe inatakiwa kuandaliwa kwenye halmashauri zote nchini, hivyo mjenge hoja kwenye miradi inayokuja ili halmashauri zilizobakia nazo ziweze kuwa na Master Plan.

"Kwa sasa lazima Serikali tuwe mbele ya mipango ya wananchi, tupange miji yetu mapema ili wananchi wakute mpango wa matumizi bora ya ardhi na kusitokee athari yeyote baadae ya kiuchumi au kisaikolojia kwa wananchi.

Usafi muhimu

Wakati huo huo, Waziri Bashungwa amewaagiza wakuu wa mikoa pamoja na wakuu wa wilaya zote nchini kuhakikisha wanasimamia suala zima la usafi hususani katika miradi yote ya barabara, masoko na stendi inayoendelea kujengwa katika maeneo yao.

Mheshimiwa Bashungwa ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake katika miundombinu inayojengwa kwa fedha za mkopo wa Benki ya Dunia jijini Dar es Salaam huku ikisimamiwa na TARURA ambapo amebaini kuwa, suala la usafi katika maeneo mengi limekuwa changamoto, hivyo inahitajika nguvu ya pamoja kwa maana ya Serikali na wananchi ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Waziri Bashungwa alionekana kuumizwa zaidi na tabia ya baadhi ya wananchi kutupa taka ovyo katika miundombinu pamoja na Bonde la Jangwani ambalo linaunganisha Mto Mzimbazi ambapo alishuhudia taka ngumu nyingi zikielea katika maji, jambo ambalo amesema linahitaji misingi mizuri ili kila mmoja atambue thamani ya usafi.

Amesema, wizara yake itaangalia namna ambavyo itashirikishana mawazo na Wizara ya Elimu ili kuona ni kwa namna gani wanawajengea uelewa zaidi wanafunzi kuhusu umuhimu wa usafi, hatua ambayo itaongeza hamasa ya kila mmoja kupenda usafi kuanzia shuleni na nyumbani.

Amesema, haipendezi kuona barabara, masoko na stendi zilizojengwa kwa gharama kubwa tena kwa fedha za Serikali zikiwa chafu huku akitaka elimu iendelee kutolewa zaidi kwa wananchi hatua itakayosaidia kuondokana na tatizo hilo.

Waziri Bashungwa pia amesisitiza azima ya Serikali kujenga daraja la juu litakaloanzia eneo la Magomeni hadi Fire na kusema kuwa ujenzi wake utasaidia changamoto iiloyopo eneo hilo hususani mafuriko hasa nyakati za mvua kufikia kikomo.

Shukurani

Kwa nyakati tofauti Mkuu wa Mkoa wa Kinondoni, Mheshimiwa Godwin Gondwe na Mstahiki Meya wa Kinondoni Songoro Mnyonge wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha ambazo zimeendelea kuipendezesha mitaa mbalimbali wilayani humo hususani kwa upande wa barabara na mitaro.

Wamesema, miundombinu hiyo mbali na kupendezesha mji pia ni suluhisho la changamoto ya muda mrefu ya baadhi ya maeneo kuzingirwa na maji na hata kuchangia uharibifu wa mali za wananchi nyakati za mvua.
Pia wamesema, wataendelea kusimamia fedha hizo ili zitekeleze miradi yenye ubora mkubwa na thamani yake iendane na fedha husika. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news